Thursday, October 4, 2018

WAANDISHI WASHINDA TUZO ZA HABARI ZA MAJI...MWAKYEMBE ATOA NENO


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAZIRI wa Habari,Sanaa ,Utamaduni na Michezo Dk.Harson Mwakyembe amekabidhi tuzo za Habari za Maji kwa waandishi mahiri wa masuala ya uwajibikaji kuhusu usimamizi wa rasilimali za maji.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika la Shahidi wa Maji kupitia Programu ya Uhakika wa Maji kwa kushirikiana na Shirika la Water Witness International,WaterAid pamoja na Journalist Enviromental Association of Tanzania(JET).

Tuzo hizo ambazo zimekabidhiwa kwa waandishi hao zinajulikana kama Tuzo za Habari za Maji kwa waandishi hao mahiri wa masuala ya uwajibikaji kuhusu usimamizi wa rasilimali za maji.Waliokabidhiwa tuzo hizo ni Mwandishi Nuzulack Dausen (Kundi B) ambalo lilihusu Uandishi mahiri wa habari za maji kwa uhakika wa maji.

Mwandishi mwingine aliyepatq tuzo ni Sylvester Domasa(Kundi B) ambalo lilihusu Mwandishi mahiri wa habari aliyetumia taarifa za mradi wa uhakika wa maji kuleta mabadiliko.Pia Mwandishi Amina Semagongwa (Kundi C) ambalo lilihusu Mwandishi mwenye umri mdogo

Akizungumza Waziri Mwakyembe amesema tuzo hizo zitaleta chachu kwa waandishi kuandika habari za maji.Kuhusu mjadala ambao ulizungumzia waandishi kutoandika habari za maji,amesema changamoto kubwa ni waandishi kutokuwa na ari ya kufanya tafiti na hiyo inatokana mazingira duni ya kufanya kazi waandishi na hivyo mkakati wa Wizara yake ni kuinua taaluma ya habari ikiwa pamoja na kuboresha maslahi ya waandishi.

"Ukame wa habari za maji katika vyombo vya habari kuna sababu nyingi ambazo zinachangia na kubwa ni ari ya kufanya kazi za tafiti kwenye vyombo vya habari." Hakuna ari ya kufanya tafiti kutokana na mazingira yaliyopo katika tasnia ya habari na ndio maana tumeandaa sheria ya huduma ya kupata habari ambayo itasaidia kuondoa changamoto,"amesema Dk.Mwakyembe.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Juma Uweso amesema tuzo hizo ni chachu kwa waandishi kujikita katika kuandika habari zinazohusu rasilimali ya maji.Pia amesema maji ni muhimu katika kufikia dira maendeleo ya Taifa na kwamba moja ya jukumu ni kulinda vyanzo vya maji.Ameongeza rasilimali za maji zimeendeleea kupungua mwaka hadi mwaka na hiyo inatokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, mabadiliko ya tabianchi na uwepo wa shughuli za kibinadamu.

"Sote tunafahamu kuwa sekta ya maji inapaswa kupewa kipaumbele na kila mmoja wetu na Serikali itaendelea kupambana na changamoto zilizopo.Pia amesema kuna changamoto ya uelewa kuhusu maji na hivyo mkakati wa Wizara ni kutumia vyombo vya habari kuelemisha umma.Hivyo amesema tuzo za maji zitatoa nafasi ya kuongeza uelewa wa Watanzania kuhusu sekta ya maji na kuomba waandishi wa habari kuendelea kushiriki kwenye tuzo hizo.

Amewapongeza Mashahidi wa Maji kwa kuandaa tuzo ambazo zimekuja wakati muafaka.Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo amesema changamoto kubwa iiyopo ni kwamba maji bado ni shughuli za Serikali.Amesema hivyo Serikali imekuwa ikihamasisha sekta binafsi kushiriki katika shughuli za maji na kwa sasa kuna mpango mkakati unaandaliwa kwa ajili ya kuhakikisha sekta binafsi zinashiriki katika shughuli za maji.

Pia amesema habari za maji zinaandikwa sana na anakumbuka hivi karibuni aliulizwa maswali 500 ndani ya saa moja kuhusu maji wakati anazungumza kwenye moja ya luninga nchini.Amesema waandishi wanaandika sana habari za maji na hasa zinazohusu usambazaji lakini zile za kulinda rasilimali maji ndio hazijapewa kiuambele.“Ili habari iandikwe kuna namna yake.Habari za maji zinaandikwa kila siku.Mfano Profesa Kitila Mkumbo akinywa maji si habari ila nikinywa maji yaliyochanganyika na kinyesi hiyo itakuwa habari,"amesema.

Ameongeza kuwa “Pia ili iwe habari lazima kuwe na mgogoro kidogo na kwa hapa nchini bado hatuna migogoro inayoibuliwa katika eneo la maji,”amesema.Naye Mratibu wa Shirika la Shahidi wa Maji matarajio ya shirika hilo ni kuona idadi kubwa ya waandishi wa habari wanashiriki na kushinda tuzo hizo.
 Waziri  wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dk.Harson Mwakyembe akizungumza na wadau mbalimbali wa maji katika hafla ya tuzo  za habari za maji zilizotolewa jana jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dk.Harson Mwakyembe (kushoto) akimkabidhi zawadi mshindi wa habari za maji,Nuzulack Dausen katika hafla iliyofanyika jana  jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii)
 Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza katika hafla ya tuzo za maji jana jijini Dar es Salaam.
 Sehemu ya wadau mbalimbali wa maji wakiwa katika hafla ya tuzo za waandishi wa habari za maji jana  jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dk.Harson Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na wageni waalikwa na washindi wa tuzo hizo.

No comments: