Friday, November 23, 2018

NAIBU WAZIRI TAMISEMI AHIMIZA WAFANYABIASHARA WENYE VIWANDA KULIPA KODI

Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI) Mwita Wairata amewasisitiza wafanyabiashara na wenye Viwanda nchini kulipa kodi ya maendeleo ili Serikali iwe na uwezo wa kufanya miradi ya kimaendeleo ambayo itasaidia wananchi wengi.

Waitara ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa kuelekea katika kilele cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo(TCCIA) ambapo amesema ili Serikali iongeze ufanisi katika kuhudumia jamii wafanyabiashara na wawekezaji katika maenneo mbalimbali wanapaswa kulipa kodi ya mapato ambayo pamoja na kusaidia uongezwaji wa miradi ya maendeleo pia itaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Amesema chama hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Taifa na kuunga mkono juhudi za Seikali ya Awamu ya tano ya Rais Dk.John Magufuli inayosisitiza uchumi wa Viwanda.“Wafanyabiashara lipeni kodi ya maendeleo, Kodi ndio itatufanya kuwawekea mazingira mazuri ya uwezeshaji na hatimaye mfanye biashara zenu kwa ufanisi mkubwa, sisi tutaendelea kuwawezesha kwani chama chenu ni muhimu sana katika kukuza ustawi wa kijamii,"amesema Waitara.

Kwa upande wake Kaimu Rais TCCIA Octavian Mshiu amsema kwa muda wa miaka 30 Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha wawekezaji waliopo katika chama hicho wanaongeza shughuli zao na kusababisha mafanikio makubwa.Amesema katika Serikali ya awamu ya tano kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wanachama wake wa kuanzisha viwanda na kufungua biashara kubwa na hivyo kuiomba Serikali kuzidi kuwashauri kwenye masuala mbalimbali ya kuwekeza ili kufikia uchumi wa kati.

Pia TCCIA imefungua matawi yake katika Nchi za China na Uturuki ili kupanua shughuli zake na kuwawezesha Wafanyabiashara, Wakulima na wenye viwanda kufanya biashara zao kimataifa zaidi ambapo Mkurugenzi wa Chamber ya China Martin Rajabu amesema wanapata ushirikiano mkubwa katika suala zima la kibiashara na raia wa nchini humo.

Chama hicho cha Wafanyabiashara, Wakulima na wenye Viwanda kilianzishwa rasmi mwaka 1988 ambapo kwa mwaka huu kinatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake na miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana na kuwaunganisha wafanyabiashara kimataifa,kuwajengea uwezo,kukuza mitaji yao na kuwawezesha kuimarisha viwanda,biashara na kilimo.

Naibu Waziri TAMISEMI Mwita Waitara (wa pili kushoto) akisalimiana na  Mkuu wa Kitengo cha Biashara benki ya KCB Masika Mkulu.Wa kwanza kushoto ni Kaimu Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo Octavian Mshiu.

No comments: