Saturday, November 3, 2018

NGARIBA WABADILI MBINU ZA UKEKETAJINaibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile pamoja na Kaimu Katibu Tawala wa MKoa wa Mnyara Bw. Anza-Amen Ndossa wakionesha Wajumbe wa Kamati ya Dawati la Ulinzi wa Wanawake na Watoto Mkakati wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MATAKUWA) mara baada ya kuzindua kamati ya hiyo ya Mkoa jana katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu Mkoa Manyara.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akikata utepe kuzindua Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto jana katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu Mkoa Manyara pembeni yake ni KaimuKatibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bw. Anza-Amen .Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJWNa Mwandishi Wetu Manyara.

Mangariba nchini wamebuni njia mpya za kuendeleza vitendo vya ukeketaji nchini kwa kutofanya sherehe wakati wa ukeketaji lakini pia kukeketa watoto wachanga na kufanya vitendo ua ukeketaji nyakati za usiku.

Hayo yamesemwa Wilayani Babati Mkoani Manyara na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akizindua Kamati za Ulinzi kwa Wanawanke na Watoto kwa mkoa wa Manyara.

Naibu Waziri Ndugulile amesema kuwa kuanzia Januari mpaka Septemba 2017 jumla ya vitendo 41,000 vya ukatili viliripotiwa na jeshi polisi nchini akifafanua kuwa kama takwimu hizi zingekuwa za ujambazi katika mkoa mmoja hali ya wananchi ingekuwa mbaya sana huku akiviita vitendo hivyo na ujambazi katika sura mpya. Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imejipanga kutokomeza vitendo vya Ukeketaji kwa kuanzisha Mpango Mkakati wa kutokomeza Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2016/2017 utakaoisha mwaka 2021/2022.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa kwa mujibu wa Takwimu inaonyesha Mkoani wa Manyara una Asilimia 27 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hivyo nguvu inahitajika sana katika kupambana na vitendo hivyo akiitaka kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kuweka suala hilo katika mipango yao ili kudhibiti ukatili huo.

Naibu Waziri Ndugulile amewataka wajumbe wa Kamati ya Ulinzi kwa Wanawake na Watoto aliyoizindua jana mkoani humo kusoma na kuelewa majukumu yao kama ilivyabainishwa katiaka mkakati wa MTAKUWA kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Mkoani Manyara.

Akitoa taarifa ya Ukatili wa Kijinsia Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Manyara Bi. Anna Fisso amesema kuwa mila zisizofaa zimekuwa zikiongeza vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Babati kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Elizabeth Kitundu amaahidi kufuatilia utendaji kazi wa Kamati hiyo ili iweze kufanya kazi ili kuondokana ama kufuta kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Akizungumza mmoja wa Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto akimwakilisha Sheikh wa Mkoa wa Manyara Sheikh Abdallah Suleiman amesema kuwa wao kama viongozi wa kiroho wanatumia ushawishi wao kutoa elimu kwa wananchi kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ili kupunguza vitendo hivyo.

Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile yupo katika ziara ya Siku 3 Mkoani Manyara katika kukagua utoaji huduma katika Sekta ya Afya, Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

No comments: