Thursday, November 29, 2018

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WAJENGEWA UWEZO KUHUSU OPRAS


Na Mwandishi Maalum, Dodoma

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt Evaristo Longopa amesema, Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya utendaji wa Kazi ( OPRAS) utasaidia sana katika kuwapima watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Dkt. Longopa ameyasema hayo hivi karibuni wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya uwezeshaji kuhusu mfumo wa OPRAS kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mafunzo hayo yaliwahusisha Manejimenti, Mawakili wa Serikali na watumishi wa kada nyingine na yalifanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Jijini Dodoma.

Katika mafunzo hayo, pamoja na watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuelimishwa Sheria na Nyaraka mbalimbali zilizoanzisha OPRAS pia walielimishwa kuhusu umuhimu wa kila mtumishi katika utumishi umma wa kujaza fomu ya OPRAS kila mwaka kwa kushirikiana na Mkuu wake wa Kazi na kwamba zoezi hilo linatakiwa kufanyika kwa uwazi.

“ Katika vikao vyetu vya menejimenti, tulikubaliana kwamba, upo umuhimu wa zoezi la upimaji na tathmini ya utendaji kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Zoezi hili litatusaidia sana katika kujipima na kuwapima walio chini yetu ilikufikia malengo ambayo Ofisi yetu imejiwekea na hatimaye malengo ya Serikali kwa ujumla”. Akasema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Akasisitiza menejiment na watumishi wote kuyazingatia mafunzo hayo kutokana na umuhimu wake na kwamba ni haki na wajibu wa kila mtumishi wa Ofisi yake kufanyiwa tathimini na kupimwa kuhusu namna anavyotekeleza majukumu yake kwa kile alichosema upimaji huo unamanufaa kwa mtumishi binafsi pia.

Wawezeshaji wa Mafunzo hayo walitoka Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Katika mafunzo hayo watumishi walisisitizwa juu ya umuhimu na haja ya kuyafahamu majukumu yake ambayo ndiyo atakayopimwa nayo pamoja na kuwa na mkataba ambao mtumishi atakuwa ameingia na kiongozi wake kabla ya kuanza kutekeleza malengo ambayo Idara au Kitengo imejiweka kwa mwaka huo.

Na kwamba upimaji na tathimini ya utendaji kazi pia husaidia kubainisha changamoto mbalimbali ambazo kwa namna moja zinakwamisha utekelezaji kwa ufanisi wa malengo ambayo Taasisi imejiwekea na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.

Kwa mujibu wa Bi. Zainabu Kutengezah . Ujazaji wa fomu ya OPRAS ni muhimu sana kwa mtumishi wa umma na zoezi hili ni la kisheria kwa kuwa linasimamiwa na sheria , Waraka na kanuni mbalimbali za utumishi wa umma. Na ni zoezi linalotakiwa kufanyika katika mazingira ya uwazi baina ya mtumishi na kiongozi wake.

Wakati wa mafunzo hayo watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ikiwa ni pamoja na zoezi la vitendo la namna bora na sahihi ya kujaza fomu ya OPRAS.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya OPRAS kwa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikakali. Mafunzo hayo yalihusisha Menejiment, Mawakili wa Serikali na Watumishi wa kada nyingine . Walioketi nyuma ni wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Zainabu Kutengezah na Bi. Shomi Mongi.
Bi. Susan S. Kalele ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Raslimali watu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akitoa maelezo kwa Menejiment kuhusu mfumo wa OPRAS
Wakili wa Serikali Bi. Juliana Mnisi akiuliza swali kwa wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Bi Dorina Kalumna akitoa maelezo kwa watumishi wenzie jinsi ya kufikia ukokotoaji wa alama ambazo mtumishi na kiongozi wake wanakuwa wameafikiana wakati wa ujazaji wa fomu ya OPRAS.

habari na picha kwa hisani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali

No comments: