Wednesday, October 24, 2018

TUME YAONYA WATAKAOHARIBU UCHAGUZI

Na Margareth Chambiri.


TUME ya Taifa ya Uchaguzi imewaonya Wasimamizi wa Uchaguzi ambao ama kwa kujua au kwa makusudi wataharibu au kukiuka taratibu za Uchaguzi kutokana na kutofuata sheria na taratibu za Uchaguzi.

Onyo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Mbarouk Salum Mbarouk wakati akifungua mafunzo kwa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi jijini Dodoma.

Mheshimiwa Mbarouk ambaye amewataka Wasimamizi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea amesema Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na ile ya Serikali za Mitaa zinaunda kosa la jinai na kutoa masharti ya adhabu kwa Afisa yeyote wa Uchaguzi ambaye atasababisha kuharibu uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi  amesema madhara ya kutozingatiwa kwa taratibu za Uchaguzi ni kusababisha kesi nyingi za Uchaguzi na kuitumbukiza Serikali katika gharama ambazo zingeweza kutumika katika shughuli nyingine za maendeleo.

Amewataka Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuyaelewa vyema maeneo wanayofanyia kazi na kujiamini ambapo pia amewakumbusha jukumu walilo nalo la kuimarisha imani ya wananchi na wadau wengine wa Uchaguzi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt Athumani Kihamia amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutoa ushirikiano kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mdogo ikiwa ni pamoja na kuvishirikisha katika kila hatua muhimu wakati wa mchakato wa Uchaguzi.

Dkt. Kihamia amesema Watendaji wote wa Tume wanapaswa kuwapo katika maeneo yao ya kazi wakati wote hususan kipindi cha Uteuzi, kufungua ofisi hadi muda wa kisheria na Vyama vyote ambavyo vimefuata taratibu vipewe fomu za Uteuzi na Wagombea wao wateuliwe kama wamekidhi vigezo.

Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi ameongeza kusema kuwa kutozingatiwa kwa mambo hayo husababisha kuharibu imani ya Wadau na kusababisha malalamiko ya kutoridhishwa na mchakato wa Uchaguzi na hatimaye mashauri ya Uchaguzi kufikishwa mahakamani.

Kadhalika Dkt Kihamia amewataka Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi hao wa Uchaguzi kutojihusisha na migogoro ya ndani ya Vyama na iwapo Vyama vitakuwa na malalamiko vielekezwe kuwasilisha malalamiko yao kwenye Kamati za Maadili na si mahali pengine popote.

Kwa mujibu wa Dkt. Kihamia chaguzi zote duniani ni kielelezo cha demokrasia na kwamba Uchaguzi huru na wa haki hutokana na Wasimamizi wa Uchaguzi wanaozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Uchaguzi husika.

Jumla ya Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi 210 kutoka katika Majimbo manne ya Serengeti, Simanjiro, Ukerewe na Babati Mjini pamoja na Kata 47 zinazotarajiwa kufanya Uchaguzi Mdogo Desemba 3, mwaka huu wanashiriki katika mafunzo hayo yatakayodumu kwa siku tatu jijini Dodoma. 
Mkuu wa Idara ya Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Irene Kadushi, akifafanua jambo wakati wa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi. 
Mkuu wa Idara ya Huduma za Sheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Emmanuel Kawishe akifafanua hoja katika mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Afisa Uchaguzi Meshack Mgovano, akieleza jambo kwenye mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Picha zote na NEC.

No comments: