*Azindua kitabu cha Mafunzo ya umeme wa jua
*Atashauri kisambazwe kwa wataalam ,mafundi mitambo
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa amewataka watalaam wote na taasisi zinazohusika na nishati ya umeme-jua kuangalia namna ya kupanua wigo wa matumizi ya nishati hiyo ya jua ambayo ipo kwa wingi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania.
Amefafanua katika kiwango cha Gigawatt 400 za umeme jua zinazotumika duniani kwa sasa bado ni Gigawatt moja tu ndio zimefungwa na kutumika katika nchi za Afrika ,Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa namna mbili.
Mkapa amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anazindua Kitabu cha Mafunzo ya Umeme wa Jua ambacho mtunzi na mwandishi wake ni Godwin Msigwa.Kitabu hicho ambacho kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili kitasaidia kusambaza taaluma na maarifa katika eneo la nishati ya umeme wa jua nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua kitabu hicho ambacho ameomba kisambazwe kwa watalaamu wa nishati ya umeme jua na mafundi mitambo wa umeme jua, amesema pamoja na duniani kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme unaotokana na jua bado nchi za Afrika zipo chini kwenye matumizi.
Mkapa amefafanua kwa mujibu wa taarifa za Mtandao wa jarida la kimataifa la nishati Jadidifu linaloitwa REN 21 ya 2018 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 jumla ya zaidi ya Gigawatt 400 za umeme jua zimefungwa duniani kote kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme ambayo sote tunaifahamu kuwa ni nishati muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha amesema ongezeko la uzalishaji wa umeme duniani kote linatokana na uzalishaji kwa kutumia umeme-jua lilifikia Gigawatt 380 katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2017. "Ongezeko hilo ni la kasi sana, jambo ambalo linaashiria kuwa kuna mwelekezo mkubwa duniani wa matumizi ya nishati ya umeme unaozalishwa kwa kutumia nishati ya jua.
"Kutokana na ukweli huu ni faraja kubwa kuona hata sisi Watanzania tuko pamoja na wenzetu wa nchi nyingine katika kukuza matumizi na teknolojia ya umeme-jua kupitia njia mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa vijana wetu. "Uzinduzi wa kitabu hiki tunaoufanya hapa ni ushahidi tosha wa jitihada zetu kama nchi kuelekea matumizi makubwa ya umeme wa nishati ya jua,"amesema.
Mkapa amesema pamoja na ongezeko hilo nchi zote za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara .Ukweli huo unakinzana na hali halisi ya eneo hilo kwa maana mbili;kwanza nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ndizo zenye maeneo mengi ambayo hayajafikiwa na umeme.
Pili nchi hizo zipo ukanda wa Tropiki ambao una jua jingi muda wote wa mwaka ambalo linaweza kutumika kuzalisha nishati hiyo ya jua. "Nichukue fursa hii kuwataka watalaam wote na taasisi husika zinazoshughulikia masuala ya nishati kuangalia jinsi ya kupanua wigo wa matumizi ya nishati hii ya jua ambayo tunayo kwa wingi katika eneo la Kusini mwa Jagwa la Sahara ikiwemo Tanzania ili kuzalisha umeme wa uhakika na gharama nafuu kwa wananchi wetu.
"Hii itasaidia kuharakisha upatikanaji wa umeme jambo ambalo litaharakisha ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuongeza ajira kwa vijana.Wenzetu wa nchi za Ulaya,China ,Marekani ,Japan na India licha ya kuwa na vyanzo vingine na vikubwa vya uzalishaji umeme kama vinu makaa ya mawe na nyukilia bado wanaendeleza uzalishaji umeme kwa kutumia teknolojia ya umeme jua,"amesema.
Mkapa ametoa mfano nchi ya Ujeruman pekee tayari imefunga zaidi ya Gigawatt 400 za umeme-jua zilizounganishwa kwenye mtandao (grid) wao wa umeme , nchi ya China zaidi ya Gigawatt za umeme-jua.Hiyo inaonesha teknolojia ya umeme huo imekuwa , imekomaa na sasa inaweza kutumika bila mashaka yoyote katika kukidhi mahitaji.
Amefafanua kinachohitajika kwa sasa ni kuweka mipango madhubuti na kuitekeleza lakini ili kufanikisha hilo wanahitaji taasisi muhimu za Serikali kama COSTECH kusimamia mipango hiyo kwa kushirikisha wabia wa maendeleo na watalaam mbalimbali kutoka serikalini na sekta binafsi.
Amesema ushirikishwaji wa tasnia za mafunzo na uandishi wa vitabu kama alivyofanya mtunzi wa kitabu hicho Godwin Msigwa ni muhimu maana mafunzo na vitabu vya teknolojia hiyo vitasaidia kwa kiwango kikubwa katika kufikia malengo ya nchi.
Ameongeza maendeleo endelevu yanategemea mazingira endelevu;mazingira endelevu yanategemea jinsi wanadamu wanavyotumia mazingira hayo katika shughuli za kawaida na uzalishaji mali ikiwa pamoja na rasilimali za uzalishaji umeme.
Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa akizungumza katika uzinduzi wa Kitabu cha Mafunzo ya Umeme Jua Kilichoandikwa na Godwin Msigwa katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Costech jijini Dar es Salaam.
.Mwenyekiti wa Bodi ya Costech, Profesa Makenya Maboko akitoa shukrani kwa Mgeni Rasmi Benjamin Mkapa.
Rais wa Awamu ya Tatu akitoa kitabu baada ya kukata utepe.
Rais wa Awamu ya Tatu akitoa kitabu baada ya kukata utepe.
Baadhi ya Wadau waliohudhuria hafla hiyo
Mtunzi wa Kitabu cha Mafunzo ya Umeme Jua, Godwin Msigwa akieleza malengo ya kitabu hicho na hatua alizozipitia, hafla ilifanyika katika ukumbi wa Costech kijiji Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment