Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limeanza operesheni maalumu ya kukamata bodaboda zote zinazoingia katikati ya Jiji ambapo ndani ya saa 24 wamekamata pikipiki 104.
Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa wakati anazungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni ambazo wanazifanya.
Amefafanua Polisi wameanza operesheni ya kukamata waendesha bodaboda ambao wanaingia katikati ya mji wakati wamezuiliwa kuingia mjini.Kamanda Mambosasa amesema baadhi ya bodaboda ambazo zimekamatwa zimetokana na makosa ya kutovaa kofia ngumu kwa wanaoendesha,kupitia njia tofauti na utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na kupakia mishikaki.
"Ni marufuku bodaboda kuingia katikati ya Mji,hatuwezi kuacha hilo likaendelea kufanyika.Walishakatazwa kuingia katikati ya mji." Mbali ya kuwakamata wanaiongia mjini pia tunaendelea na operesheni ya kukamata bodaboda ambazo zinatumika kutenda matukio ya uhalifu.Pia tutakamata bodaboda ambazo wanaoziendesha wanashindwa kufuata sheria za usalama barabarani.
*Bodaboda zimekuwa kero kubwa kwa wananchi kwani wamekuwa wakichangia kusababisha ajali kwa kupitia barabara ambazo haziruhusi.Barabara ya kwenda wao wanaitumia kwa kurudi tena wakiwa wamebeba mishikaki."Wengine wanapita hapa hapa nje Ofisi za Jeshi la Polisi na hawana wasiwasi.Tunajua tunapozungumzia bodaboda kunakuwa na maneno mengi lakini lakini niseme watu wafuate maelekezo ambayo tunayatoa," amesema Mambosasa.
Ameongeza kutokana na operesheni hiyo wameshakamata bodaboda 104 kutokana na makosa mbalimbali likiwamo la kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.Pia amesema kwamba kuna baadhi ya waendesha bodaboda kabla ya kufanya makosa wanaandaa faini na kisha wanalipa.Hivyo amesema inaonekana faini zimezoeleka na hivyo wahusika watapelekwa mahakamani.
Wakati huo huo Mambosasa amesema Polisi kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania(Tanesco) wamefanikiwa kukamata watu 60 ambao wanatuhumiwa kujihusisha na kuhujumu miundombinu ya umeme na kujiunganishia umeme bila itaratibu na kuchezea mita za Luku.Kamanda Mambosasa amesema wapo ambao wamefikishwa mahakamani na wengine wanaendelea kuhojiwa na kisha watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Amesema kuwa wanaojihusisha na kuhujumu miundombinu ya umeme wafahamu opereshenii hiyo ni endelevu na kwamba watakaoendelea wajue wao ni wafungwa watarajiwa kwani hatabaki salama.
No comments:
Post a Comment