SHULE ya Msingi Tusiime imeendelea kufanya vizuri kitaaluma baada ya kufanikiwa kuwa ya 13 kitaifa kati ya shule 10,090 na kuwa ya pili kwa Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa na wanafunzi wengi kuliko shule zote.
Shule hiyo pia imefanikiwa kuwa ya kwanza kwa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kati ya shule 90 na kutoa wanafunzi bora wawili kati ya wasichana 10 bora kitaifa na mvulana mmoja kwenye 10 bora kitaifa wavulana.
Wasichana wawili wa shule hiyo waliongia 10 bora ni Hamisa Kasele aliyeshika nafasi ya nne na Kareen Gabriel aliyeshika nafasi ya tano kitaifa.
Shule hiyo imekuwa ya 13 kitaifa ikiwa na jumla ya wanafunzi 243 ambapo 239 wamepata wastani wa alama A.Shule nyingi zilizoingia 10 bora zilikuwa na wastani wa wanafunzi 70,60, 65 kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani NECTA hivyo Tusiime kuwa shule yenye wanafunzi wengi zaidi.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na gazeti hili kuhusu matokeo hayo ya Tusiime walisema wamefurahishwa na matokeo ya shule hiyo ya darasa la saba mwaka huu hasa kwa wanafunzi wote 239 kupata wastani wa alama A.
Mmoja wa wazazi hao, Aisha Yusuf alisema wameyapokea matokeo hayo kwa furaha ya aina yake kwani si kazi rahisi wanafunzi wote 239 kufaulu kwa wastani wa alama A.
“Walimu wa Tusiime wanafundisha kwa kweli maana kuwa wa 13 kitaifa ukiwa na wanafunzi 243 si kitu rahisi na ukiangalia shule nyingi zilizoingia 10 bora kitaifa zina idadi ndogo sana ya wanafunzi, zingine zina 60,70, 65 na 80 na moja tu ndiyo ina wanafunzi 120 hivyo walimu Tusiime wamejitahidi kufundisha,” alisema
“Shule imekuwa ikifanya vizuri na kwa kweli wanaendelea kufanya vizuri nimeangalia matokeo si watoto wangu tu waliopata alama A kwenye masomo yao wanafunzi wote wamepata A masomo yote, mazingira ya shule ni mzuri nadhani nayo yamechangia sana kufanikisha haya,” alisema mzazi mwingine Amos Mpango.
Samson Zungu alisema matokeo yamewafurahisha sana na kwamba bila shaka ni matunda ya jitihada za walimu na uongozi wa shule hiyo ambao wamekuwa bega kwa bega na wazazi wa wanafunzi katika kufuatilia maendeleo ya taaluma ya wanafunzi hao.
Mkurugenzi wa shule za Tusiime Albert Katagira, aliipongeza bodi ya shule hiyo wazazi, walimu, wafanyakazi wote wa shule na wanafunzi kwani mafanikio hayo yametokana na mchango wao mkubwa.
“Tumejipanga 2019 tuwe wa kwanza kitaifa,” alisema
Aidha, aliishauri serikali kwamba upangaji wa matokeo ya shule 1O bora uzingatie idadi ya wanafunzi kwani kwa kufanya hivyo baadhi ya shule za serikali zitaingia 10 bora.
“Endapo watafanya ushindani wa shule zenye zaidi ya wanafunzi 200 shule nyingi za serikali zitaingia kwenye 10 bora,” alishauri Katagira
Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Msingi Tusiime, Maxon Binomtonzi akiwapa matokeo ya darasa la saba wanafunzi wa shule hiyo ambayo ilikuwa na watahiniwa 243 imefanikiwa kuwa ya 13 kitaifa kati ya shule 10,090 nchini na kuwa ya pili Mkoa wa Dar es Salaam na ya kwanza Wilaya ya Ilala.
No comments:
Post a Comment