Wednesday, November 28, 2018

KITUO CHA KULEA WASICHANA (NHGO) CHAPOKEA MSAADA WENYE THAMANI YA ZAIDI YA MILION 10 KUTOKA FCS

Kwa kuwa vijana ndio nguvu kazi ya taifa ni vema kuwajengea misingi mizuri ya kupenda kujitolea kwa ajili ya jamii yao, Na ndio maana Foundation for Civil Society imeweza kuandaa mashindano kwa ajili ya vijana kutoa stori zao za namna walivyoweza kijitoa katika kusaidia jamii na mwisho kuwapa zawadi wenye story nzuri zaidi.
Hayo yamesemwa mapema jana na Afisa Uhusiano, Biashara na Maendeleo wa Taasisi ya Foundation for Civil Society Martha Olotu wakati akiongea na waandishi wa habari kwa Niaba ya Mkurugenzi wa FCS Bw. Francis Kiwanga katika Jumanne ya Kutoa (Giving Tuesday), ambapo kwa mwaka huu wameweza kutoa misaada katika kituo cha New Hope for Girls Center kilichopo kimara jijini Dar es salaam.Akielezea sababu za kuchagua kituo hicho afisa huyo amesema ni moyo wa upendo na wakujitolea alionao huyo Mama kwa kuwachukua mabinti wanaoishi katika mazingira hatarishi, Yatima, na walioterekezwa na familia zao na kuamua kuishi nao nyumbani kwake wakiwa ni kama sehemu ya familia yake na sio kama watoto ambao wapo kwenye kituo cha kulelewa.

Aliongeza kuwa mbali na tukio hilo la kuandaa mashindano kwa vijana, lakini pia kampeni hiyo ilitanguliwa na tukio la kijitolea damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa mbalimbali wenye uhitaji wa damu katika Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha MOI ambapo watu 38 waliweza kijitolea damu.

Aidha aliendelea kusema kuwa wametoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Milioni Kumi hii ikiwani FCS, wananchi mbalimbali, pamoja na mashirika mengine yaliyoguswa na tukio hilo, lakini kwa wafanyakazi wa Foundation for Civil Society wamejichanga na wametoa mashine ya Photocopy ikiwa ni kama njia ya kuacha alama katika kituo hicho.

Kwa upande wake Mama mlezi wa wasichana hao Bi. Consoler Eliya alisema kuwa sababu iliyomsukuma kufanya hivyo ni kutokana na ugumu wa maisha pamoja na mazingira hatarishi ambayo ameyapitia wakati akiwa msichana, Ikiwa ni pamoja na kupigwa sana, kukosa nafasi ya kusoma kutokana na magonjwa yaliyotokana na kipigo cha mara kwa mara.

Aliendelea kusema kuwa kutokana na vipigo ilifikia hata kwenda kufanyiwa upasuaji mara kadhaa, kulazwa stoo ya uchafu na kuamshwa kwa kumwagiwa maji, kufedheheshwa kwa maneno na matusi hali iliyosababisha kuishi kama omba omba mtaani na hata kulazimishwa kuolewa akiwa na umri wa miaka 11, na baada ya hayo yote alipiga goti kwa mungu na kumuomba akimsaidia atakuwa ni mama kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kama aliyopitia yeye.

Na kwa kumtegemea mungu aliweza kuvushwa katika majaribu hayo na ndipo alianza kumlea mtoto wa kwanza akiwa bado ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa kutumia Boom lake, na alipomaliza chuo alikuwa na wasichana saba na mpaka sasa yeye na mumewe wanawahudumia wasichana 40 na wawili wakiwa ni watoto wao wa kuwazaa wenyewe.

Naye Janeth Thobias ambaye ni miongoni mwa wasichana wanaolelewa na Mama huyo alisema kuwa sababu ya wao kuonekana ni wenye Amani na Furaha, ni kutokana na mafundisho mazuri anayowapatia na kila siku, lakini pia upenda kuwasihi wasahau yale waliyofanyiwa hapo nyuma eidha na ndugu au walezi wao na kuwakumbusha mara kwa mara kuwa silaha pekee itakayowakomboa katika maisha yao ni upendo.

Aliendelea kusema kuwa sababu nyingine ni malezi mazuri wanayopatiwa na Mama huyo, kwa kuishi nao kama sehemu ya familia yake na mara kwa mara anawasisitiza kuhusu umuhimu wa elimu na kuwataka wasome kwa bidii kwa kuwa elimu ndio msingi wa maisha yao.
Afisa Uhusiano, Biashara na Maendeleo wa Foundation for Civil Society Martha Orotu akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mapema jana jijini Dar es salaam katika siku ya Jumanne ya Kutoa (.Giving Tuesday).
Msichana Janeth Thobias ambaye ni miongoni mwa mabinti wanaolelewa katika kituo hicho akisoma Risala mbele ya wageni waalikwa mapema jana jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wasichana wa kituo cha New Hope for Girls Center wakiimba shairi mbele ya wageni waalikwa.
Edna Chilimo kutoka Foundation for Civil Society akiongea na Wasichana wa kituo cha New Hope for Girls Center.
Baadhi ya zawadi zilizotolewa kwa kituo hicho.
Zawadi nyinginezo.
Baadhi ya wasichana wa kituo cha New Hope for girls Center wakionyesha maonyesho ya mavazi mbele ya wageni waalikwa.
Baadhi ya washiriki wa Jumanne ya kutoa wakifuatilia matukio yanayoendelea katika tafrija hiyo.

No comments: