Sunday, July 1, 2018

Viongozi wa Mahakama Wakumbushwa Kusimamia Utendaji wa Madalali


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha viongozi wa Mahakama kusimamia kwa makini upangaji na utendaji wa madalali ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za wadaawa.

Jaji Mkuu, Prof. Juma ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akikabidhi hati 24 za uteuzi kwa Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa pamoja na kushuhudia uapisho wa Naibu Wasajili 9 uliofanywa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Eliezer Feleshi.

Prof. Juma amesema kuwa mara nyingi shughuli za madalali hulalamikiwa, wananchi wanafahamu kuwa madalali ni sehemu ya Mahakama kwahiyo eneo hilo lazima liangaliwe kwa umakini hasa pale fedha za wadaawa zinapotumiwa vibaya na baadhi ya madalali.

“Pamoja na Kanuni za sasa kuwataka madalali wapitie mafunzo lakini bado mna wajibu wa kusimamia majukumu yao, pia tunazifanyia mabadiliko kanuni za madalali ambapo watalazimika kuweka fedha zote kwenye akaunti ya Mahakama kabla ya kuweka katika akaunti zao ili tuweze kudhibiti matumizi mabaya ya fedha ambazo ni dhamana kwa wananchi,” alisema Prof. Juma.

Prof. Juma ameongeza kuwa upangaji wa kesi ni eneo lingine linalotakiwa kusimamiwa kwa umakini kwani kesi zinatakiwa zipangwe kwa kuzingatia muda wa kusajiliwa au vipaumbele maalum kama maelekezo yanavyotolewa na viongozi wa Mahakama hali itakayosaidia kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Aidha, amewataka viongozi hao kuwa kichocheo cha maboresho ya Mahakama ya Tanzania pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa na bila upendeleo wowote huku wakizingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa.

Vile vile amewakumbusha kuwa uteuzi wao ni ishara tosha kwamba wameaminiwa kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ngazi hizo za uteuzi na wameshakuwa walezi wa watumishi katika maeneo yao hivyo ni jukumu lao kuwatambua viongozi wa baadae ambao watachukua nafasi zao.

Akiongelea kuhusu mfumo wa kisasa wa kielektroniki katika utoaji wa huduma, Prof. Juma amesema kuwa mfumo huo wa kufungua mashauri kwa njia ya kielektroniki utasimamiwa na Msajili Mkuu ambapo vitaanzishwa vibanda vya kuwasaidia wananchi kufungua mashauri kwa kielektroniki lengo likiwa ni kumaliza kabisa tatizo la upoteaji wa majalada.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikabidhi hati za uteuzi kwa baadhi ya Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa wakati wa sherehe za kuwakabidhi hati Mahakimu hao 24 pamoja na kuwaapisha Naibu Wasajili 9. Sherehe hizo zimefanyika leo jijini Dodoma. 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akisaini kiapo cha uadilifu cha mmoja wa Naibu Wasajili katika sherehe za kuwakabidhi hati Mahakimu 24 pamoja na kuwaapisha Naibu Wasajili 9. Sherehe hizo zimefanyika leo jijini Dodoma. 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akishuhudia mmoja wa Naibu Wasajili akisaini kiapo cha maadili katika sherehe za kuwakabidhi hati Mahakimu 24 pamoja na kuwaapisha Naibu Wasajili 9. Sherehe hizo zimefanyika leo jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wakati wa sherehe za kuwakabidhi hati Mahakimu 24 pamoja na kuwaapisha Naibu Wasajili 9. Sherehe hizo zimefanyika leo jijini Dodoma.Kushoto kwake ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi  

Baadhi ya Naibu Wasajili na Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa wakiwa katika picha wakati wa sherehe za kuwakabidhi hati Mahakimu 24 pamoja na kuwaapisha Naibu Wasajili 9. Sherehe hizo zimefanyika leo jijini Dodoma. 

No comments: