Na Francis Godwin,Iringa
MWENYEKITI wa bodi ya shirika la umeme Tanzania (TANESCO ) Dkt Alexander Kyaruzi amesema kuwa hali ya uzalishaji wa umeme nchini ni nzuri na kuwa watanzania wasitegemee kuwepo kwa mgao wa umeme kwa mwaka huu.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji umeme kijiji cha Ndolezi katika Halmashauri ya mji Mafinga Dkt Kyaruzi alisema kuwa pamoja na kuwa kipindi cha kiangazi kinakwenda kumalizika ila hali ya maji katika vituo vya uzalishaji umeme vya Kidatu na Mtera ni nzuri na kuwa maji hayo yataendelea kuongezeka zaidi kwani msimu wa masika unakaribia.
Kuhusu kasi ya usogezaji wa umeme katika vijiji ,vitongoji na maeneo ya visiwa alisema kuwa kasi inaendelea vizuri na kuwa hadi mwaka 2021 maeneo yote ya nchi umeme utakuwa umefika na hakutakuwa na kijiji wala kisiwa ambacho wananchi watakuwa hawana umeme .
Pamoja na umeme huo wa maji na gesi ambao unatumika kwa sasa bado alisema shirika limeendelea na uvumbuzi wa vyanzo vingine vya umeme kama umeme wa joto ardhi ambao tafiti zinaonyesha baadhi ya mikoa kama mkoa wa Mbeya kuwepo kwa umeme huo .
" Tunategemea miaka mitano mbele kuwa na umeme utakaozalishwa kupitia joto ardhi hivyo bado nchi itaendelea kuwa na uhakika wa umeme baada ya kuwa na vyanvyo tofauti tofauti " alisema Dkt Kyaruzi
Alisema kuwa maeneo Ziwa ngozi mkoani Mbeya ni eneo la kwanza ambalo wamefanikiwa kufanya utafiti na kuonekana lina weza kuzalisha umeme wa joto ardhi na tayari wamempata mkandarasi wa kufanya zoezi la uchimbaji wa eneo hilo .
Dkt Kyaruzi alisema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli imekuwa na makusudi mema kwa watanzania na kuweka mkakati kabambe wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2021 kila mtanzania kuweza kupata umeme hivyo wao kama watekelezaji wa mpango huo watahakikisha wanatekeleza kwa nguvu zote .
Awali akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndolezi wakati wa hafla ya uwashaji umeme kijijini hapo mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi alisema hatakubali kuona ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi ya umeme katika mkoa huo .
Mkuu huyo wa mkoa alimtaka mkandarasi wa wakala wa Nishati Vijijini (REA) anayetekeleza mradi wa umeme katika kijiji cha Ndolezi kuhakikisha anakamilisha zoezi la usambazaji wa umeme katika kijiji hicho ndani ya siku 21 .
Pia mkuu huyo wa mkoa alisema mkandarasi lazima kuhakikisha anapeleka umeme katika maeneo yote ya umma kama zahanati ,shule na mengine kama alivyoelekezwa na kuacha kupeleka umeme kipendeleo kwa baadhi ya watu .
Wakati huo huo mkuu wa mkoa wa Iringa amepiga marufuku halmashauru zote za Mkoa huo kuruhusu usafirishaji wa nguzo za umeme pasipo kulipia ushuru wa nguzo wa asilimia tano kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa na bunge.
Asema wilaya ya Kilolo pekee kupitia kampuni ya New Foret amebaini ukwepati wa kodi wa shilingi bilioni 2.7 pesa ambazo walipaswa kulipa ushuru wa asilimia 5 kwa kila nguzo na wao wakawa wanalipa shilingi 5000 kinyume na sheria zilizotungwa na bunge.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo kabla ya kwenda kuwasha umeme wakati akizungumza na wadau wa mazao ya Misitu pamoja na viongozi wa halmashauri za wilaya ya Mufindi katika ukumbi wa mikutano kabla ya kuanza ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Alisema kuwa kitendawili cha umasikini wetu mkoa wa Iringa kimeanza kuteguliwa baada ya kubaini mabilioni ya fedha yanayopotea katika kipengere kimoja pekee cha nguzo za umeme kutokana na halmashauri kufanya mazungumzo yasiyo rasmi ya kuchukua ushuru wa shilingi 5000 kwa kila nguzo badala ya kukusanya ushuru wa asilimia 5 kwa kila nguzo.
Hapi alisema kuwa katika kuona mkoa wa Iringa kwa mwaka ujao unaongoza kitaifa katika ukusanyaji wa mapato ni lazima kwa wakurugenzi wote kusimamia ukusanyaji wa mapato yatokanayo na mazao ya Misitu kwa kufuata sheria na sio makubaliano yaliyo nje ya sheria zilizopitishwa na bunge toka mwaka 2013 pamoja na kufanyiwa marekebisho mbali mbali.
"Sheria hii ipo wazi na hakuna namna zaidi ya kutekeleza kwa maslahi ya nchi na mkurugenzi atakayeshindwa kusimamia basi atakuwa ameamua kutofuata sheria na litakalo mkuta yeye kama mkuu wa mkoa atakuwa amenawa mikono" alisema Hapi
Kuwa lazima mapato ya serikali kuweza kukusanywa kwa ufanisi na wakurugenzi na wakuu wa wilaya ni lazima kusimamia zoezi hilo kwa ufanisi .
Akitolea mfano alisema kwa wilaya ya Kilolo pekee kupitia kampuni moja ya New Foret company amebaini ukwepaji wa kodi wa shilingi zaidi ya bilioni 2 ambazo kampuni hiyo imeshindwa kulipa asilimia 5 za nguzo kwa muda wote na badala yake kampuni hiyo imekuwa ikilipa shilingi 5000 kwa kila nguzo kinyume na sheria zilizotungwa na bunge .
"Kwa pesa hizi pekee ambazo kampuni imeshindwa kulipa iwapo wilaya ya Kilolo ingeweza kukusanya ingeweza kujenga hospitali ya wilaya kwa pesa hizo ama kujenga shule zaidi ya tano au kupeleka maji kwa wananchi" alisema mkuu wa mkoa
Kuwa kwa upande wake yupo kwa ajili ya kusimamia sheria hivyo atahakikisha kodi iliyokwepwa kwa muda wote toka sheria ilipopitishwa inalipwa na namna ya kulipa watakubaliana na halmashauri jinsi pesa hizo zitakavyotolewa ila kuanzia sasa ni marufuku nguvu kusafirishwa bila kulipia asilimia 5 iliyopitishwa kisheria na bunge .
Alisema kuwa anatambua zipo nguzo za saizi mbali mbali kama saizi tatu tofauti na zipo zinazouzwa hadi milioni moja sasa kuchukua ushuru wa shilingi 5000 kwa nguzo ya milioni 1 ama nguzo ya shilingi 500,000 utaona ni kwa kiasi gani halmashauri zinavyopoteza mapato yake .
Mkuu huyo wa mkoa alisema kupitia eneo hilo pekee utaona ni kwa kiasi gani ukwepaji kodi huo ulivyokuwa na mnyororo mrefu kwani iwapo wataamua kufuatilia jambo hilo kwa kina wengi watakamatwa kwa kesi ya uhujumu uchumi .
"Ila tumesema kwa kuanzia sasa sheria isimamiwe kwa nguzo zote zinazotoka kulipia ushuru kwa asilimia 5 pili kuanzia makubaliano ya namna gani watalipa pesa wanazodaiwa na kama itashindikana basi watendaji wa umma watasema wanakusanya mapato kwa sheria gani Kilolo wao wamekwisha fanya wamebaini wanadai shilingi bilioni 2.7 hivyo halmashauri nyingine fanyeni hivyo "
Hata hivyo alisema hatakubali kuona mapato ya serikali yanapotea na kama kampuni za nguzo zitashindwa kulipa watatumia taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na vyombo vingine kuona wahusika wote wahujumu uchumi kukamatwa.
Hivyo alitaka ndani ya wiki tatu apewe taarifa ya namna kamati zitakazoundwa na wakuu wa wilaya kukaa na kukubaliana namna ya pesa hizo zitakavyo lipwa ikishindikana ataleta vyombo vyake kuona wote waliohusika kuhujumu uchumi wanafikishwa mahakamani .
"Kuwa hakuna atakayekusaidia kukwepa mapato hata upige simu kwa waziri gani kwani haya ni maagizo ya mheshimiwa Rais hivyo jambo la muhimu ni kukubali kulipa kwa utaratibu uliopo na wale watakaokubali wataweka utaratibu ila watakao kataa na kutaka kwenda mahakamani tutawabana wao kabla.
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ali Hapi mwenye suti nyeusi na mkurugenzi wa bodi ya Tanesco Dkt Alexander Kyarusi kulia wakiwasha umeme kijiji cha Ndolezi Mafinga mkoani Iringa
Mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi akisikiliza kero za wananchi juu ya umeme wilayani Mufindi jana
Mwenyekiti wa bodi ya Tanesco Dkt Alexander Kyaruzi (kushoto) akifuatilia taarifa ya meneja wa Tanesco Mafinga wakati wa uwashaji umeme kijiji cha Ndolezi
Wananchi Mufindi wakitoa kero zao kwa mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi wakati wa kuwasha umeme kijiji cha Ndolezi Mafinga
No comments:
Post a Comment