VIONGOZI wa ngazi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wamepongeza uongozi wa Kliniki ya Heameda iliyopo Bunju B ambayo imekuwa ikitoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wa wilaya hiyo na maeneo mengine huku ukiahidi kushughulikia kero ya ubovu barabara inayoelekea kwenye kliniki hiyo ambayo imetajwa kutoa mchango mkubwa kuokoa maisha ya Watanzania.
Hayo yamesemwa jana na ujumbe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kupitia Mkuu wake wa Wilaya Daniel Chongolo na Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo Dk.Christowell Mande wakati wa uzinduzi rasmi wa Kliniki ya Heameda ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP Reginald Mengi.
Akizungumzia Kliniki hiyo Chongolo amesema Serikali inathamini mchango wa kliniki hiyo kwa kutoa huduma kwa wananchi wa Kinondoni na hasa walioko maeneo hayo ambayo hayana vituo vingi vya afya.Pia amejibu kuhusu ombi kero ya barabara inayoingia kwenye kliniki hiyo kwa kuahidi kuishughulikia mara moja kwa kuitengeneza.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Dk.Mande amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika kutoa huduma za afya na iko tayari kufanya kazi na kliniki hiyo.
"Tunawakaribisha muda wowote kufanya kazi katika dhana ya PPP.Kikubwa ambacho tunaweza kueleza hapa ni kwamba tunathamini mchango wenu na tunaomba tuedelee kushirikiana katika kuwahudumia Watanzania,"amesema.
Wakati huo huo mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Kliniki ya Heameda Dk.Reginald Mengi amesema kijana wa Kitanzania Dk.Hery Mwandolela ambaye ndio mmikili wa Kliniki hiyo amefanya maajabu makubwa na anastahili kuwa mfano wa kuigwa.
"Nimefurahi kwani tulionana miaka 23 iliyopita ukiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha ukiwa huna kitu lakini leo umefanya jambo kubwa sana ndani ya nchi yetu.Nitoe mwito kwa vijana wengine kuiga mfano huu kwa kuthubutu.Ukisema neno na ukaliamini linatokea, na kila wakati ukiwa a kauli mbiu ya I can, I must ,I will ...kila kitu kinawezekana,' "amesema.
Pia ameguswa na ubovu wa barabara ya kuingia kwenye kliniki hiyo ambapo amesema atachangia ujenzi wa barabara hiyo baada ya Mkuu wa Wilaya kueleza kwamba ataishughulikia.
Awali Mkurugenzi wa Kliniki ya Heameda ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya moyo Dk.Hery Mwandolela amesema Kliniki yao ilianza mwaka 2010 ikiwa na wafanyakazi wawili na walikuwa kwenye vyumba viwili vya kupangisha lakini sasa kuna wafanyakazi 30 ina miliki jengo kubwa na vifaa vya kisasa.
"Heameda Kliniki imefanikiwa kufikia malengo iliyojiwekea ikiwemo kutoa huduma bora za kisasa kwa asilimia 95 na tumetoa huduma za matibabu kwa wagonjwa 13000 tangu tulipoanza tena kwa ufanisi mkubwa.Pia watalaamu wao wametoa elimu ya afya na upimaji kwa wafanyakazi wa taasisi binafsi na za Serikali.Baadhi ya taasisi hizo ni BoT,Tanesco,CRDB, TTCL,Tantrade ,NBC,NMB, Cocacola, na Vodacom ambao wote waliendelea kupata huduma bora na bado ni wateja wetu,"amesema.
Dk.Mwandolela pia amesema wameweza kuendesha uchunguzi wa afya bure kwa wananchi katika Kliniki yao Julai mwaka huu kwa kuwahudumia wananchi wa Dar es salaam na sehemu nyingine.Huduma hiyo ilitolewa na madaktari bingwa kutoka India kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa hapa nchini ambapo jumla ya wanachi 521 walipata huduma.
Amefafanua kati ya hao 72 walikuwa na shinikizo la damu bila kujua , 16 walikuwa na kisukari,wanaume nane waligundulika na satarani ya tezi dume na wananchi 89 walikuwa na matatizo ya macho.
Dk.Mwandolela amefafanua kwa kuzingatia ubora wa kimataifa Heameda Kliniki ina matarajio ya muda mfupi na ya muda mrefu ambapo amesema matarajio ya muda mfupi ambayo ni ndani ya mwaka mmoja ni kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa wa nje kwa kukamilisha vipimo vyote muhimu na kuboresha huduma za dharura.
Wakati matarajio ya muda wa kati ambayo ni ndani ya miaka miwili ni kuanzisha huduma za kulaza wagonjwa , upasuaji na kulaza wagonjwa mahututi (ICU), kuanzihsha kozi fupi kwa madaktari za kufundisha kwa vitendo jinsi ya kufanya na kutafsiri kwa usahihi vipimo muhimu vya moyo yaani Echo, ECG, ABPM,Holter na TMT kwani vipimo hivyo ni muhimu sana katika kuchunguza magonjwa ya moyo na kuokoa maisha ya mgonjwa.
"Madaktari wengi nchini hata walio katika daraja la ubingwa hawana ujuzi wa kufanya tafsiri sahihi ya vipimo hivyo.Pia kuweka mashine za CT Scan kwa ajili ya moyo na magonjwa mengine.
Wakati matarajio ya muda mrefu ni kumalizia ujenzi kwa sehemu iliyobakia , kufungua chuo cha mafunzo ya kada mbalimbali za afya kwa kiwango cha Stashahada(Diploma), na hapo baadae kuwa chuo kikuu cha afya.
Kuhusu lengo lao kuu amesema ni kuifanya kliniki hiyo kuwa hospitali bora ya kuokoa maisha Watanzania hasa wenye magonjwa ya moyo.Pia kutoa huduma nzuri za afya kwa wananchi.Kuhusu maono yao ni kuwa na hospitali kubwa yenye hadhi ya juu nchini Tanzania na kimataifa.
Amefafanua kuwa Kliniki ya Heameda ilianzishwa rasmi Oktoba 20 mwaka 2010 baada ya kusajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu chini ya wizara ya Afya.Kliniki hiyo ina watalaam waliobobebea katika fani ya magonjwa ya moyo na fani nyingine mbalimbali za afya kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.
Kuhusu changamoto Dk.Mwandolela amesema ubovu wa miundombinu hasa barabara inayoingia hospitalini hapo imekuwa kero kubwa kwa wagonjwa na wafanyakazi hasa katika msimu wa mvua na tayari taarifa hizo wameshazifikisha kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Changamoto nyingine ni ukubwa na ugumu wa gharama za uwekezaji hasa kwa kutuma mikopo inayotolewa na benki za biashara zinazotoza riba kubwa badala ya kutumia benki za uwekezaji zenye riba nafuu.
Ametumia nafasi hiyo kuwaomba vijana wa kitanzania kuiga mfano wake lakini pia kuamini kwenye falsafa iliyobebwa na kauli mbiu iliyojikita kwenye kuamini katika kuweza huku akitoa ombi kwa Dk.Mengi awe mlezi wao ili waweze kutumia kipawa na ujuzi alionao kufanikisha ndoto na malengo ya kliniki yao.
Mgeni
rasmi kwenye uzinduzi wa Kiliniki ya Heameda Dk.Reginald Mengi akikata
utepe kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa Kliniki hiyo leo jijini Dar es
Saalam.Anayeshangilia mmiliki wa kliniki hiyo ambaye pia ni Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Dk.Hery Mwandolela
Mwenyekiti
wa Kampuni za IPP Media Dk.Reginald Mengi (katikati) akiwa pamoja na
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Dk.Hery Mwandolela(kulia) na kushoto
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo wakiangalia ujumbe uliopo
kwenye jiwe la msingi ikiwa ni ishara ya kuzinduliwa rasmi kwa Kliniki
ya Heameda ambayo ni maalum kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu ya
magonjwa ya moyo.
Mkuu wa Wilaya Kinondoni jijini Dar es Salaam Daniel Chongolo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Heameda iliyopo Bunju B jijini Dar es Salaam ambapo ameahidi kutatua kero ya barabara inayoelekea kwenye kliniki hiyo
Mmiliki wa Kliniki ya Heameda ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo Dk.Hery Mwandolela akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo leo jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kampuni za IPP Dk.Regenald ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Kliniki ya Heameda akiwa kwenye picha ya pamoja
Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Kliniki ya Heameda iliyopo Bunju B jijini Dar es Salaam Dk.Reginald Mengi akikabidhi cheti maalum kwa Dk.Isaac Maro kwa kutambua mchango wake katika kliniki hiyo.
Mwenyekiti
wa Kampuni za IPP Dk.Reginald Mengi(kushoto) aliyekuwa mgeni rasmi
kwenye ufunguzi wa Kliniki ya Heameda iliyopp Bunju B jijini Dar es
Salaam akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel
Chongolo(kulia) leo.Katikati ni Mmiliki wa kliniki hiyo Dk.Hery
Mwandolela
No comments:
Post a Comment