Thursday, October 4, 2018

RC NDIKILO AONYA AMCOS,WATU WANAOSHAWISHI WAKULIMA WA KOROSHO KUKATAA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA

SERIKALI Mkoani Pwani, imetoa onyo kwa watu ama vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS ) wanaoshawishi wakulima kukataa mfumo wa stakabadhi ghalani pamoja na kupeleka korosho kwenye maghala makubwa na badala yake wanawarubuni kuuza kwa mtindo wa kangomba .

Aidha umetoa wito ,kwa wadau mbalimbali kujenga ghala la Kibiti ili yaweze kupewa leseni ya kutumika katika msimu ujao wa ukusanyaji na ununuzi wa korosho .Akifungua mkutano wa wadau wa zao la kibiashara la korosho ,wilayani Mkuranga ,mkuu wa mkoa huo ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema ,yeyote aliyejipanga kukataa mfumo huo ni mhujumu uchumi na biashara hiyo haikubaliki.

Alisema, kuwa na maghala machache ni mpango wa serikali hivyo hawatakuwa na nafasi ya kutumia maghala ya vichochoroni ambayo yameshasababisha changamoto nyingi msimu uliopita ."Tunazijua Amcos ambazo zilitutia doa ,tuwajua majina na mipango wanayoyafanya ,nawataadhalisha kabisa ,hatutaki tuharibu sifa yetu tena "tutamnyakua mmoja baada ya mmoja "

Ndikilo pia alikemea, baadhi ya wanunuzi wa korosho waache kuhujumu uchumi kwa kushinda minada kisha kushindwa kulipia kwa wakati na makubaliano ya mkataba na kuanzia sasa hawatawachekea wanunuzi wa aina hiyo."Msimu huu unaokuja hatutaki utani ,tumechoka kuwa kichwa cha wendawazimu ,kila mmoja anufaike mnunuzi na mkulima bila kumyanyasa mkulima " alibainisha.

Alielezea ,tangu wameanza kutumia mfumo huo msimu wa mwaka 2015/2016 waliuza tani 8,800 ,mwaka 2016/2017 tani 13,300 na msimu wa 2017/2018 tani 20,650 hivyo kila msimu umekwenda ukiongezeka kwa uzalishaji.


Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa ,bei nayo imepanda mwaka hadi mwaka kwa mwaka 2015/2016 ilikuwa sh.2,900 kwa kilo ya korosho kwa daraja la kwanza,ambapo 2017/2018 korosho daraja hilo iliuzwa kwa sh. .3,800 na kuongeza mapato .Ndikilo alifafanua ,haikuwa rahisi kufikia malengo hayo kwani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maghala madogo,yasiyo na ubora na kuathirika kwa ubora wa korosho katika msimu uliopita na uhaba wa magunia .

Hata hivyo ,alitaka magunia ya mkoa yasiangukie kwa watu asiowaaminifu ili kuendelea kulinda korosho ya mkoa huo .Awali meneja uratibu huduma ,kutoka bodi ya usimamizi wa stakabadhi za maghala ,Temu fidelis alisema kuna maghala mawili yaliyosajiliwa likiwemo la Mkuranga ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 15,000 za korosho na litahifadhi korosho za wakulima kutoka Mkuranga ,Mafia ,Kibiti ,Rufiji .

Alitaja ghala jingine ni la Tanita wilayani Kibaha ambalo litahifadhi tani 5,000 za korosho kutoka Kibaha ,Kisarawe ,Bagamoyo na Chalinze ,na maghala hayo yataendeshwa na mwendesha ghala .Katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji ,Shangwe Twamala aliwasihi ,wakulima wa mkoa wa Pwani wasirudi nyuma ili kupata manufaa.

Nae kaimu naibu mrajis -uthibiti kutoka tume ya maendeleo ya ushirika Tanzania ,Collins Nyakunga alibainisha , mwaka jana walifanya uchunguzi na kubaini kuna uhuni unafanywa na baadhi ya AMCOS ikiwemo kufanya ubabaishaji na kusababisha hasara .

Alisema ,chama cha ushirika kinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na mtendaji anaajiriwa kama mwajiri mwingine na ukiona unashindwa kutekeleza majukumu yako acha kazi nafasi hiyo apewe mwingine.
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo akifungua mkutano wa wadau wa zao la kibiashara la korosho ,wilayani Mkuranga

 Baadhi ya washiriki kwenye mkutano wa wadau wa zao la kibiashara la korosho ,wilayani Mkuranga ,Mkoani Pwani .(picha na Mwamvua Mwinyi )
 Kaimu naibu mrajis -uthibiti kutoka tume ya maendeleo ya ushirika Tanzania ,Collins Nyakunga akitolea ufafanuzi jambo wakati wa mkutano wa wadau wa zao la kibiashara la korosho ,wilayani Mkuranga ,mkoani Pwani.
 Katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji ,Shangwe Twamala akizungumza jambo katika mkutano wa wadau wa zao la kibiashara la korosho ,wilayani Mkuranga ,Mkoani Pwani.(picha na Mwamvua Mwinyi 

No comments: