Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa shughuli za mfuko wa Bima ya Afya(NHIF) kwenye kamati ya
kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo jijinini Dodoma
ambapo alisema wachangiaji wa mfuko huo wameongezeka kutoka wanachama
164,706 mwaka 2001/2002 hadi wanachama 873,012 septemba mwaka huu.
Mkurugenzi wa NHIF Bw.Bernad
Konga akijibu maswali kutoka kwa wajumbe wa kamati ambapo alisema mfuko
wake upo tayari kuanza mara moja kutoa huduma kupitia vifurushi vipya
vitakavyojulikana kama JIPIMIE ili watanzania waweze kupata huduma za
matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini
Wakurugenzi wa NHIF wakipitia taarifa ya mfuko huo wakati ikiwasilishwa kwenye kamati mapema leo
Waziri Ummy Mwalimu akiwasilisha
taarifa ya NHIF kwa kamati na kusema kuwa Mpango wa Wizara ni
kuhakikisha wagonjwa wa mfuko huo wanapata huduma nzuri kupitia vituo
vyote vya afya 7,142 vinavyotoa huduma za NHIF vikiwepo vile vya
binafsi.
Katibu Mkuu Afya Dkt.Mpoki
Ulisubisya(wa kwanza kulia),Mkurugenzi wa NHIF Bw.Benard
Konga(anayefuata)pamoja na wakurugenzi wengine wa Wizara na NHIF
wakifuatilia taarifa hiyo.
.WazirinUmmy Mwalimu akifafanua jambo mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo jijini Dodoma.
Waziri Ummy Mwalimu akijadiliana
jambo na Katibu Mkuu wa Idara Kuu Afya Dkt.Mpoki Ulisubisya(mwenye
miwani)na Mkurugenzi wa NHIF Bernad Konga
Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo
wakimsikiliza Waziri wa Afya(hayupo pichani)akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa Mfuko wa bima wa NHIF(Picha zote na Wizara ya Afya)
Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe.Peter Serukamba akichangia taarifa hiyo
Na.WAMJW,Bungeni,Dodoma
Idadi ya wanachama wachangiaji wa
mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeongezeka kutoka wanachama 164,708
waliokuwa wameandikishwa mwaka 2001/2002 hadi wanachama 873,012 mwezi
Septemba 2018.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mfuko huo kwenye
kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Bungeni jijini
Dodoma.
“Ongezeko hili limetokana na
kanuni na misingi inayotumika katika kuendesha utaratibu wa mfuko huu
ikiwa ni pamoja na uchangiaji wenye usawa kwa kuzingatia viwango vya
mshahara,usawa katika kupata huduma na ushiriki wa Serikali katika
usimamizi kwa faida ya wanachama” alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa kwa
upande wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), jumla ya kaya zilizojiunga hadi
Septemba mwaka huu ni 2,220,953 ikiwa ni sawa na wanufaika wapatao
13,506,330 sawa na asilimia 25 ya watanzania wote’ kwa hiyo mifuko hii
yote inatoa huduma kwa watu 17,656,697 sawa na asilimia 33 ya watanzania
wote kwa mujibu wa idadi ya makadirio ya watanzania kwa sasa.
Idadi ya wanufaika imeongezeka
kutoka 691,774 mwaka 2001/2002 hadi wanufaika 4,150,367 sawa na
asilimia 8 ya watanzania wote” alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa
mpaka sasa idadi ya wanachama wengi waliojiunga asilimia 67 ni
watumishi wa umma ambao wanajiunga kwa mujibu wa sharia.
Hata hivyo Waziri Ummy alisema
mfuko unaendelea kutoa elimu na kubuni vifurushi mbalimbali
vitakavyovutia wananchi wengi kujiunga na kufaidika na mfuko ambapo
utawawezesha wanachama wengi zaidi kujiunga hasa wale wa sekta isiyo
rasmi na kujiwekea malengo ya kuwafikia watanzia asilimia 50 mwaka 2020.
“Mfuko umekamilisha uandaaji wa
vifurushi vya michango na mafao kulingana na uwezo wa wananchi kulipia
bima ya afya,suala hili lipo katika hatua za mwisho kabla ya kuanza kwa
utekelezaji”. Alisisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa mpango
huo utamwezesha mwananchi kuchagua vifurushi vya aina mbalimbaliu vya
huduma anayoitaka kwa utaratibu utakaojulikana kama ‘JIPIMIE’ na
wanachama watalipa kidogo kidogo kwa utaratibu ujulikanao kama
‘DUNDULIZA’ ambao tayari umeshakamilika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe.
Peter Serukamba amesema kuwa NHIF wanatakiwa kuweka mfumo wa kutoa
huduma za bima ya afya kwa mashirika makubwa ya hapa nchi na yale ya nje
kwa kuwauliza huduma zipi wangependa kuhudumiwa katika hospitali za
hapa nchini hususan zile za binafsi na hivyo kuweza kuongeza idadi kubwa
ya wateja watakaohudumiwa na NHIF.
Naye Mkurugenzi wa NHIF Bw.
Bernad Konga akijibu maswali ya wajumbe wa kamati hiyo alisema kwamba
NHIF imekubali kuboresha huduma zao na hivyo wapo tayari kuanza huduma
za vifurushi za ‘JIPIMIE’ mara moja ili wananchi waweze kupata huduma
za afya kulingana na vipato vyao.
Aidha, alisema hivi sasa
wameajiri madaktari wapatao kumi na nane na kuwaweka kwenye hospitali
kubwa za Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutatua changamototo za
wateja wa huduma za bima hiyo zikiwemo za kunyanyapaliwa pamoja na
kukagua fomu zinazojazwa na wataalam wa hospitali hizo ili kupunguza
malalamiko ya wateja wa huduma za bima ya NHIF na kuahidi wataongeza
hospitali zingine awamu inayofuata
No comments:
Post a Comment