Sunday, October 28, 2018

WAZIRI LUKUVI ALITAKA SHIRIKA LA NYUMBA NHC KUWA MFANO KATIKA KUSIMAMIA NA KUTUNZA NYUMBA ZAKE

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuwa mfano katika, kuhifadhi, kutunza na kujenga nyumba bora za gharama nafuu kwa ajili ya kuziuza au kuzipangisha kwa wananchi wakiwemo watumishi wa umma.

Aidha, amelitaka shirika la NHC kuwa mfano kwa taasisi nyingine zinazojishughulisha na ujenzi kwa kujenga nyumba bora na wakati huo kuwapangisha wananchi kwa malipo ya kodi ya mwezi mmoja mmoja badala ya utaratibu uliozoeleka wa kupangisha kwa malipo ya kipindi cha miezi sita au mwaka mzima na kuepuka kutumia ‘vishoka’ wakati wa kupangisha nyumba zake.

Lukuvi aliyasema hayo jana alipolitembelea Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkoa wa Kilimanjaro wakati wa mwisho wa ziara yake ya kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya za Hai, Moshi na Same mkoani Kilimanjaro.

Alisema, Shirika la Nyumba la nyumba NHC lazima liwe na mkakati mzuri wa ukarabati nyumba zake na kubainisha kuwa haiwezekani Shirika kubwa kama hilo kuwa na nyumba nyingi katika maeneo ya vitovu vya miji huku nyingi ya nyumba hizo zikiwa zimechoka na kusisitiza kuwa hataki kusikia NHC inakuwa na nyumba za aina hiyo.

Amelitaka Shirika kujipanga vizuri na kuhakikisha linashirikiana vizuri na ofisi za Mikoa na Halmashauri kwa lengo la kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi na wakati huo kutangaza shughuli zake kwa kuwa NHC ina Kampuni yake ya ujenzi iliyosheheni wataalamu wa fani mbalimbali sambamba na kuwa na uwezo wa kujenga majengo mbalimbali kama vile Shule, Hospitali, Vituo vya Afya na Vyuo.

Aidha, Lukuvi amelitaka Shirika la NHC kuimarisha kitengo chake cha huduma kwa wateja na kujiwekea utaratibu wa kuwatembelea wapangaji wake kwa lengo la kufahamu changamoto zinazowakabili katika nyumba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kilimanjaro Juma Kiaramba alimueleza Lukuvi kuwa Shirika la NHC katika mkoa huo liko kwenye mazungumzo na halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 25 za gharama nafuu na mradi huo utagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.4 na utachukua miezi kumi na nane mpaka kukamilika.

Kwa mujibu wa Kiaramba, NHC mkoa wa Kilimanjaro pamoja na kufanya ukarabati wa majengo yake katika mkoa huo, kwa sasa Shirika iko kwenye mazungumzo na taasisi mbalimbali mkoani humo ikiwemo halmashauri ya Same kwa ajili ya kujenga nyumba za gharama nafuu ingawa kumekuwa na chanagamoto kubwa ya uhaba wa ardhi katika maeneo kadhaa ya mkoa huo.

No comments: