Wednesday, October 10, 2018

TAASISI YA AGRI THAMANI FOUNDATION YASAINI MKTABA WA MAKUBALIANO NA OFISI YA MKUU WA MKOA KUTOKOMEZA CHANGAMOTO YA LISHE KAGERA

Na: Sylvester Raphael

Taasisi mpya ya Agri Thamani Foundation iliyoanzishwa kwa lengo kuu la kuboresha lishe Mkoani Kagera na kuongeza ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika kuongeza Mnyororo wa thamani kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi imetiliana saini na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera katika Mkataba wa Makubaliano ili kuanza utekelezaji wa shughuli zake ifikapo Novemba Mosi, 2018.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation ambaye ni mzawa wa Mkoa wa Kagera Bi Neema Lugangira mara baada ya kutiliana saini kwenye Mkataba wa Makubaliano na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Nesphory Bwana alisema kuwa aliamua kuanzisha Taasisi hiyo kutokana na Mkoa wa Kagera kuwa na kiwango kikubwa cha watoto wenye udumavu na utapiamlo kutokana na kutopata lishe bora na stahiki.

“Nimeamua nianzishe Taasisi ambayo itausaidia Mkoa wetu wa Kagera hasa kuondoa udumavu kwa watoto kwani ukiangalia haraka utaona kuwa Mkoa wa Kagera kila zao linakubali kustawi lakini watoto hawapati lishe bora jambo ambalo linapelekea kudumaa kwao na mtoto akiwa na udamavu hawezi kuwa na kiwango kizuri cha akili hata kukua kwake kunaathirika.” Alieleza Bi Neema.

Bi Neema alieleza kuwa ili kufanikisha suala la kuondoa udumavu Kagera kwanza ni kuongeza ushiriki wa Wanawake na Vijana katika kuongeza Mnyororo wa Thamani katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo alitolea mfano katika kwenye kilimo kuwa Kagera kuna Mazao mengi lakini huenda akina mama hawajui namna bora ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao hayo lakini pia hawajui maana ya kufanya kilimo baishara ili kuingiza kipato na kuongeza ajira kwa vijana.

“Tutajikita katika Kilimo Biashara kwa kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao mfano mama anayelima viazi lishe afundishwe namna ya kukausha viazi hivyo na kuchanganya na mazao mengine na kutengeneza unga bora wa lishe, kwanza mama huyo watoto wake hawawezi kupata udumavu, pili atakuwa amejua namna bora ya kutunza unga wa viazi lishe badala ya kutunza viazi vyenyewe ambavyo mwisho wa siku vinaharibika.” Alifafanua Bi Neema

Bi Neema anasema kuwa Mkoa wa Kagera umebarikiwa kila zao kukubalika na wananchi wa Kagera wanalima mazao yote, masoko ya mazao hayo yapo lakini tatizo mazao hayo hayalimwi katika mfumo wa kuyaongezea Mnyororo wa Thamani yanapelekwa sokoni hivyo hivyo jambo ambalo linapelekea Mkulima kunyonywa lakini wakulima hanufaiki na mazao hayo kwani watoto wao utawakuta na udumavu kutokana na kutopata lishe bora.

Aidha, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Nesphory Bwana alimshukuru Bi Neema kuwa na wazo na akaamua kulifanyia kazi wazo hilo ili lifanye kazi katika Mkoa wa Kagera ambako yeye ni mzaliwa. “Ungeweza kuanzisha Taasisi kama hii lakini ukaipeleka mikoa mingine lakini wewe uliona uusadie Mkoa wako, kwaniaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera nakushukuru sana.” Alitoa Shukrani Bw. Nesphory.

Pia Bw. Nesphory alimhakikishia Bi Neema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ipo tayari kushirikiana naye ili kupunguza kiwanngo cha udumavu katika Mkoa wa Kagera. Vile vile Bw. Nesphory alimuomba Bi Neema kushirikiana na Mkoa katika kuelimisha wananchi wa Mkoa wa Kagera kuhusu Sera ya Ushiriki wa Watanzania (Local Content) katika miradi mbalimbali inayoyekelezwa au inayotarajiwa kutekelezwa mfano Mradi wa Bomba la mafuta, na Mradi wa Mapori ya Biharamulo Burigi na Kimisi (BBK) kuwa Hifadhi za Taifa.

Hapo awali Mkoa wa Kagera ulishaanza kuchukua hatua za kupambana na utapiamlo na udumavu wa wtoto ambapo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu mwezi Machi 2018 alizindua Kampeni ya kila kaya kuwa na angalau miche mitano ya matunda kuzunguka nyumba ili watoto wapate matunda aina mbalimbali kwaajili ya lishe bora na kuhamasisha ulaji matunda hayo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo Mstaafu Mhe. Kijuu aliziagiza Taasisi zote za Serikali na zisizokuwa za Serikali kuhakikisha zipanda miche ya matunda katika maenneo ya Taasisi hizo. Pia alitoa wito kwa baadhi ya Taasisi hizo kugharamia uanzishwaji wa vitalu vya miche ya matunda ili kuigawa miche hiyo kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kuinunua ili wapewe bure kuipanda katika kaya zao.

Kitakwimu Katika Mkoa wa Kagera Asilimia 39.1% ya wanawake kati miaka 15 hadi 49 wana upungufu wa damu, Asilimia 57.2% ya watoto chini ya miaka mitano wana upungufu wadamu, na Asilimia 41.7% ya watoto chini ya miaka mitano wana udumavu. Aidha, Kitaifa Mkoa wa Kagera unashika nafasi ya nne katika mikoa kumi ya mwanzo inayoongoza kwenye udumavu wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano Rukwa ikiongoza na asilimia 56.3% na Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa kwa asilimia 14.6% (Kwa Mujibu wa “Tanzania Demographic and Health Survey” 2015/2016)

Bi Neema Lugangira anasema kuwa fursa za kuboresha lishe zipo katika Mashirika mengi ya Kimataifa lakini mpaka atokee mtu au Taasisi itakayokuwa na malengo thabiti ya kutekeleza miradi kama hiyo na ikaleta matokeo chanya kwenye eneo husika kama yeye na Taasisi yake anavyolenga kufanya.

Taasisi mpya ya Agri Thamani Foundation ilianzishwa Mwezi Julai 2018 na Bi Neema Lugangira ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Mlezi wake ni Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Kayanza Peter Pinda. Aidha, Taasisi hiyo inatarajia kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi mwezi Novemba 2018 baada ya kutiliana saini katika Mkataba wa Makubaliano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Oktoba 10, 2018 na ofisi za Taasisi hiyo zitakuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Kagera.
 Bi Mwasham Msabaha Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation akisaini Mkataba wa Makubaliano
 Bi Neema Lugangira Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation Akimsikiliza Kaimu Katibu Tawala Bw. Nesphory Ofisini Kwake
 Bi Neema Rugangira Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation akisaini Mkataba wa Makubaliano
 Bi Neema Rugangira Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation na Kaimu  Katibu Tawala Mkoa Bw. Nesphory Bwana  Wakisaini Mkataba wa Makubaliano.
 Bi Neema Rugangira Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation na Kaimu  Katibu Tawala Mkoa Bw. Nesphory Bwana Wakipeana Mikono Baada ya Kusaini Mkataba

 Kabla ya Kusaini Mkataba wa Makubaliano.
 Kaimu  Katibu Tawala Mkoa Bw. Nesphory Bwana  akisaini Mkataba wa Makubaliano Pamoja Bw. Isaya Tendega Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji.
 Kaimu  Katibu Tawala Mkoa Bw. Nesphory Bwana  akisaini Mkataba wa Makubaliano.
Picha ya Pamoja

No comments: