Na Asha Ngoma
Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation na mvumbuzi wa madini ya Tanzanite Mzee Jumanne Mhero Ngoma wameadhimisha miaka 51 tangu madini hayo yagunduliwe mwaka 1967 katika hotel ya Serena Hotel jijini Dar es salaam.
Hata hivyo sherehe hizo hazikuwa na shamrashamra zilizoandaliwa na badala yake wakafanya Press conference baada ya kuahirisha sherehe kutokana na maombolezo ya kitaifa ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere huko Ukara, Mkoani Mwanza.
Tanzanite Founder Foundation ni Taasisi isiyo ya kiserikali lilioanzishwa na kusajiliwa mwaka 2013 ikiwa na lengo kuu la kuwajengea uwezo vijana na watu wote waishio migodini na maeneo jirani ili kuboresha na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku kutokana na madini haya.
Tanzanite Founder Foundation na wadau leo
imeona iadhimishe miaka 51 tangu madini haya ya kipekee duniani kuvumbuliwa nchini Tanzania.
Madini haya husheherekewa ulimwenguni na mashirika, taasisi na wafanya biashara Mbalimbali wa madini lakini hayajawahi kusherehekewa wala kuadhimishwa nchini Tanzania. Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation imeona iadhimishe siku hii kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu madini haya ikiwa ni pamoja na kutoa historia fupi ili kutoa tathmini ya tulipotoka na tulipo kwa sasa ikiwa ni pamoja na kudhihirishia ulimwengu kuwa Tanzanite ni fahari yetu na urithi wetu watanzania.
Madini ya Tanzanite yalivumbuliwa mwaka wa 1967 na Mzee Jumanne Mhero Ngoma ambaye ni Mtanzania, a iyaokota madini haya katika eneo la Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Arusha wakati huo na kuyapeleka kwa ofisi ya Madini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro ambayo nayo hawakuyatambua ni madini gani.
Wakashauri wayachukue wayapeleke katika maabara ya madini ya Taifa iliyopo Dodoma. Mnamo Septemba 23, 1967 Mjiolojia Mkuu wa Serikali Ndugu Ian McClouds alitoa majibu ya kimaabara ya utambulisho na uthibitisho kuwa Madini haya ni jamii ya Zoisite na kuthibitisha kuwa yatakua na thamani baadae.
Hili lilithibitishwa baadae na majiolojist wengine kutoka vyuo mbali mbali kama Gemological Institute of America, Havard University, British Museum na Heideberg University. Majibu haya ya kimaabara alipewa Mgunduzi wa madini hayo ambaye ni Mzee Jumanne Mhero Ngoma.
Serikali iliendelea kutambua na kuthibitisha ugunduzi huo ambao Mzee Jumanne Mhero Ngoma alifanya na alipewa hati ya Mtu wa Kwanza Kugundua Kito kiitwacho Tanzanite na serikali ya awamu ya kwanza katika sherehe za Mei Mosi zilizofanyika Mkoani Mbeya mwaka 1984 na pia serikali ya awamu ya Nne katika sherehe za Muungano zilizofanyika Ikulu mwaka 2015.
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alimpatia Tuzo ya Daraja la pili kwa kutambua ugunduzi wake. Tunashukuru serikali ya awamu ya Tano ya Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa kumtangaza rasmi kuwa ndiye mgunduzi wa madini ya TANZANITE wakati wa uzinduzi wa ukuta unaozunguka eneo la Migodi ya Madini ya Tanzanite - Mirerani. Hivyo madini haya ni ya kwetu Watanzania na tujivunie urithi wetu.
Madini haya adimu yalibadilishwa jina na kampuni ya uuzaji madini inayojulikana kama Tiffany & co. mnamo mwaka 1968 kwa ajili ya kampeni ya kuyatangaza madini hayo.
Kampuni hiyo ilipendekeza madini haya yaitwe TANZANITE badala ya Zoisite kwa kuwa yanatoka Tanzania. Tangu kuvumbuliwa kwa madini ya TANZANITE na kukua kwa soko la madini hayo adimu eneo la Mirerani lilijaa wachimbaji na wanunuzi wengi kiasi cha kufikia Mwaka 1971 migodi ya TANZANITE ikawa chini ya serikali kwa sababu ya kutokua na usimamizi mzuri wa uchimbaji holela na wizi wa madini uliokithiri.
Makampuni kutoka nje ya nchi na ndani ya nchi walianza kuchimba na kuuza TANZANITE na kukawa na migogoro ambayo ilipelekea serikali kugawa eneo A, B C na D ya maeneo ya machimbo ili kupunguza migogoro. Kwa kuzuia wizi uliokithiri serikali ya awamu ya tano ya Rais John Pombe Joseph Magufuli ikaamua kujenga ukuta unaozunguka eneo la migodi ya madini ya Tanzanite, jambo ambalo litaongeza thamani zaidi ya madini ya Tanzanite na kutarajiwa kupanda kwa bei katika siku za usoni.
Madini ya Tanzanite ni adimu mara 1000 ukilinganisha na almasi. Kwa sasa madini ya Tanzanite ni ya pili kwa thamani Duniani katika kundi la madini ya vito. Pia iliingizwa kwenye rekodi ya dunia kama madini ya siku ya kuzaliwa ya Desemba (December Birth stone) pia madini haya yanatambulika sehemu nyingine kama madini ya kusherehekea miaka 24 ya ndoa (24th wedding anniversary) Duniani.
Kwa kutambua umuhimu wa madini haya ya Tanzanite hufanya sherehe za kujiongezea soko la madini haya ikiwa ni pamoja na kuyatangaza kuwa yanatoka nchini mwao kama vile nchi ya Kenya, India na sasa China ambao ni wauzaji wakuu wa madini haya nchi za Ulaya, Marekani na bara la Asia. Nadhani kwa sasa kuna umuhimu kuadhimisha siku hii na kudhihirishia ulimwengu ukweli kuwa Madini ya Tanzanite yanatoka Tanzania na ni urithi wetu na huu ndio uzalendo wetu badala ya kukaa kimya na wageni kutoka nje ya nchi kutangaza kuwa ndio waliovumbua madini haya ya Tanzanite jambo ambalo sio kweli ni muhimu kuweka mambo wazi na ukweli ujulikane ulimwenguni. Tusiposema sisi watasema wao na watatunyang'anya hata urithi wetu.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation Bi. Asha Ngoma akiwa na mvumbuzi wa madini ya Tanzanite Mzee Jumanne Mhero Ngoma (wa pili kushoto) na watendaji wa taasisi hiyo katika mkutano na wanahabari katika kuadhimisha miaka 51 tangu madini hayo yagunduliwe mwaka 1967 huko Mirerani. Mkutano huo umefanyika leo katika hotel ya Serena jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation Bi. Asha Ngoma akipongezana na mvumbuzi wa madini ya Tanzanite Mzee Jumanne Mhero Ngoma
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation Bi. Asha Ngoma akiwa na mvumbuzi wa madini ya Tanzanite Mzee Jumanne Mhero Ngoma
No comments:
Post a Comment