Thursday, October 25, 2018

Tanzania na Ubelgiji Kushirikiana Sekta ya Uwekezaji


Naibu Waziri , Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Injinia Stella Manyanya akiwahutubia washiriki wa kongamamano la uwekezaji na biashara (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo uliofanyika mapema leo Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa kongamano la uwekezaji baina ya Makampuni 41 kutoka Ubelgiji na Sekta binafsi 200 kutoka Tanzania wakifuatilia mazungumuzo ya kongamano hilo yaliyofanyika mapema leo Jijini Dar es Salaam



Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),John Mnali akiwasilisha maada kwa washiriki wa kongamano, kuhusu fursa zinazopatikana nchini pamoja na huduma zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa wawekezaji .



Washiriki kutoka Tanzania wakifuatilia mazungumuzo katika kongamano la uwekezaji na biashara yalifanyika mapema leo katika ukumbi wa Serena Hoteli Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),John Mnali akisisitiza jambo kwa washiriki wa kongamano ( hawapo pichani), kuhusu fursa zinazopatikana nchini pamoja na huduma zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania, katika kongamano linalofanyika Jijini Dar es Salaam. (Picha na Paschal Dotto-MAELEZO)

…………………………………………………………………………..

Na  Paschal Dotto-MAELEZO

Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imezitaka sekta binafsi na makampuni kuchangamkia fursa za uwekezaji na biashara ili kuweza kuimarisha mitaji yao pamoja na kupanua wigo wa masoko na kutangaza fursa za uwekezaji kwa kushirikiana na makampuni ya nchi za nje.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika kongamano la kibiashara linalohusisha makampuni zaidi ya 41 kutoka nchini Ubelgiji na sekta binafsi 200 kutoka Tanzania, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Injinia Stella Manyanya, amesema kuwa Tanzania na Ubelgiji zimekuwa na mashirikiano ya siku nyingi katika masuala ya kiuchumi.

“Nchi ya Ubelgiji tunashirikiana nayo kwenye masuala ya bandari za Dar es Salaam na Zanzibar, lakini pia natambua kuwa Ubelgiji wana mahusiano na nchi za Rwanda na Congo kwa hiyo ni rahisi kuunganisha ukanda huu kwa kutumia bandari zetu na kufungua biashara katika ukanda huo”, alisema Injinia Manyanya.

Aidha, Injinia Manyanya alibainisha kuwa kongamano hilo litafungua ukurasa mpya kwa jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwani amekuwa akisisitiza masuala ya uwekezaji ili kujenga Tanzania ya Viwanda ambapo ameweza kuzuia rushwa, urasimu na ufisadi kitu ambacho kimevuta wawekezaji wengi kuja kuwekeza hapa nchini.

Alieleza kuwa fursa za uwekezaji zimefunguliwa Tanzania na kuwasihi wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.

“Tanzania kuna fursa nyingi sana za uwekezaji ikiwemo fursa za kilimo, masuala ya umeme, madini, utalii pamoja na uvuvi, kwa ujumla sasahivi viwanda vinaweza kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini”, alisema Injinia Manyanya.

Pia alitoa wito kwa makampuni na sekta binafsi za Tanzania kushirikiana na makampuni hayo ya Ubelgiji ili kuingia ubia wa kuwekeza na kufanya biashara kwa lengo la kuimarisha sekta ya uwekezaji na biashara kwa manufaa ya Watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), John Mnali, alisema kuwa ugeni huo umekuja kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji pamoja na kufanya biashara kwenye sekta za utalii, umeme, viwanda na kilimo.

“Tumepata mwitikio mkubwa kwa sekta na makampuni binafsi kuja kushiriki kwenye kongamano na mazungumzo haya, kwa hiyo napenda kuwaomba Watanzania wenye makampuni kunapokuwa na makongamano kama haya wasibaki nyuma na sisi TIC jukumu letu ni kuwasaidia, hivyo basi watakaokubaliana watapata vibali na leseni za uwekezaji pamoja na biashara”, alisisitiza Mnali.

Kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Ubelgiji linafanyika Jijini Dar es Salaam kwa siku tatu na limezinduliwa na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Injinia Stella Manyanya.

No comments: