Saturday, November 3, 2018

ARUSHA KUJA NA VITUO 4 MAALUMU VYA POLISI VILIVYOGHARIMU ZAIDI YA MIL. 80

Na Vero Ignatus, Arusha.

Kikao cha Sekta ya wadau wa Utalii kimefanyika Mkoani Arusha kikiwa na lengo la kuona namna wanatekeleza azimio la kusimika vituo vinne Maalum vya Polisi kwa ajili ya Ukaguzi wa magari yanayosafirisha watalii.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ambapo Mkuu wa mkoa Mrisho Gambo amesisitiza azma yake katika kuhakikisha utalii unatengenezewa mazingira mazuri ya ukuaji.“Hakuna kitu kinatupa sifa mbaya kwa wageni kama kusimamishwa na askari kila baada ya kilomita moja''alisema Gambo

Amesema Vituo hivyo maalum vya ukaguzi vitasaidia kuondokana na changamoto hiyo kwakuwa sekta ya utalii inategemewa sana katika kuliingizia taifa pato ."Magari yote yatakua na vituo maalum vya ukaguzi, tunafanya yote haya kwakua sekta ya utalii tunaitegemea sana kama taifa kwa kutuingizia pato la taifa.” Alisema Gambo.

Vituo hivyo vinne vinavyogharimu zaidi ya shilingi Milioni 80 vimetengenezwa kwa michango ya wafanyabiashara ya Utalii TATO na vinatarajiwa kuwekwa katika maeneo ya Kikatiti, Ngaramtoni, Makuyuni na Karatu.

Kwa upande wa serikali kupitia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na TANAPA, Mkurugenzi mkuu wa hifadhi za Taifa Dr. Kijazi amesema wao kama wadau wa mkubwa wa sekta hii wanaunga mkono wazo hili na wako tayari kuhakikisha taasisi zao zinajenga vyoo katika vituo hivi.“Sisi kama hifadhi za Taifa ni wanufaika namba moja endapo sekta hii inaboreshewa mazingira, na kwa kuunga mkono jitihada hizi mimi na wenzangu wa mamlaka ya Ngorongoro tunaahidi kujenga vyoo katika vituo vyote vinne kwa kushirikiana na ofisi za wakuu wa wilaya” alisema Kijazi.

Kwa niaba ya wafanyabiashara ya utalii Bwana Sirili Nko ambaye ni Katibu wa TATO, ametoa pongezi kwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha kwa kuonyesha juhudi za kUkuzaji na kUboresha sekta ya Utalii Mkoani Arusha.Toka kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha Gambo amefanya jitihada nyingi za kuboresha sekta ya utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo.
Kutoka kushoto ni mhifadhi mkuu wa mamlaka ya Ngorongoro Dkt. Fredy Manongi akifuatiwa na Mkurugenzi wa TANAPA Dr. Alan Kijazi
Wamiliki wa makampuni ya Utalii wakifuatilia mjadala wa kuweka vituo maalumu vya polisi mkoani Arusha.
Mdau wa Sekta ya Utalii wakitoa maoni yao juu ya zoezi la uwekaji wa vituo maalum vya polisi.
 

No comments: