Saturday, October 27, 2018

LUKUVI AAGIZA WALIOKUWA WAFANYAKAZI WA USHIRIKA KUTOONDOLEWA ENEO LA LAMBO ESTATE NA KUPATIWA EKARI MBILI KILA MMOJA

HAI, KILIMANJARO-

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amekata mzizi wa fitna ambapo ameagiza waliokuwa wafanyakazi wa chama cha ushirika katika eneo la Lambo Estate Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro kutoondolewa katika eneo hilo na kila mmoja kupatiwa ekari mbili kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kimaisha.

Uamuzi huo wa Lukuvi wa kutoa ekari mbili kwa wananchi 78 unafanya kutolewa kwa jumla ya ekari 156 kati ya ekari 1600 na unatokana na mgogoro wa muda mrefu baina ya waliokuwa wafanyakazi wa ushirika na uongozi .Mgogoro uliibuka baada ya wafanyakazi hao kutakiwa kuondoka katika makazi yaliyopo kwenye eneo la shamba kutokana na utumishi wao kukoma.

Waziri Lukuvi alitoa maamuzi hayo katika wilaya Hai ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kutembelea wilaya za Hai, Moshi na Same kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya hizo mkoa wa Kilimanjaro. Mhe Lukuvi ameshangazwa na ushirika wa watu wachache kutaifisha ardhi na kuamuru watu waliokuwepo muda mrefu katika eneo la lambo estate kuondoka na kusema kuwa safari hii serikali itawanyoosha wale wote wanaofanya ujanja wa kuwaonea wanyonge. *”Sijawahi kuona ushirika wa namna hii ambapo wenye rasilimali hawanufaiki na ardhi iliyopo katika kijiji chao halafu ardhi hiyo inakodishwa kwa wanachama wa ushirika wanaotoka vijiji vingine”* alisema Waziri Lukuvi.

Huku akishangiliwa na wananchi wakati akitoa maamuzi hayo, Mhe. Lukuvi alisema amekwenda katika eneo hilo la Lambo Estate kushughulikia mgogoro wa ardhi. Suala la ushirika litashughulikiwa na waziri mwenye dhamana na vyama vya ushirika ambae ataamua iwapo ushirika huo unafaa. Waziri Lukuvi alisisitiza kuwa, serikali haiwezi kuwaondoa wazee walioishi kwa muda mrefu. Waziri wa Ardhi ametoa maagizo kwa wananchi watakaopewa ekari mbili kuwa maeneo watakayopatiwa ni kwa ajili ya kufanyia shughuli zao na hawaruhusiwi kuuza na kwa yeyote atakayeamua kuondoka eneo hilo basi eneo hilo litabaki kuwa la serikali.

Kufuatia maelekezo hayo Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kuanza mara moja zoezi la kuwagawia wananchi ekari hizo kama ilivyoagizwa na mhe Lukuvi.

Awali Katibu wa jumuiya ya wanaushirika Edward Chedi alimueleza Mhe Waziri Lukuvi kuwa mgogoro wa eneo hilo ulianza mara baada ya shamba hilo kutaifishwa na ajira za walikuwa wafanyakazi wa ushirika kukoma mwaka 2001 na kuwepo mfululizo wa kesi uliofikia ngazi ya Mahakama Kuu na kuagizwa waliokuwa wafanyakazi kulipwa mafao na kukabidhiwa vyeti vya kutambuliwa pamoja na ekari hamsini za kujikimu kwa kipindi watakachokaa hapo kabla ya kuondolewa. 

No comments: