Wednesday, June 20, 2018

Tanzania sasa mwanachama wa mataifa yanayokataa taka

Na Nelson Nchobe wa LITA

Duniani kote taka ni kero au adha ndogo katika familia kwa sababu moja tu: katika ngazi ya kaya watu ni wachache na taka ni adha ambayo watu hao wachache wanaweza kuimudu. Ili kuondokana na kero hiyo, kwa desturi, wanakaya hukusanya taka na kuziweka eneo moja.

Lakini kaya nyingi katika mtaa au kijiji zinapokusanya taka nakuzirundika eneo moja, ubaya wa taka unapanda daraja; taka inakuwa siyo adha au changamoto ndogo tena bali taka inageuka nakuwa ni tatizo KUBWA; rundo hilo la ataka linakuwa ni jambo la hatari. Hivyo ndivyo ilivyo duniani kote.

Kwa hiyo katika nchi zote duniani ukusanyaji na uhifadhi salama wa taka vimekuwa ni tatizo sugu kwa sababu kila siku taka huzalishwa majumbani, ofisini na viwandani. Taka hizo sasa zimekuwa ni kitu cha hatari kwa uhayi wa mwanadamu na viumbe wengine. Taka zimekuwa jambo la hatari kwa sababu kimsingi taka ni uchafu na uchafu ni chanzo cha magonjwa karibu yote. Lakini si hayo tu, taka zingine ni sumu inayoharibu mazingira na kuangamiza viumbe hai, wakiwemo wanadamu.

Kwa kuwa ukusanyaji na uhifadhi salama wa taka ni tatizo la kidunia, mataifa yote yamekuwa yakihangaika ili kushinda tatizo hilo. Sasa dalili za kupambana vilivyo na tatizo hili kidunia zinaanza kuonekana mwisho wa upeo wa macho kwa sababu kuna juhudi zinazoratibika zikiongozwa na asasi ijukanayo kama Let’s Do It World chini ya taasisi iitwayo Let’s Do It Global Foundation. 

Japo ukusanyaji na uhifadhi salama wa taka nchini Tanzania bado ni ndoto, Tanzania tayari imesajiliwa na taasisi ya Let’s Do It Global Foundation kuwa ni kati ya nchi zenye dhamira ya kweli katika kupambana na taka na kulinda mazingira. Lakini kusajilika tu hakutoshi; kikubwa ni bidii ya kweli ya kukusanya na kuhifadhi salama taka zizalishwazo nchini kwa mujibu wa sheria. Afrika ina nchi 42 ambazo zimesajiliwa katika zoezi hili wanachi wan chi hizo tayari wameishapata mafunzo.

Kihistoria msukumo wa hiari wa kupambana na taka ulianzia katika nchi ndogo ya Estonia huko Ulaya mwaka 2008. Msisimko huu sasa umesambaa duniani na nchi 133 and watu takribani milioni 20 wanashiriki katika ukusanyaji wa hiari wa taka zinazozagaa sehemu zisizo rasmi au taka zilizo nje ya madapo yanayotambuliwa na mamlaka husika katika nchi.

Huko Estonia msisimko huu wa kushangaza tarehe 3 Mei, 2008 uliamsha ari ya watu kuchukia taka katika nchi yao hata watu 50,000 wakaungana pamoja na kuisafisha nchi yao yote katika muda wa saa tano tu! Na Waestonia waliisafisha nchi yao chini kauli mbiu ya Let’s Do it ( yaani basi na tulifanye jambo hili). 

 Wao walikusanya taka bila shuruti kwa mapenzi ya taifa lao, kwa uelewa na dhamira ya kweli ya kujitegemea, pasipokujua kwamba wanawasha moto wa heri utakaosambaa duniani kote na kuzaa asasi iitwayo Let’s Do It World na taasisi mama ya Let’s Do It Global Foundation.

Mtu anaweza kusema, jambo hili liliwezekana kwa sababu Estonia ni nchi ndogo. Hapana. Jambo hili liliwezekana kwa sababu ya umakini wa na ari ya wananchi na umahili wa viongozi waasisi wa jambo hili wakiungwa mkono na serikali kuu na serikali za mitaa za nchi hiyo. Hakuna muujiza mwingine! 

Kama Watanzania tunataka kufanikiwa katika jambo hili ni budi kuwa makini na kuiga umahili wa Waestonia. Maneno na hotuba nzuri vitu vizuri na muhimu, lakini umahili na vitendo ni vitu vizuri na muhimu zaidi. Wananchi wa Estonia walichagua kutenda kwa hiari ndiyo maana wanapigiwa mafano na mataifa 133 kote duniani.

Chini ya uratibu wa asasi ya Let’s Do It World na taasisi Let’s Do It Global Foundation, sasa dunia imechagua tarehe 15 Septemba, mwaka huu kuwa siku ya kukusanya taka kwa hiari duniani. Jambo hili serikali ya Tanzania imelikubali. Kauli ya serikali ya kuunga mkono rasmi jambo hili imo katika barua ya tarehe 28 Februari, 2018 iliyoandikwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Kabla ya kauli hiyo rasmi, tarehe 15 Februari, 2018 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw Selemani Jafo, alizindua kampeni hii ya Let’s Do It-Tanzania na kueleza shahuku yake ya kuona zoezi hili linafanikiwa. Aliueleza mkutano wa wadau kuwa udhibiti wa taka, hasa katika miji ya Tanzania, ni changamoto kubwa sana na kwamba waadhirika wakubwa ni watu maskini. Alieleza kwamba taka zitupwazo ovyo tayari zimeanza kuingia mitoni na baharini na kuchafua vyanzo hivyo vya maji.

Heshima ya Tanzania na umakini wa baadhi ya taasisi zake umeifanya taasisi inayosimamia na kuendeleza moto wa mageuzi ya kuchukia taka, yaani Let’s Do It Global Foundation, kuiteua asasi isiyo ya kiserikali ya Nipe Fagio kuongoza, hapa Tanzania, harakati au kampeni ya kukusanya na kuhifadhi salama taka zilizokusanywa. Kiongozi wa Taasisi hii, Bi Tania Hamilton, anasema asasi yao haikuchaguliwa tu, bali ina historia ya kufanyakazi na raia.

“Tazama suala la kuwaendea watu na kuwa karibu nao, kuwapa elimu na uelewa juu ya taka na kuwaongoza wabadili tabia, ni kazi yetu ya msingi toka 2013. Kwa hiyo ni jambo linaloingia akilini kuona asasi yetu inateuliewa kuwa kiongozi wa shughuli hii nchini. Tunakiri pia kuwa ni heshima kubwa kwetu,” ameeleza Bi Tania. Amesema asasi yake itatumia mtandao wake wa wabai kufanikisha jambo hili. Lakini mafanikio ya jambo hili yatategemea hasa mwitiko wa Watanzania wote, hasa watu wazima.

Tarehe 25 Mei, asasi ya Nipe Fagio iliandaa mkutano Jijini Dar es Salaam kuashiria kukamilika kwa maandalizi ya kampeni kwa upande wa Tanzania.

Katika mkutano huo walitambulishwa wadau mbali mbali na kuelezwa mkakati wa kitaifa wa Let’s Do It Tanzania (LDI-T). Kauli mbiu ya kidunia ya LDI ni “watu kwa ajili ya kuwa na sayari safi” (people for a clean planet).

Bi Hamilton, ambaye peia ni muasisi wa Nabaki Afrika, ameeleza mkutano huo kuwa kampeni hii ya usafi ni endelevu na kwamba nguvu na msingi wake ni harakati ya kujitolea ya kiraia (civic movement). Katika Tanzania miji sita imeteuliwa kwa zoezi hili ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Moshi, na Mbeya.

Bi.Hamilton amesema mwaka 2012 jarida la Forbes liliitaja Dar es Salaam kuwa jiji la 12 kwa uchafu duniani, na kuwaomba wadau kuzingatia elimu ya mazingira kwa wananchi hasa viongozi wa serikali za mtaa. 

Kiongozi huyu pia aligusia suala la kubadili mtazamo wa watu kuhusu taka. Katika kampeni hii kidunia na hapa Tanzania, amesema suala la kubadili mtazamo na fikira za watu kuhusu taka ni muhimu sana na wanalichagiza kama “upofu dhidi ya uchafu” (trash blindness). Ameomba katika harakati hizi, chagizo hili liwe ni mbinu ya kubadili mtazamo na tabia za watu juu ya taka zinazowazunguka. Iwe ni mbinu ya kuwafanya Watanzania wachukie taka.

Sasa, kuliko nyakati nyingine za nyuma, mawazo na mbinu za kutekeleza kampeni ya usafi kitaifa na kidunia vimepatikana. Lengo ni kuzifanya kaya, mitaa na vijiji vichukie taka na kuwa na ari ya kuzikusanya na kuhakikisha zinapelekwa na mamlaka husika katika mahali salama.

LITA ni mtandao wa waandishi wa habariza sayansi, ubunifu na teknolojia.

No comments: