Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi kubomoa
uzio wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya
kuchezea watoto na kusitisha mara moja shughuli za ujenzi kwenye eneo
hilo. Pichani, Waziri Mkuu akimwonyesha Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma,
Godwin Kunambi ( wapili kushoto) ramani ya jiji la Dodoma inayoonyesha
matumizi sahihi ya eneo hilo, Oktoba 21, 2018. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi kubomoa uzio
wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya
kuchezea watoto na kusitisha mara moja shughuli za ujenzi kwenye eneo
hilo. Pichani, mabati yakiwa yamezungushwa kwenye eneo hilo wakati
Waziri Mkuu alipolitembelea, Oktoba 21, 2018.(Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
………………………………………………………………………………
*Ni baada ya kujengwa kwenye eneo la wazi na kuziba barabara
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi kubomoa uzio
wa mabati uliojengwa kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya
kuchezea watoto na kusitisha mara moja shughuli za ujenzi kwenye eneo
hilo.
Uzio huo ambao mbali na kujengwa
katika eneo la wazi lililotengwa kwa ajili ya kuchezea watoto kwenye
mtaa wa Mji Mpya kata ya Madukani pia umeziba barabara ya tisa, hivyo
kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumapili, Oktoba 21, 2018) wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi
jijini Dodoma, ambapo alitembelea eneo hilo na kuagiza libomolewe na
lisalie kama inavyoonekana katika ramani na aliyeuziwa atafutiwe eneo
lingine.
“Huu mji umejengwa kwa ramani,
hamuwezi kubadili ramani kwa lengo la kumpa mtu eneo. Kwa nini mmeziba
barabara ya tisa na huu mji unatambulika kwa barabara, sasa bomoeni hapa
nataka barabara iendelee kutumika na eneo la kuchezea watoto libaki
wazi,”Waziri Mkuu amemuagiza mkurugenzi
wa jiji ahakikishe wanayatumia maeneo ya wazi kwa ajili ya kujenga
sehemu za mapumziko ili kuwawezesha wananchi kupata maeneo ya kupumzika
mara wanapomaliza kufanya shughuli zao za kikazi.
Amesema ni vema jiji likatenga
ardhi na kupima viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya
biashara, makazi, taasisi, huduma za jamii, viwanda pamoja na maeneo ya
wazi kwa ajili ya mapumziko. “Msifanye makosa kama yaliyofanyika Dar es
Salaam.”Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya
Ardhi na Mipangomiji wa jiji la Dodoma, Bw. Joseph Mafulu alimuonyesha
Waziri Mkuu ramani ambayo iliyotolewa na iliyokuwa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ambayo ilibadilisha matumizi ya
eneo hilo na kumpa muwekezaji.
Baada ya Bw. Mafulu kuonesha
ramani hiyo Waziri Mkuu alitoa ramani halisi ya jiji la Dodoma ambayo
inaonesha eneo hilo ni la wazi na ni mahususi kwa ajili ya michezo ya
watoto, hivyo alisisitiza kuwa litumike kama ilivyokusudiwa na si
vinginevyo.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu
aliwaonya watumishi wa halmashauri ya jiji la Dodoma kutorudia makosa
yaliyofanywa na CDA na kwamba jukumu lao ni kuhakikisha wanayasahihisha
makosa yaliyofanywa na mamlaka hiyo ili jiji liweze kupangika vizuri.Naye Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma, Bw. Kunambi aliahidi kuyafanyia kazi kikamilifu maelekezo yote
yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kesho (Jumatatu, Oktoba 22, 2018)
ataandika barua kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Mheshimiwa William Lukuvi kwa ajili ya kufuta hati ya eneo hilo na
muwekezaji watampa eneo lingine.
Awali,Waziri Mkuu alizungumza na
watumishi wa halmashauri ya jiji la Dodoma, ambapo aliwataka wabadilike
na wasimamie vizuri rasirimali za umma pamoja na kuwahamasisha na
kuwasisitiza wananchi wafanye kazi kwa bidii ili kufikia malengo
maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu alisema mtumishi
asiyeweza kufanya kazi kwa bidii anaweza kupata matatizo kwa sababu
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa Rais Dkt. John Magufuli
imedhamiria kuwahudumia wananchi ipasavyo. Kadhalika, Waziri Mkuu
aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini pamoja na mameneja
wasimamie vizuri utendaji kazi wa watumishi mbalimbali katika maeneo
yao. Alisisitiza kuwa lazima watumishi wafanye kazi na matokeo
yaonekane.
Pia Waziri Mkuu alifungua ofisi
kuu ya kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutupora na kisha
alitembelea kiwanda cha kusindika zabibu cha Alko Vintage na kukagua
uzalishaji wa mvinyo katika kiwanda hicho kilicho jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment