Tuesday, October 2, 2018

MAHAKAMA YAGOMA KUFUTA KESI YA TUHUMA ZA UTAKATISHAJI FEDHA INAYOMKABILI AVEVA,NYANGE

Na Karama Kenyunko,Globu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haiwezi kifuta kesi ya utakatishaji wa fedha inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange maarufu Kaburu sababu kesi hiyo imeishafikia hatua ya usikilizwaji wa awali.

Badala yake Mahakama kwa mara nyingine, imetoa amri na kuwapa siku 14 upande wa mashtaka kutekeleza amri iliyoitoa ya kuwataka aidha wafute mashtaka dhidi ya Zacharia Hanspoppe na mfanyabiashara, Franklin Lauwo au wabadilishe hati ya mashtaka kwa kuwaondoa washtakiwa hao ili kesi isikilizwe.

Uamuzi huo umetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kutokana na ombi la mawakili wa washtakiwa hao wakiongozwa na Nehemia Nkoko kuiomba mahakama ifute kesi hiyo kwa sababu upande wa mashtaka wameshindwa kuiendesha.

Akisoma uamuzi huo hakimu Simba amesema amepitia hoja za pande zote mbili na ameona kuwa, huu si muda muafaka wa kufuta kesi hiyo kwa sababu tayari ilikuwa katika hatua ya (PH) na pia ilishatoa amri ambayo bado haijatekelezwa.Hakimu Simba amesema upande wa mashtaka wanatakiwa watekeleze amri iliyotolewa Mei 12 mwaka ,2018, kwa hiyo haiwezi kufuta kesi hiyo, kwa sababu itafuta hadi amri ambayo tayari ilishaitoa na haijatekelezeka.

"Si muda mwafaka wa kufuta kesi hii, natoa siku 14 kuanzia kesho kwa upande wa mashtaka kufanya mabadiliko na kama hawatafanya hivyo, Mahakama inaweza kuamua vingine itakavyoona inafaa, " amesema Hakimu Simba.Aidha Hakimu Simba ametaka amri hiyo itekelezeke kwa sababu hawajulikani ni lini Hansoppe na Lauwo watakamatwa  wakati Aveva na Kaburu wapo mahabusu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 16 mwaka 2018 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa PH.Awali, Wakili wa utetezi, Nkoko aliomba Mahakama hiyo iwafutie mashtaka, washtakiwa hao kwa sababu wameshindwa kuiendesha kesi hiyo.Akijibu hoja hiyo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidia na Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai,  aliiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu bado wanaifanyia kazi amri waliyopewa na mahakama ya kumtafuta Hanspope na Lauwo.

Amedai Septemba 14 mwaka huu, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa wanawatafuta Hanspope na Lauwo jambo ambalo ni moja ya utekelezaji wa amri iliyotolewa na mahakama.

Katika kesi hiyo washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 10 likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

No comments: