Na Veronica Simba – Kilosa
Imeelezwa kwamba, jumla ya shilingi bilioni 45 za kitanzania, zimetengwa na Serikali kwa ajili ya kupeleka umeme katika Vijiji 150 vya Mkoa wa Morogoro, kupitia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA.)
Hayo yamebainishwa Jumatatu, Julai 9, 2018 na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Mandela, Kata ya Magole, wilayani Kilosa; ambapo pamoja na mambo mengine, alizindua rasmi uwashaji wa umeme wa REA IIIA, kwa Mkoa wa Morogoro.
Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alisema kuwa, miradi hiyo kwa ujumla wake, katika Awamu ya Kwanza inajumuisha Vijiji 3559 ambavyo vitatumia takribani shilingi bilioni 900 za kitanzania.
“Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais wetu John Magufuli, imejielekeza katika kuhakikisha nishati inafika kwenye maeneo mengi nchini ili kwenda kusukuma uchumi wa viwanda ambao tunaujenga,” alisema.
Akielezea hatua itakayofuata baada ya uzinduzi huo, Naibu Waziri alisema kuwa, ni kuwaunganishia wateja umeme katika maeneo husika, ambapo alisema gharama yake ni shilingi 27,000 tu.
“Serikali imegharamia gharama nyingine zote. Kazi ya mwananchi anayepitiwa na Mradi huu ni kujaza Fomu maalum, ambayo pia inatolewa bure pamoja na kulipia kodi kidogo ya shilingi 27,000.”
Aidha, sambamba na hilo, Naibu Waziri alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania wote, hususan wa maeneo ya vijijini kuwa, umeme utafika kwa wote kwa awamu tofauti, hivyo hakuna haja ya kutoa rushwa kwa yeyote ili kupatiwa huduma hiyo.
Alisema kuwa, Serikali inatambua mahitaji ya umeme vado ni makubwa kwa wananchi, ndiyo sababu inaanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali, ukiwemo wa ujazilizi, ili kuwafikia wote.
Akifafanua kuhusu Mradi wa Ujazilizi, Naibu Waziri alisema kuwa, unahusisha kupeleka umeme katika maeneo ambayo tayari yana miundombinu ya umeme, lakini hayajaunganishiwa nishati hiyo, hivyo Mradi utapita kujaziliza maeneo yaliyorukwa.
Awali, wakizungumza katika Hafla hiyo ya uzinduzi, viongozi wa Serikali wa eneo hilo, akiwemo Diwani wa Kata husika, Alafat Kaunda, waliomba Wigo wa Mradi husika uongezwe ili kuyafikia maeneo yote, ambapo Naibu Waziri alisema kuwa Serikali imezingatia suala hilo na umeme utafika kote kwa awamu.
Mbali na tukio hilo la uzinduzi, Naibu Waziri pia alifanya ziara katika Vijiji vya Mfuru na Madudu vilivyoko Kata ya Mtete wilayani humo, ambapo alizungumza na wananchi na kuwaeleza mipango ya Serikali ya kuwapelekea umeme wa uhakika.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akikata Utepe maalum, kuashiria uzinduzi rasmi wa uwashaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA), kwa Mkoa wa Morogoro. Tukio hilo lilifanyika Jumatatu, Julai 9, 2018 katika Kijiji cha Mandela, Kata ya Magole, wilayani Kilosa.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kilemba chekundu) akifurahia kwa kucheza muziki na wananchi wa Kijiji cha Mandela, Kata ya Magole, Wilaya ya Kilosa, baada ya kuzindua rasmi uwashaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA), kwa Mkoa wa Morogoro. Tukio hilo lilifanyika Jumatatu, Julai 9, 2018.
Mwakilishi wa Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Kusambaza umeme wilayani Kilosa, kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA), Wingod Siyao kutoka Kampuni ya State Grid Electrical & Technical Works Ltd; akitoa ahadi mbele ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kilemba chekundu), kukamilisha Mradi huo kwa wakati. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kijijini Mfuru, Kata ya Kitete, Wilaya ya Kilosa, Jumatatu, Julai 9, 2018.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Mandela, Kata ya Magole, Wilaya ya Kilosa, alipowasili kwa ajili ya kuzindua rasmi uwashaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA), kwa Mkoa wa Morogoro. Tukio hilo lilifanyika Jumatatu, Julai 9, 2018.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mandela, Kata ya Magole, Wilaya ya Kilosa, wakitoa maoni yao kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), wakati wa hafla ya kuzindua rasmi uwashaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA), kwa Mkoa wa Morogoro. Tukio hilo lilifanyika Jumatatu, Julai 9, 2018.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mandela, Kata ya Magole, Wilaya ya Kilosa, wakitoa maoni yao kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), wakati wa hafla ya kuzindua rasmi uwashaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA), kwa Mkoa wa Morogoro. Tukio hilo lilifanyika Jumatatu, Julai 9, 2018.
Mtoto kutoka Kijiji cha Mfuru, Kata ya Kitete, Wilaya ya Kilosa, akisukuma Pampu ya Kisima ili kukinga maji, kama alivyokutwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) kijijini hapo, Jumatatu, Julai 9, 2018. Katika Mkutano wake na wananchi wa eneo hilo, Naibu Waziri alieleza dhamira ya Serikali kuwapelekea umeme wa uhakika ili kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama.
No comments:
Post a Comment