Monday, October 22, 2018

TAASISI ZA FEDHA ZATAKIWA KUTOA ELIMU YA NIDHAMU YA FEDHA KWA WAJASIRIAMALI

NA MWAMVUA MWINYI,KIBAMBA.
 
TAASISI mbalimbali za kifedha zimeaswa kutoa elimu kwa wajasiriamali kuhusiana na nidhamu ya matumizi ya fedha katika biashara zao ,kabla ya kuwakopesha ili waweze kunufaika na mikopo wanayowapatia.
 
Pamoja na hayo, wajasiriamali hao wametakiwa kuwa wabunifu kwa kuzalisha bidhaa zilizo bora na kuhifadhiwa vizuri ili kuendana na soko la ushindani wa kibiashara.

Hayo yalisemwa na Beatrice Mbawala ambae alimwakilisha mkuu wa wilaya ya Ubungo jijini Dar es salaam, wakati wa uzinduzi wa kikundi cha Gogoni Vicoba Investor, kilichopo kata ya Kibamba .Alieleza, elimu juu ya fedha wanazokopa wajasiriamali ni muhimu kwani baadhi yao wamekuwa wakifilisika kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya fedha .
 
Beatrice alisema kuwa ,baadhi ya wajasiriamali wameshindwa kufikia mafanikio  na kuwa wajasiriamali wakubwa kutokana na kushindwa kuwa na nidhamu ya fedha wanazokopa .“Akinamama ,wajasiriamali mliopo hapa mhakikishe mnakuwa waaminifu na kuwajali wateja wenu,kuzalisha bidhaa bora na kuacha kutumia mikopo mnayochukua kutafuta kiki mitaani,kwa kufanya ufahari”alieleza Beatrice.
 
Nae mkufunzi wa vicoba kutoka taasisi ya Pamoja Entrepreneurship Support for Community  Development (Pescode) Enethlena Wadelanga alisema ,wanawapa mafunzo ya ujasiriamali kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kifikra na kujitetea kwa kuunganisha nguvu ujuzi na uzoefu.Alifafanua ,jamii  inapaswa kuamka ili kuleta maendeleo kwa kuungana kwani vita ya kiuchumi ni ya pamoja kwa ajili ya kuboresha maisha kupitia shughuli zao za kila siku za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za kila mwanachama.  
 
Enethlena alifafanua, wanatarajia kujenga ofisi kwa ajili ya kufanyia shughuli zao na kuanzisha ufugaji wa kuku na kuwaomba wadau kuwaunga mkono hasa taasisi za kifedha ili waweze kujiinua kiuchumi.Mwanachama Mariam Kawawa alisema kuwa wangehitaji kutengewa eneo kwa ajili ya wajasiriamali kufanyia kazi kuliko kila mtu kufanyia sehemu yake ambapo baadhi ya bidhaa huzalisha uchafua na kutupwa holela.
 
Mariam alibainisha, kutokana na kujiunga kwenye vicoba hiyo ameweza kunufaika na mafunzo mbalimbali ambapo kwa sasa anazalisha bidhaa mbalimbali na kuweza kujikwamua kiuchumi huku akiwa ametoa ajira kwa watu wengine ambao anashirikiana nao.Gogoni Investor ilianzishwa mwaka mmoja uliopita na ina wanachama 50 ambao kuna makundi mawili A na B ikiwa na malengo ya kujikwamua kiuchumi .
 Beatrice Mbawala (wa pili kushoto) akiangalia bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali kutoka kikundi cha Gogoni Vicoba Investor, wakati alipomwakilisha mkuu wa wilaya ya Ubungo jijini Dar es salaam, katika uzinduzi wa kikundi hicho, kilichopo kata ya Kibamba ,(wa kulia) ni mkufunzi wa vicoba kutoka taasisi ya Pamoja Entrepreneurship Support for Community  Development (Pescode) Enethlena Wadelanga
IMG-20181021-WA0023
Beatrice Mbawala akizungumza wakati alipomwakilisha mkuu wa wilaya ya Ubungo jijini Dar es salaam, katika uzinduzi wa kikundi cha Gogoni Vicoba Investor, kilichopo kata ya Kibamba.Picha na Mwamvua Mwinyi
……………………….

No comments: