Friday, October 12, 2018

SHUBASH PATEL ATOA MABATI 1,000 KUIMARISHA SEKTA YA ELIMU PWANI


NA MWAMVUA MWINYI,PWANI 

SEKTA ya elimu mkoani Pwani, inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa 3,678 katika shule za msingi pamoja na nyumba za walimu 5,188.


Kufuatia changamoto hiyo ,kampuni ya Sayona fruits ,iliyopo Mboga huko Chalinze imetoa mabati 1,000 yenye thamani ya sh.mil 24 ,kwa ajili ya umaliziaji wa majengo mbalimbali ya shule za msingi mkoani humo .

Akipokea mabati hayo ,kutoka kwa mkuu wa kitengo cha mahusiano cha kampuni hiyo ,Abubakar Mlawa , mkuu wa mkoa wa mkoa huo mhandisi Evarist Ndikilo alisema ,wanakabiliana na changamoto hizo kwa kushirikiana na halmashauri,jamii na wadau wa elimu . “Miundombinu ya shule za sekondari na hasa shule za msingi bado kuna upungufu ,ambapo mkoa una jumla ya shule za msingi 613 huku za serikali zikiwa ni 562 na 51 ni za watu binafsi “

“Shule za msingi pekee mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 700,671, yaliyopo 3,993 na upungufu ni vyumba vya madarasa 3,678 ” alifafanua Ndikilo. Ndikilo alitaja pia tatizo la nyumba za walimu ili waweze kuishi vizuri hivyo kuna mahitaji ya nyumba hizo 6,779 . Alisema ,nyumba zilizopo ni 1,591 na upungufu ni nyumba za walimu 5,188.#

“Mtaona ni namna gani bado tuna changamoto za miundombinu kwenye sekta ya elimu ambapo inasababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kusoma kwenye mazingira bora na walimu kufundisha katika mazingira yasiyo ridhisha ” alisisitiza. Hata hivyo akimshukuru mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Sayona Shubash Patel ,Ndikilo alisema ni mdau mkubwa kimkoa kwani amekuwa akisaidia kwenye sekta mbalimbali . Alielezea kati ya mabati hayo,yataanza na shule yetu ya msingi Mkoani kwani ina mahitaji mengi na kumalizia majengo mengine katika shule nyingine.

Awali akikabidhi mabati hayo , Abubakar Mlawa alisema ,msaada huo utawezesha kuezeka baadhi ya vyumba vya madarasa ,matundu ya vyoo na nyumba za walimu. Alieleza ,licha ya kuwekeza lakini pia wanashiriki kusaidia huduma za kijamii ikiwemo kuboresha sekta ya elimu . “Sayona lengo lake kubwa ni kuweka mazingira bora ya kusoma kwa wanafunzi wetu ,hivyo tumekuja kukukabidhi mabati haya 1,000”; alisema Mlawa . Nae ,ofisa elimu wa mkoa wa Pwani ,Abdul Maulid aliwashukuru Sayona kwa msaada huo ambao unakwenda kuimarisha sekta ya elimu .

Alitoa rai na kuwaomba wawekezaji wengine kujitoa kusaidia sekta ya elimu kwa kuiga mfano wa kampuni ya Sayona.

Akipokea msaada wa mabati , mkuu wa mkoa wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto )kutoka kwa mkuu wa kitengo cha mahusiano cha kampuni ya Sayona fruits iliyopo Mboga Chalinze ,Abubakar Mlawa (kulia) ,msaada ambayo umeelekezwa kuimarisha sekta ya elimu .( picha na Mwamvua Mwinyi )

No comments: