Monday, November 12, 2018

Msaada wa Tshs. 86 Mil kunufaisha Wagonjwa wa Saratani ya Koo Muhimbili

Mkurugenzi Mtendaji wa Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akipokea kifaa tiba cha aina ya STENTS kwa ajili ya wagonjwa wenye tatizo la saratani ya koo la chakula kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Boston Scientific ya Marekani, Troy Lengel. Wengine kushoto ni wawakilishi kutoka hospitali ya Muhimbili, Mayo Clinic ya Marekani na Chuo Kikuu cha San Francisco nchini Marekani na kulia ni wawakilishi kutoka MUHAS na Hospitali ya Muhimbili.
Pichani ni vifaa tiba aina ya STENTS ambavyo wagonjwa wenye tatizo la saratani ya koo la chakula wameanza kuwekewa ili kuwasaidia kumeza chakula kutokana na mfumo wa koo kuharibiwa na ugonjwa huo. 

…………………. 

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vifaa tiba aina ya Stents vyenye thamani ya Tshs. 86.2 milioni kutoka kampuni ya Boston Scientific ya Marekani kwa ajili ya wagonjwa wenye tatizo la saratani ya koo la chakula. 

Stents ni vifaa maalum mithili ya springi ambavyo vinaweza kuwa vya plastiki au chuma vyenye uwazi katikati wanavyowekewa wagonjwa wenye uvimbe kwenye koo lililoziba ili kupanua sehemu hiyo na kuruhusu kupitisha chakula. Kuna stents za aina mbalimbali kutegemeana na mgonjwa ana shida ya aina gani. 

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini, Dkt. Masolwa Ng’wanasayi amesema kampuni hiyo imetoa stents 25 ambazo zitatumika kwa wagonjwa 25 wenye satarani ya koo la chakula ili kuwasaidia kumeza chakula na kuendelea na matibabu ya mionzi. 

“Mgonjwa mwenye tatizo la saratani ya koo la chakula, anakuwa hawezi kumeza chakula na hali hii inasababisha mgonjwa kupungua uzito na kushindwa kuendelea na matibabu mengine, hivyo vifaa hivi vitawasaidia kumeza chakula na kuendelea na matibabu mengine,” amesema Dkt. Ng’wanasayi. 

Amesema kifaa tiba (Stent) kimoja hivi sasa kinauzwa Tshs. 3.4 milioni na kwamba kampuni hiyo imeahidi kupunguza bei hadi kufikia dola 100 za Marekani kwa kifaa tiba kimoja sawa na Tshs. 230,000. 

“Wameahidi kwamba watapunguza gharama za vifaa tiba hadi kufikia dola 100 za Marekani. Lengo ni kuhakikisha wagonjwa wengi wenye tatizo la saratani ya koo wanapatiwa matibabu,” amesema Dkt. Ng’wanasayi. 

Leo wagonjwa tisa wenye tatizo la saratani ya koo la chakula wamepatiwa matibabu ya kuwekewa kifaa hicho na baada ya matibabu hayo wameweza kumeza chakula vizuri na hivyo kurejea kwenye hali zao za kawaida. 

Kwa muda wa miaka miwili, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) na Hospitali ya Ocean Road kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Marekani, Chuo Kikuu cha San Francisco nchini Marekani na Kampuni ya Boston Scientific ya Marekani wamekuwa wakifanya utafiti wa kutumia kifaa tiba hicho kwa wagonjwa wenye tatizo la saratani ya koo la chakula. Utafiti huo, umebainisha kwamba matumizi ya kifaa hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wenye tatizo la saratani ya koo la chakula.

No comments: