Wednesday, November 21, 2018

MKUTANO MKUU APHFTA WAWAKUTANISHA WADAU, SUALA LA ADA NA USAJILI LATOLEWA MAJIBU

 Leandra Gabriel, na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii

SERIKALI imesema ipo katika mpango wa kutengeneza muongozo ambao utasaidia katika utoaji huduma kwenye hospitali binafsi ikiwemo suala la ongezeko la gharama ambazo zinawafanya wananchi wa kawaida kushindwa kupata huduma.

Mkurugenzi wa tiba, Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema hayo leo Novemba 20.2018 wakati wa uzinduzi wa mkutano wa 19 wa wadau wa afya na hospitali binafsi.

Amesema kuwa muongozo huo utasaidia hospitali binafsi ambazo hutoa huduma kwa gharama kubwa kuacha kuwabagua wagonjwa wa dharula kwani ni lazima afya ya mtu ije kwanza."Tunashughulikana hospitali zenye tozo kubwa kwa wagonjwa, kwani ni sawa kwao kuweka gharama zao kutokana na mfumo wa kutibu magonjwa maalumu, ni sawa kwa hospitali hizo kuwa na gharama zao ila kwa magonjwa ya dharura lazima huduma zitolewe bila kuangalia hadhi ya hospitali hizo" ameeleza Dkt. Gwajima.

Aidha amesema kuwa malengo ya kufanya mkutano huo ni kujadili juu ya kuimarisha utoaji wa huduma katika vituo vyao vya kutolea huduma.Dkt. Gwajima amesema kuwa sekta binafsi zinamiliki asilimia 40 za utoaji wa huduma za afya nchini na pia wanashiriki sana katika utoaji ajira na wao kama serikali wanatambua mchango wao na changamoto zao lazima wazifanyie kazi.

Aidha amesema kuwa kuwa sekta binafsi ni muhimu na pasipo sekta binafsi utoaji wa huduma za afya hazitaweza kutekelezeka kwa ubora hivyo lazima kuwepo na mabadiliko katika mtazamo chanya wa kusimamia sera za afya.Amesema kuwa bado serikali inaendeleza mikakati ya kuongeza wataalam wa afya katika vyuo mbalimbali ili kuongeza huduma bora katika vituo vya afya nchini.

Na amewataka kuwa na umoja ili kuweza kusaidia agenda ya Tanzania katika kuboresha sera ya afya nchini ambayo ni moja kati ya vipaumbele kwa serikali ya awamu ya tano.Aidha amesema kuwa wamepokea maelekezo kutoka Wizara ya afya katika kuhakikisha bodi zinazosajili maabara na vituo afya na zahanati kuwa kitu kimoja katika utendaji na kuhakikisha ada zinazolipwa ni tatu pekee na watoa huduma wataokikiuka hilo APHFTA litoe taarifa ili wachukuliwe hatua.

Pia amewataka sekta binafsi kutimiza majukumu yao na vituo vyote viwe vilivyojiandikisha na kusimamiwa vizuri na serikali bado ina imani nazo kwa kuwa zina mchango mkubwa katika sekta ya afya.Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa APHFTA Dkt. Samwel Ogillo amesema kuwa hicho ni kikao chao cha mwaka ambapo kimewakutanisha wadau wa sekta binafsi na umma na kujadili namna ya kuimarisha sekta ya afya.

Dkt. Ogillo amesema kuwa changamoto kubwa ilikuwa ni katika usajili wa vituo na maabara na wamefurahi kusikia kuwa ni ada tatu pekee ndizo wanazotakiwa kulipa na kuwa na taasisi moja ya kusimamia usajili wa vituo hivyo.

Pia amesema kuwa suala la tozo katika kununua bidhaa nchini litawarahisishia katika mchakato wa kutoa huduma kama urasimu ukikoma kwa kuwa kuaagiza vifaa nje ya nchi kunachangia katika upandishwaji wa gharama za matibabu katika hospitali binafsi.

Afisa mtendaji wa wanachama wa wamiliki binafsi wa vituo vya afya Dkt. Samwel Ogillo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo ambao umejikita zaidi katika kujadili namna ya kuimarisha zaidi sekta ya afya nchini .
Mwenyekiti wa chama cha wamiliki binafsi wa vituo vya afya nchini (APHFTA) Dkt. Kaushik Ramaiya (kushoto) wakifuatilia mjadala uliozinduliwa na Mkurugenzi wa tiba leo jijini Dar es salaam, kulia ni Afisa mtendaji wa APHFTA Dkt. Samwel Ogillo. (Picha na Erick Picson, Blogu ya jamii)
Mkurugenzi wa tiba kutoka Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati akifungua mkutano wa 19 wa wanachama na wamiliki binafsi wa vituo vya afya leo jijini Dar es salaam.

Baadhi wa wadau wa sekta binafsi na umma walioshiriki mkutano huo, wakifuatilia mjadala wa ufunguzi wa mkutano wa 19 wa wanachama na wamiliki binafsi wa vituo vya afya, zahanati na maabara.

No comments: