Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama eneo lililoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme katika Maporomoko ya Mto Rufiji- Stieglers Gorge wakati alipotembelea eneo hilo Oktoba 4, 2018. Kushoto kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Eneo litakapojengwa tuta la kukinga maji katika Mradi wa Kuzalisha Umeme kwenye Maporomoko ya Mto Rufiji- Stieglers Gorge ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilitembelea, Oktoba 4, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa tawi la reli litakalounganisha Stesheni ya Fuga katika reli ya TAZARA na eneo utakapojengwa Mradi wa Umeme wa Moporomoko ya Mto Rufiji – Stieglers Gorge wakati alipotembelea Stesheni hiyo, Oktoba 4, 2018. Kushoto ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na kushoto kwa Waziri Mkuu ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Tanzania wa TAZARA, Fuad Abdallah.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka wa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) kuhusu ujenzi wa tawi la reli litakalounganisha Stesheni ya Fuga katika reli ya TAZARA na eneo utakapojengwa Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Mto Rufiji – Stieglers Gorge wakati alipotembelea eno hilo Oktoba 4, 2018. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Tanzania wa TAZARA, Fuad Abdallah. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiksalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo wakati alipowasili kwenye eneo utakapojengwa Mradi wa Umeme katika Maporomoko ya Mto Rufiji – Stieglers Gorge, Oktoba 4, 2018. Kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephen Kebwe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Moporomoko ya Mto Rufiji – Stieglers Gorge, Oktoba 4, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Tanzania wa TAZARA, Fuad Abdallah wakati alipotembelea Stesheni ya TAZARA ya Fuga kukagua ujenzi wa tawi la reli hiyo litalounganisha steheni hiyo na eneo utakapojengwa Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya mto Rufiji – Stieglers Gorge, Oktoba 4, 2018.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kujenga mradi wa kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya mto Rufiji, Stiegler’s Gorge utasaidia sana kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo utakapojengwa mradi huo, leo (Alhamisi, Oktoba 4, 2018), Waziri Mkuu amesema umeme utakaotokana na maji, utazalishwa kwa gharama nafuu na utakuwa wa uhakika zaidi.
Amesema kwa vile umeme utakaozalishwa katika mradi wa Stiegler’s Gorge utakuwa wa bei nafuu na hivyo kuwa rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini, utatumika kama nishati mbadala kwa kuni na mkaa ambao umechangia sana kwenye uharibifu wa mazingira hasa ukataji miti.
Waziri Mkuu Majaliwa amewaomba viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wawaelimishe Watanzania kuwa mradi wa Stiegler’s Gorge una faida kubwa kwa Taifa kiuchumi na hauna athari za mazingira na badala yake utayaboresha.
Amewahakikishia Watanzania kuwa mradi huo utajengwa na utakamilika katika muda uliokusudiwa ambao ni miezi 36 kuanzia siku mkandarasi atakapokabidhiwa kazi hiyo.
Akizungumzia usalama katika eneo la mradi, Waziri Mkuu amesema viongozi wa mikoa ya Morogoro na Pwani wahakikishe kwamba wanaweka ulinzi wa kutosha kuanzia sasa na wakati ujenzi utakapoanza ili kuzuia hujuma na vitendo vya wizi na udokozi vinavyoweza kuvuruga kasi ya ujenzi wa mradi.
Amesema vifaa vitakavyoletwa na mkadarasi lazima vilindwe na wajenzi watakaoshiriki katika ujenzi wa mradi wahakikishiwe usalama wao na mali zao.
Amewataka wananchi pia washiriki katika ulinzi kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kuhusu watu wenye mienendo inayoweza kuzorotesha ujenzi wa mradi huo kwani jukumu la ulinzi si la polisi peke yao.
Kuhusu ajira kwa vijana wanaotoka katika maeneo yanayozunguka mradi, Waziri Mkuu amesema utaratibu utawekwa ili vijana wenye sifa wapewe nafasi ya kushiriki kwenye usaili na ikibidi watafanyiwa mchujo kwenye maeneo yatakayofikiwa na wengi.
Aliwaasa wote watakaobahatika kupata ajira ya kushiriki katika ujenzi wa mradi huo wawe waadilifu na wachapakazi ili kulinda heshima ya vijana wa Kitanzania na kuwashawishi wajenzi wa mradi kuajiri vijana wengine zaidi.
Kuhusu Wizara ambazo zinaguswa na maandalizi ya ujenzi wa miundombinu inayohitajika katika ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge, Waziri Mkuu ameagiza wizara hizo zishirikiane ili kuhakikisha kwamba kila Wizara inatimiza majukumu iliyopangiwa kwa wakati.
Wizara ambazo tayari zimeanza kuweka miundombinu wezeshi kwa mradi huo ni pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayosimamia ujenzi wa barabara na tawi la reli itakayounganisha eneo la mradi na stesheni ya Fuga katika reli ya TAZARA kazi ambayo imeanza na Waziri Mkuu wenyewe aliikagua.
Wizara ya maji nayo tayari imetimiza jukumu lake la kupeka maji katika eneo la mradi wakati wizara ya nishati imepeleka umeme. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Kilimo nazo zipo kwenye eneo la mradi kutimiza majukumu yote yanayozigusa.
Awali, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliishukuru Serikali kwa kukubali kutoa fedha ambazo zimesaidia sana katika ujenzi wa miundombinu ya maandalizi ya ujenzi wa mradi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 04, 2018.
No comments:
Post a Comment