Thursday, October 25, 2018

JAJI MRUMA AKAGUA MRADI WA UJENZI WA MAHAKAMA YA MWANZO MAGOMA-KOROGWEMuonekano wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Magoma lililopo katika hatua za mwisho za ujenzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amiri Rajabu Mruma (kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Fundi wa Kampuni ya SUMA JKT alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Magoma Wilayani Korogwe.
Mhe. Jaji Mruma akiendelea na ukaguzi.
Jaji Mruma akitoa elimu kwa Wajumbe wa Kamati ya maendeleo ya Kata ya Hale Wilayani Korogwe.
Mhe. Jaji Mruma (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya maendeleo ya kata ya Hale. Mstari wa kwanza kulia ni Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe, Bw. Emmanuel Machimo akifuatiwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Bw.Ahmed Ng’eni.
(Picha na Amina Ahmad, Mahakama Kuu, Tanga)Na Amina Ahmad, Mahakama Kuu, Tanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Amir Mruma amemuhimiza Mkandarasi SUMA JKT kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Magoma iliyopo Wilayani Korogwe ili ianze kutumika mara moja.

Akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Korogwe; Mhe. Jaji Mruma alipata fursa ya kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mahakama hiyo Oktoba 23 ambapo hata hivyo aliridhishwa na hatua iliyofikiwa.

Katika ziara yake Wilayani humo, Mhe. Jaji Mfawidhi alifanikiwa pia kukutana na Kamati za Maendeleo za Kata ya Magoma na Mashewa na kutoa elimu juu ya haki na wajibu wa wananchi katika migogoro ya ardhi, kesi za ubakaji, mimba za utotoni na usimamizi wa Mirathi.

Kwa upande wao; Wajumbe wa Kamati za Maendeleo (WDC) walitoa shukrani zao za dhati kwa Jaji Mfawidhi kwani ilikuwa ni mara yao ya kwanza kukutana na Jaji na kupewa elimu ya kisheria, hali iliyowapelekea kumuomba Jaji Mfawidhi aendelee na utarabu wa kukutana nao mara kwa mara kuwajengea wigo na uelewa mpana wa masuala ya kisheria ili kufanikisha majukumu yao.

Sambamba na hilo, wajumbe hao walipongeza pia huduma zinazotolewa na Watumishi wa Mahakama na kukiri kwamba hakuna malalamiko yoyote juu ya huduma za Mahakama katika vituo vyao.

Mhe. Jaji Mruma anatarajia kuendelea na ziara hiyo kwa kuongea na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Korogwe, kukagua Mahakama ya Wilaya Korogwe, Mahakama za Mwanzo Old Korogwe, Manundu, Bungu na Vugiri.

Vilevile atazungumza na Watumishi wa Mahakama hizo, Kamati za maendeleo za Kata zilizomo Mahakama husika pamoja na wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Manundu na Gereza la kilimo Kwa Mgumi lengo likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji haki kwa ujumla.

No comments: