Friday, July 20, 2018

BILIONI MBILI KUWEZESHA WAHITIMU WA FANI ZA KILIMO SUA KUANZISHA MIRADI YA KILIMO BIASHARA

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG, Morogoro.

Taasisi binafsi ya kusaidia Sekta ya kilimo nchini (PASS) imetenga kiasi cha shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya kuwawezesha Wahitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kuweza kuanzisha miradi ya Kilimo Biashara .

Upatikanaji wa fedha hizo umelenga uanzishwaji wa miradi 100 ya majaribio katika Chuo hicho kupitia mpango wa Maalumu utoaji wa Mazoezi na Majaribio kupitia Vituo Maalum (Incubators)  vyenye lengo la kutoa uzoefu kwa Wajasiliamali Vijana .

Hatua hiyo imebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PASS Bwana Nicomed Bohay baada ya kuingia makubaliano  na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ya  kuwaandaa kwa vitendo Wajasiliamali vijana wahitimu wa fani mbalimbali hususani katika sekta ya Kilimo.

“Baada ya kuona uwepo wa changamoto ya Wahitimu katika masuala ya kilimo pamoja na fani nyinginezo wakishindwa kushiriki katika shughuli za kilimo-biashara baada ya kukosa mitaji PASS kupitia Idara yake ya Agribusiness Innovation Center (AIC)  imeona ije na mpango huu”

Amesema mpango huo  utawawezesha Wajasiliamali vijana kupata mitaji pamoja na nyenzo mbalimbali katika maeneo maalumu kwa lengo la kuwaandaa kuwa Wajasilimali watakao weza kumiliki Miradi ya Kilimo-Biashara.

Bwana Bohay amesema kipaumbele kitatolewa kwa Wajasiliamali Vijana watakaojihusisha na uzalishaji wa mbogamboga kwenye mahema (greenhouse), ufugaji wa samaki, Kuku, mbuzi, usindikaji na viwanda vidogo vya kuzalisha bidhaa zinazotokana na kilimo kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Wenzetu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine (SUA)  wametoa eneo la kutoshereza wa miradi ya Wajasiliamali Vijana kwa lengo la kuhakikisha vijana wetu wanapata mahali pa kuanzia kabla ya kujitegemea” alisema Bwana Bohay.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Sokoine Prof, Raphael Chibunda amesema kuwa ushirikiano huo na Taasisi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo PASS umekuja wakati muafaka na kuwataka wahitimu pamoja na watafiti chuoni hapo kuchangamkia fursa hiyo.

“ Kwetu sisi mradi huu wa kuwalea wahitimu wetu kwa kuwapatia mitaji, nyenzo na ushauri na maeneo maalumu ya kutekeleza kile walichokisoma darasani kwa vitendo ni faraja sana kwani siku zote tumekuwa tukiwaandaa vijana wetu waweze kukabiliana na changamoto za Maisha huko mtaani kwa kutumia elimu waliyoipa hapa chuoni”

“Sasa tunawapa fursa hiyo hapahapa chuoni kabla hawajaingia huko mtaani……,wataondoka hapa wakiwa ni wajasiliamali mahili wa kilimo Biashara na mchango wao Kiuchumi kwa taifa na jamii utaongezeka sana. alisema Prof Chibunda .

Mpango huu unatajwa kuwa suluhu ya changamoto ya ajira kwa Wahitimu hususani wa masuala ya Kilimo ambapo kwa vijana watakao pitia katika vituo maalumu vya uwezeshaji (Incubators) watakuwa na uwezo wa kujiajiri na kujiendeleza kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PASS Bwana Nicomed Bohay akiongea katika hafla ya makubaliano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ya kuwaandaa kwa vitendo Wajasiliamali vijana wahitimu wa fani mbalimbali hususani katika sekta ya Kilimo iliyofanyika chuoni hapo mjini Morogoro. Kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Sokoine Prof. Raphael Chibunda. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG, Morogoro.
Baadhi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Morogoro wakifuatilia kwa makini halfa hiyo.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Sokoine Prof. Raphael Chibunda akitoa shukrani zake za pekee kwa Taasisi binafsi ya kusaidia Sekta ya kilimo nchini (PASS) jinsi walivyojitoa kuwasaidia wajasiliamali kujikwamua katika kilimo kibiashara ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa elimu.
Wageni pamoja na wakuu wa idara mbali mbali katika chuo kikuu cha SUA mjini Morogoro wakimsikiliza kwa makini makamu wa chuo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PASS Bwana Nicomed Bohay (katikati waliokaa) na Makamu Mkuu wa Chuo cha Sokoine Prof. Raphael Chibunda (kwanza kushoto) wakiasaini mkataba wa makubaliano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ya kuwaandaa kwa vitendo Wajasiliamali vijana wahitimu wa fani mbalimbali hususani katika sekta ya Kilimo. Wanaoshuhudia ni wafanyakazi wa PASS na Chuo Kikuu cha SUA.
Wakibadilishana mkataba wa makuabaliano.
Wakionyesha mkataba kwa furaha.
Picha ya pamoja baina yao.
Wakiagana kwa furaha mara baada ya tukio la makabidhiano kumalizika.

No comments: