Tuesday, October 16, 2018

TCCIA, KAIMU BALOZI WA LIBYA NCHINI WAJADILI FURSA ZA KIBIASHARA,UWEKEZAJI

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii 

CHAMA cha Wafanyabishara wenye Viwanda na Kilimo nchini(TCCIA) kimefanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Libya nchini Tanzania Saleh Kusa Arze ambapo kwa sehemu kubwa mazungumzo yao yamejikita kuangalia fursa za kibishara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili. Katika mazungumzo hayo nchi ya Libya imeonesha nia ya kuwekeza hasa katika sekte ya nishati ya umeme na kilimo na kuna kampuni ya Libya inataka kuwekeza kwenye mradi wa umeme wa megawati 400. 

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mbele ya Balozi Arze , Kaimu wa Rais wa TCCIA Octavian Mshiu amesema ujio wa balozi huyo kwenye chemba yao umekuwa wa mafanikio makubwa kwani wamezungumza mambo mengi yanayoonesha nia njema katika eneo la biashara kati ya nchi hizo mbili. "Tunashukuru kwa ujio wa Kaimu Balozi wa Libya nchini kwetu.Kikubwa ambacho tumezungumza pamoja na mambo mengine kuna moja ya kampuni ya nchi hiyo inataka kuja nchini kuwekeza katika mradi wa umeme wa megawati 400.Tararibu bado zinaendelea na pale tutakapokuwa tayari tutatoa taarifa. 

Mshiu pia ametoa rai kwa wafanyabishara nchini kuitumia TCCIA hasa kwa kuzingatia uwepo wao unalenga kuangalia fursa ambazo wafanyabishara wanaweza kuzitumia vema katika kujenga uchumi wa nchi yetu kwa maslahi ya Watanzania wote. "Mwaka huu tunatarajia kusheherekea miaka 30 ya uwepo wa TCCIA. Tumetoa mchango mkubwa na dhamira yetu ni kuendelea kupanua wigo wa fursa za biashara na uwekezaji nchini.

 Tunataka kuthibitisha tupo kwaajili ya kuisaidia Serikali katika jitihada za kujenga uchumi,"amesema Mshiu Kwa upande wa Kaimu Balozi Arze amepongeza jitihada za TCCIA katika kuwanunganisha wafanyabiashara wa nchi yake na Tanzania na kuna maeneo ambayo wanatamani kuja kuwekeza na hivyo wameona ni vema kuanza mchakato wa mazungumzo kabla ya kukutana na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali. 

"Kuna maeneo ambayo wafanyabiashara wetu wa Libya wanatamani kuja kuwekeza, hivyo leo nimekuja TCCIA nikiamini kuwa watakuwa sehemu ya kuwaunganisha wafanyabishara wetu na chemba hii ya biashara.Tunataka pande zote mbili zinufaike na fursa za kibiashara zilizopo,"amesema Kaimu Balozi Arze . Wakati huo huo Mkurugenzi wa TCCIA Fatma Hamis amesema ombi kubwa la Kaimu Balozi wa Libya ni kuhakikisha sekta ya biashara inapewa kipaumbele kati ya Tanzania na Libya na kuwaunganisha wafanyabiashara wa pande zote mbili."Kuna wafanyabiashara wa nchi yao wanataka kuwekeza katika nyanja mbalimbali.

" Fatma Hamis amefafanua"Kaimu Balozi wa Libya nchini Tanzania ombi lake kubwa kwetu ni kutaka chemba yetu ya biashara kuwaunganisha na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali ili wafanyabiashara wao wapate fursa ya kuja kuwekeza nchini kwetu na wa kwetu wapate fursa ya kufanya biashara nchini kwao,"amesema.
Kaimu Rais wa Chama cha wenyeviwanda na Kilimo (TCCIA) Octavian Mshiu aliyekaa kushoto akisalimiana na Kaimu Balozi wa Libya nchini Tanzania Saleh Kusa Arze leo jijini Dar es Salaam baada ya kufika katika ofisi za TCCIA kwa lengo la kujadili masuala ya biashara na uwekezaji.
 Kaimu Balozi wa Libya nchini Tanzania Saleh Kusa Arze(kulia) akifafanua jambo kuhusu fursa za uwekezaji baada ya kukutana na Kaimu Rais wa TCCIA Octavian Mshiu leo jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Rais wa TCCIA Octavian Mshiu (wa kwanza kulia)akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Balozi wa Libya nchini Tanzania Saleh Kusa Arze(wa pili kulia). Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa TCCIA Fatma Hamis na wa kwanza kushoto ni Msaidizi wa Kaimu Balozi

No comments: