Monday, June 25, 2018

WAZIRI WA AFYA ASEMA HAKUNA EBOLA NCHINI ILA KUNA HATARI YA KUUPATA

*Ataja hatua ambazo wanazochukua kukabiliana nao kote nchini 
*Akiri kuripotiwa homa ya Chikungunya,  Dengue katika Jiji la Dar 

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema hakuna ugonjwa wa Ebola nchini ila kuna hatari ya kuupata.

Hivyo amewahakikishia Watanzania kutokuwa na hofu ha kueleza Serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuweka mashine za kupima ugonjwa huo katika mipaka yote nchini na kuweka vituo vya matibabu kote kila mkoa.

Waziri Mwalim ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumzia homa ya Chikungunya na Dengue ambapo amekiri kuwepo kwa wananchi waliougua magonjwa hayo.Kuhusu Ebola amesema hawajapokea wala kupata  taarifa za mtu yoyote kuugua ugonjwa huo nchini.

"Hatuna mgonjwa wa Ebola ila tupo katika nchi sita ambazo zipo hatarini kupata ugonjwa huo kutokana na kupakana na nchi ya Congo ambayo  iripotiwa watu 43 kuugua Ebola."Pia kuna muingiliano mkubwa wa watu nchini kwetu.Hivyo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) tupo hatarini kuupata,"amefafanua.

Waziri Mwalim amesema Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla tayari wamejipanga kukabiliana na Ebola kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kuunda timu maalum ya kufuatilia.Pia wametenga maeneo ya kutoa huduma za afya kila mkoa iwapo kutabainika kuna mgonjwa wa Ebola amebainika iwe rahisi kupatiwa matibabu.

Ameongeza wametoa mafunzo kwa watoa huduma za afya ikiwa ni mkakati wa kuwalinda iwapo watapokea mgonjwa wa Ebola wakati wa kumhudumia.Akizungumzia homa ya  Chikungunya Waziri Mwalim amekiri wapo watanzania wanne ambao walibainika kuugua ugonjwa huo mkoani Tanga.

"Maana ya Chikungunya ni aliyepinda kutokana na kupinda kwa mgonjwa na kupata maumivu makali.Na ugonjwa huu uliingia nchini mwaka 1952.
"Niwatoe hofu wananchi wote wasiwe na wasiwasi ila kikubwa pale wanapoona kuna mtu ana dalili za ugonjwa awahai kufika hospitali,"amesema.

Pia amesema kuna watanzania 226 ambao waliugua homa ya Dengue ambapo baada ya kubainina walipata matibabu na kupona na hakuna aliyekufa.Amesema wagonjwa hao wote walikuwa wa Mkoa wa Dar es Salaam na hakuna taarifa za mkoa mwingine nchini kuwa na wagonjwa wa ugonjwa huo.

"Tunatoa taarifa hizi kwasababu WHO inatutaka kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa za magonjwa hayo mara kwa mara."Hatuwezi kuficha ni kweli walibainika wagonjwa wa Chikungunya na Dengue na kikubwa tukachukua hatua za kukabiliana.Hakuna aliyefariki dunia,"amesisitiza.

Ametaja dalili za homa ya  Dengue na Chikungunya zinafanana ambazo ni homa za ghafla, kichwaa kuuma na uchomvi mwilini. Wakati mwingine dalili za ugonjwa huo hazina tofauti na Maralia."Ugonjwa huo huenezwa na mbu ambao wanang'ata wakati wa mchana. Sasa kuhusu matibabu ukiwa na malaria unapata dawa. Lakini magonjwa hayo hutubiwa kulingana na dalili.

"Hivyo ni vema mwenye dalili za ugonjwa huo akawahishwa hospitali na habari njema waliougua ugonjwa huo wametibiwa na kupona na hakuna aliyepoteza maisha labda kama Kifo chake hakijaripotiwa,"amesema.

No comments: