Monday, October 22, 2018

Wafanyakazi wa Vodacom watoa msaada wa vifaa vya kusomea kwa wanafunzi wasioona Jijini Dar es Salaam.

Wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania PLC, kupitia mpango wake wa Pamoja na Vodacom leo wametoa msaada wa vifaa vya kusomea kwa Wanafunzi zaidi ya 150 wenye ulemavu katika shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya shule hiyo iliyoko Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Elimu bora kwa wote ni moja kati ya nguzo kuu za asasi ya Vodacom Tanzania Foundation hivyo msaada huu wa nyenzo za kujifunzia pamoja na vifaa mbalimbali vya elimu kwa ajili ya wasioona pamoja na wale wenye uoni hafifu utaisaidia shule kukabiliana na matakwa mbalimbali ya kuhudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Upatikanaji wa vitabu vya nukta nundu (vitabu maalum kwa Wasioona) pamoja na maandiko mengine, ni hafifu na msaada huu utasaidia katika kupunguza ukubwa wa tatizo hili. Msaada huu kutoka kwa Wafanyakazi wa Vodacom unahusisha mashine kumi na karatasi maalum za kuchapia maandishi ya nukta nundu (Maandishi maalum kwa Wasioona), viti, faili za plastiki (maalum kwa ajili wasioona), vifaa hivi vitasaidia zaidi ya wanafunzi 67 wenye shida ya macho katika shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko. Kwa sasa Walimu wataweza kuandaa lesoni na vifaa maalum vya kufundishia kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu. Zaidi ya hayo, Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania PLC wamejitolea nguo, sabuni na vyakula mbalimbali ili kuwasaidia wanafunzi hao.

Akizungumza kwa niaba ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Vodacom, Mkurugenzi wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani George Lugata alisema, “elimu ni haki ya msingi na kipengele muhimu cha malengo endelevu ya milenia, tunatambua mchango muhimu wa shule ya msingi Uhuru Mchanganyiko katika kuwalea Watoto walio pembezoni wenye ulemavu kwa kuwapa elimu bora inayoendana na mahitaji ya wanafunzi.” 

Asasi ya Vodacom Tanzania Foundation imekuwa ikitumiwa na wafanyakazi wa Vodacom kurejesha fadhila kwa jamii na kuwainua walio pembezoni wa jamii. Pamoja na Vodacom ni mojawapo kati ya mpango unaotumika, na kupitia mpango huu wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom wameweza kuwa mawakala wa mabadiliko kwa kuwasilisha changamoto zilizoko katika jamii yao. 

“Tuna shauku ya kuisaidia jamii yetu, na huu umekuwa ni utaratibu wetu kwa miaka zaidi ya 12 kupitia Vodacom Tanzania Foundation,” alisema Lugata huku akiongeza kwamba hii ni mara ya pili kwa Vodacom kutoa msaada kwa shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ambapo mwaka 2011 walitoa msaada wa Shilingi 12 milioni ili kujenga mabweni na vyoo kwa ajili ya wanafunzi hao. 

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa nchi, ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu (anayeshughulikia Walemavu) Stella Ikupa Alex aliishukuru kampuni ya Vodacom kwa msaada huo na kufafanua namna ambavyo msaada huo utasaidia kupunguza mzigo ambao serikali imekuwa ikiubeba kuihudumia shule hiyo huku akiomba taasisi zingine kufuata nyayo za Vodacom. 

“Zaidi ya nusu ya watoto wenye ulemavu nchini hawaendi shule hii ikisababishwa na hali zao, kwa sasa Tanzania kuna Watoto 4.2 milioni wenye ulemavu,” alisema Naibu Waziri Stella Ikupa, “pamoja na maendeleo mazuri yaliyofanyika kutokana na juhudi mbalimbali lakini bado kuna watoto wenye ulemavu hawapelekwi shule, ila kwa msaada wa taasisi kama Vodacom Foundation tumeweza kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya watoto wenye ulemavu hawaachwi pembezoni katika ulimwengu wa elimu,” aliongeza. 

Mkuu wa shule hiyo, Anna Mshana alielezea furaha yake kwa niaba ya wanafunzi, “tumefurahishwa sana na ukarimu wa Wafanyakazi wa Vodacom, Zawadi zao zitatusaidia sana katika kufundisha na pia kuwawezesha wanafunzi wetu kuelewa kwa haraka yale wanayofundishwa maana wengi wa wanafunzi hawa wanatoka katika familia zenye kipato cha chini, alisema.


Kamishna msaidizi watu wenye ulemavu, ofisi ya waziri mkuu, sera, bunge, ajira na watu wenye ulemavu, Beatrice Fungamo (Kushoto) akipokea moja ya mashine maalum za kuandikia maandishi ya nukta nundu (Braille) zilizotolewa jana na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation na wafanyakazi wa Vodacom Tanzania PLC wakiongozwa na mkurugenzi wa kanda ya Pwani George Lugata, vifaa hivyo vitaleta ufanisi katika kutoa elimu bora kwa wasioona na wale wenye uoni hafifu. 

No comments: