Friday, November 30, 2018

DKT. NDUGULILE ASIKITISHWA NA UTENDAJI KAZI SEKTA YA AFYA NA MAENDELEO YA JAMII TANGA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na watendaji wa Wilaya ya Lushoto wakati wa ziara yake mkoani Tanga kufuatilia utekelezaji wa utoaji huduma katika Sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akipokea zawadi ya ua kutoka kwa mmoja wa mtoto anayeishi katika makao ya kululelea watoto yatima na wenye shida ya Irente yaliyopo Lushoto mkoani Tanga wakati wa ziara yake mkoani humo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akiwa amembeba mmoja wa mtoto anayeishi katika makao ya kululelea watoto yatima na wenye shida ya Irente yaliyopo Lushoto mkoani Tanga wakati wa ziara yake mkoani humo. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesikitishwa na utendaji kazi usioridhisha katika Sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii kwa mkoa wa Tanga kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri katika utekelezaji wa majukumu yao 

Ameyasema hayo leo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga alipofanya ziara ya kujionea shughuli zinazosimamiwa na Wizara yake katika Sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii na kukuta baadhi ya maafisa wahusika wakiwemo Waganga Wakuu wa Wilaya na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Lushoto hawapo katika ziara yake.. 

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya Wilaya ya Lushoto amesema kuwa watendaji wa Wilaya hiyo hawako makini katika kutekeleza majukumu yao na hakuna usimamizi wa moja kwa moja katika kuhakikisha mambo yanaenda wilayani hapo. 

“Nimesikiliza taarifa sijaona masuala ya Maendeleo ya Jamii na pia Afisa Maendeleo ya Jamii hayupo hapa na nimetembeela na Wilaya nyingine Waganga Wakuu wa Wilaya hawakuwepo hii inaonesha hamko makini katika kazi yenu” alisisitiza Dkt. Ndugulile 

Dkt Ndugulile amesema usimamizi na uwajibikaji ni njia pekee itakayowezesha kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu katika Sekta zilizopo na hapo baadae itabidi kila awajibike katika ngazi yake ya uteuzi iwapo hatashindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo. 

Ametolea mfano katika taarifa ya Wilaya iliyosomwa kwake kuwa kuna baadhi ya vituo vya afya vilivyopokea hela ya ujenzi na ukatarabati wa vituo hivyo havijakamilika na vingine kutokuwa na milango ikiwa Wilaya ya Lushoto ni wazalishaji wa mbao na kusema kuwa taarifa aliyopokea imeegemea katika Sekta ya Afya na kusahau Sekta ya Maendeleo ya Jamii ambayo inasimamia masuala muhimu ikiwemo mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni. 

Naibu Waziri Ndugulile ameupa uongozi wa Wilaya ya Lushoto mwezi mmoja kukamilisha kuweka milango katika majengo yote yaliyopo katika vituo vya Afya vilivyopokea fedha ya ujenzi na ukarabati jumla ya Shillingi Billioni 1.4. 

Aidha Dkt. Ndugulile ameagiza kufanyika kwa marekebisho kasoro ndogo ndogo za kitaalam katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma bora kwa wananchi wa Wilaya hiyo. 

Akitoa maombi kwa niaba ya wananchi wa Lushoto mbele ya Naibu Waziri Ndugulile, Mbunge wa Jimbo la Lushoto Mhe. Shaban Shekilindi ameomba kupatiwa gari ya kubeba wagonjwa vifaa vya X Ray pamoja na kuogezewa watumishi ili kuendana na kasi ya utoaji wa huduma za afya katika Wilaya ya Lushoto. 

Naibu Waziri Ndugulile amemaliza ziara yake ya Kikazi ya Siku kadhaa katika Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga katika kufuatilia utendaji kazi katika Sekta ya Afya na Maendelo ya Jamii.

No comments: