Wednesday, June 6, 2018

TFS YAZUNGUMZIA UMUHIMU WA KUTUMIA NISHATI MBADALA ILI KULINDA MAZINGIRA


Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)umesema ipo haja kwa Watanzania kuhakikisha wanatumia nishati mbadala na hasa mkaa mbadala kwa lengo la kulinda mazingira na hasa misitu iliyopo nchini huku akielezea namna ambavyo kasi ya ubaribifu mazingira ikiendelea kuongezeka.

Hayo yamesemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Profesa Dos Santos Silayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani ambapo kwa Tanzania kitaifa yamefanyika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Michuzi Blog, Profesa Silayo amesema takwimu zinaonesha bado kuna uharibifu mkubwa wa mazingira na hivyo kuiomba jamii kutumia nishati mbadala ili kulinda mazingira na kubwa zaidi ameshauri kutumia mkaa mbadala kwa ajili ya kupikia.

Akizungumzia Siku ya mazingira duniani ambayo yameambatana na maonesho ya nishati mbadala, Profesa Silayo amesema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wameshiriki kwasababu msitu inabeba dhamana kubwa katika mazingira na unapozungumza mazingira basi yanaonekana maeneo ya misitu na ekolojia yote.

Ameongeza maonesho hayo yametoa fursa ya kukutanisha wadau mbalimbali na hasa wanaotengeneza nishati mbadala kwa ajili ya mkaa mbadala."Wadau wote ambao wamefika hapa wanaonekana kutoa mbadala wa mkaa badala ya msitu asili ambayo imekuwa ikikatwa kwa ajili ya matumizi ya mkaa na kuni.

"Hivyo mkaa mbadala utasaidia kutunzwa kwa mazingira na kuwa salama na hivyo misitu ya asili itabaki ikiendelea kusaidia kutunza vyanzo vya maji na mambo mengine muhimu,"amesisitiza.Akizungumzia umuhimu wa teknolojia ya nishati mbadala amesema kuwa miti iliyokuwa inakatwa kwa ajili ya mbao badala sehemu kubwa ya miti hiyo kupotea sasa itatumika kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala na hivyo kutapunguza kasi ya ukataji wa miti.

"Hivyo maonesho haya kwate ni muhimu kwani inatoa nafasi ya kuangalia ushiriki wa wadau katika kuangalia namna ya kupunguza kasi ya uharibifu wa mazingira kwa kuanzisha nishati mbadala ya mkaa na tunafahamu hekta 400,000 zinaharibiwa au kupoteza uwezo wake wa kiasilia,"amesema.Kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa kulinda mazingira, Profesa Silayo amesema kuwa zipo hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa ikiwamo ya kupanda miti na kuhakikisha maeneo ambayo yameharibiwa hayaharibiwi zaidi.

Ametoa mwito kwa Watazania kutumia teknolojia ya nishati mbadala kwani imekuwa zaidi, hivyo ni vema wakabadilisha fikra na kueleza changamoto iliyopo watu wengi bado hawajaona umuhimu wa kutumia mbadala ya mkaa."Nitoe rai kwa wananchi tutumie nishati mbadala ya mkaa ili kutunza mazingira na hasa ukataji wa misitu kwa ajili ya mkaa,"ameongeza.

Alipoulizwa kuhusu kasi ya uharibifu wa misitu Profesa Silayo amejibu kuwa kimsingi kasi ya uharibifu wa mazingira ni kubwa na hiyo inatokana na sababu mbalimbali zaidi ya kukata misitu na kufafanua pamoja na hali hiyo bado wanaendelea kuchukua hatua kukabiliana nayo.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania, Profesa Dos Santos akiteta jambo jana akiwa katika maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yaliyofanyika kitaifa Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania, Profesa Dos Santos akiangalia mkaa mbadala ambayo unatengenezwa kwa mabao ambao haujatokana na miti asili baada ya kutembelea banda la Accaso International Ltd jijini Dar as Salaam Jana. (Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii)

No comments: