Friday, November 16, 2018

HUKUMU KESI YA MATUMIZI MABAYA INAYOMKABILI TIDO MHANDO KUTOLEWA DESEMBA 18 ,2018

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Desemba 18 mwaka huu inatarajia kutoa hukumu dhidi ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando.

Katika kesi hiyo, Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh.milioni 887.1.

Hakimu Mkazi Mkuu,Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo, amefikia hatua hiyo baada ya Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( Takukuru), Leonard Swai kuieleza Mahakama kuwa wamekwisha wasilisha majumuisho yao ya mwisho mahakamani hapo.

Naye Wakili wa utetezi wa Tido, Dk. Ramadhani Maleta ameiarifu Mahakama kuwa wakili mwenzake Martin Matunda ambaye walikuwa na wakimtetea Tido, amefariki dunia na lakini nao pia wamekwisha wasilisha hoja zao za mwisho.

Kutokana na taarifa hiyo Swai ameiomba Mahakama kuipangia Kesi hiyo tarehe ya hukumu ambapo Hakimu Shaidi amepanga kusoma hukumu hiyo Desemba 18, mwaka huu.Mwishoni mwa mwezi uliopita, Tido kupitia mawakili wake Martin Matunda na Dk Ramadhani Maleta walifunga ushahidi wa upande wa utetezi.

Katika kesi hiyo jumla ya mashahidi watatu wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo walitoa ushahidi na kufunga ushahidi wa upande wa mashtaka.Miongoni mwa mashahidi hao ni Afisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.

Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Juni 16, 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBCli hasara ya Sh887,122,219.19.

No comments: