Saturday, November 3, 2018

NIMERIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA SGR-MAJALIWA*Ni baada ya kuhakikishiwa kipande Dar-Morogoro kitakamilika Aprili 2019 badala ya Julai

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa mfumo wa reli ya kisasa (SGR) inayojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi.

Amesema kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa km. 300 ambacho kilitakiwa kukamilika Julai 2019, wataalamu wamesema watakamilisha Aprili 2019.Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Novemba 3, 2018) alipotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia eneo la Shaurimoyo Dar esSalaam hadi Soga, Pwani.

“Nimeridhishwa na viwango na maendeleo ya ujenzi kwa sehemu ulivyofikia pamoja na ushiriki wa Watanzania wengi katika mradi huu, tunataka muendelee kujenga kwa kasi hii.”Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona malengo ya Rais Dkt. John Magufuli ya kutaka kuona SGR inakamilika na kuanza kutumika nchini yanatimia.

Kuhusu suala la ajira, Waziri Mkuu amesema amefarijika kusikia asilimia 96 ya watu walioajiriwa katika mradi huo ni Watanzania, amewataka wawe mabalozi wazuri.“Watanzania mnaofanya kazi katika mradi huu hakikisheni mnawajibika kwa kufanyakazi kwa bidii, uaminifu na muwe mabalozi wazuri ili wengine waweze wapate ajira.”

Awali,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya mradi huo wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora unagharimu sh. trilioni 7.1.Alisema mradi wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa km 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza umegawanyika katika vipande vitano, kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu km 300 na kitagharimu sh. trilioni 2.7.

“Kipande kingine ni kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa km. 422 ambacho kitagharimu sh. trilioni 4.4, Makutupora hadi Tabora km. 376.5, Tabora hadi Isaka km 162.5 na Isaka hadi Mwanza km. 311.25.”Mkurugenzi huyo alisema kukamilika kwa reli hiyo ya kisasa kutachochea mipango ya Serikali katika kutekeleza sera ya viwanda na kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Pia reli hiyo itachochea mapinduzi ya kiuchumi kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususan kwa nchi zisizopakana na bahari kwani watasafirisha mizigo yao kwa haraka na uhakika.Akizungumzia mradi huo kwa ujumla, Kadogosa alisema maendeleo ya mradi huo ni asilimia 32 kwa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro na asilimia 3. 31 kwa kipande cha Morogoro-Makutupora.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, NOVEMBA 3, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli Tanzania  (TRC), Masanja Kadogosa kuhusu ujenzi wa Reli ya SGR wakati alipotembelea kambi ya Kampuni ya Yapi Markezi inayojenga Reli hiyo,  katika eneo la Shaurimoyo jijini Dar es salaam, Novemba 3, 3018
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua maandalizi ya  ujenzi wa madaraja  ya  kupitisha treni  juu  wakati alipotembelea kambi ya Kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga reli ya Kisasa ya SGR   Oktoba 3, 2018. Kambi hiyo ipo eneo la Shaurimoyo jijini Dar es salaam. Wapili kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua kazi ya utengenezaji mataluma ya reli ya SGR wakati alipotembelea Kambi ya Kampuni ya Yapi Merkezi katika eneo la Soga mkoani Pwani, Oktoba 3, 2018. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua utandikaji wa  reli ya SGR katika eneo la Soga mkoani Pwani, Oktoba 3, 2018.  Wapili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua utandikaji wa  Reli ya SGR katika eneo la Soga mkoani Pwani, Oktoba 3, 2018.   Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe. 
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua utandikaji wa  Reli ya kisasa ya  SGR katika eneo la Soga mkoani Pwani, Oktoba 3, 2018.   Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe na kulia kwa Waziri Mkuu ni Mkurugenzi Mkuu wa Shiraki la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na  wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga reli ya kisasa ya SGR kati ya Dar es slaam na Morogoro baada ya kukagua ujenzi wa reli hiyo katika eneo la Soga mkoani Pwani,  Oktoba 3, 2018.  Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

No comments: