Wednesday, November 21, 2018

DKT. MPOKI AKEMEA TABIA YA ABIRIA NA MADEREVA KUCHIMBA DAWA MAENEO YASIYOHUSIKA

NA WAJMW-DODOMA

Madereva wa mabasi yaendayo mikoani na abiria wametakiwa kuacha tabia ya kujisaidia “Kuchimba dawa” katika maeneo yasiyo rasmi ili kutunza na kuepuka uharibifu wa mazingira unaoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja kusababisha magonjwa ya milipuko.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua mkutano unaojumuisha Maafisa Afya kutoka mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini pamoja na wadau wa mazingira, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Dkt. Mpoki amekemea tabia hiyo hatarishi kwa ustawi wa mazingira huku akiwataka maafisa Afya na wadau wa mazingira nchini kusimamia afua zilizowekwa zinaendelea kutekelezwa ili kulinda mazingira ambayo yanatuzunguka.

“Kuna watu wengine nimeshawahi kuwaona kwenye basi wanatupa taka ovyo na mabasi mengine yanasimama porini ili abiria wajisaidie, hii tabia siyo nzuri na inatakiwa ikemewe kwa nguvu zote, Idara ya Kinga Pamoja na wadau wao wanakuja na mpango mkakati wa kuondoa kabisa dhana ya watu kusimama kujisaidia porini, "sisi tunatakiwa kuwa msitari wa mbele kupiga marufuku mabasi kusafiri bila kuchafua mazingira”.

Dkt. Mpoki amesema ni aibu kubwa kwa taifa kuona watu hawafuati kanuni za usafi huku akiwataka Maafisa Afya kuhakikisha wanafanya kazi kwa nguvu ili ionekane kuwa kero kwa watu wengine na watakaobainika kuchafua mazingira wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.

Aidha, Dkt. Mpoki ameongeza kuwa jamii inatakiwa kuzingatia matumizi ya vyoo bora na kunawa mikono mara baada ya kujisaidia ili kuepuka magonjwa ya milipuko yanayoweza kusababishwa na tabia ya uchafu ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kujisaidia ovyo porini ili kaulimbiu ya “Nyumba ni Choo” iweze kutekelezwa ipasavyo kwa kujenga vyoo vya kisasa katika maeneo mbalimbali ili huduma ipatikane mahala pote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema takwimu zinaonesha kaya zilizokua na vyoo bora mwaka 2012 zilikua asilimia 19.5 lakini hivi sasa nchi nzima kaya zenye vyoo bora ni asilimia 51.4.

Dkt. Subi amesema kutokana na takwimu hiyo inaonesha kuna mafanikio katika uhamasishaji kwa jamii kutumia vyoo bora na kuacha kutumia vyoo ambavyo havina viwango na salama kwa matumizi, na badala yake serikali inaendelea kutoa elimu na kusisitiza jamii kutumia vyoo bora ili kuepuka magonjwa yanayoweza kuzuilika ikiwemo kipindupindu, magonjwa ya tumbo na kuhara.

Pamoja na hayo, maafisa Afya wametakiwa kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma, kuhamasisha usafi wa mazingira na kufikia maeneo ya mazalia ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria ili kutokomeza ugonjwa huo ambao umekua hatari kwa jamii hasa kwa wanawake wajawazito na watoto.

Mkutano huo unaojumuisha Maafisa wa Afya nchi nzima una lengo la kutoa elimu na kubadilishana uzoefu wa kufanya kazi lakini msisitizo mkubwa ikiwa ni utunzaji wa mazingira na kuzingatia kanuni bora za afya pamoja na usafi wa mazingira na usafi na afya ya binadamu.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya akitoa neno mbele ya Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri pamoja na Wadau wa Mazingira leo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya akikagua maonesho ya vyoo baada ya kufungua kikao cha Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri pamoja na Wadau wa Mazingira leo jijini Dodoma katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete. 
 Maafisa Afya wa Mkoa na Halmashauri wakifuatilia kwa makini ufunguzi wa Mkutano wao uliofunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya leo jijini Dodoma katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete wenye lengo la  kusisitiza umuhimu wa mazingira. 
 Picha ya Pamoja ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya katika baada ya kikao cha  Maafisa Afya wa Mkoa, Halmashauri pamoja na Wadau wa Mazingira kilichofanyika leo jijini Dodoma.

No comments: