Tuesday, June 19, 2018

TAARIFA YA ZIARA YA WAZIRI MAHIGA NCHINI NORWAY

   
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeihakikishia Serikali ya Norway kuwa inaendelea kuelekeza nguvu zake kwenye kuweka mikakati sahihi ya kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi, ikiwemo nchi ya Norway, ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.

Hayo yamesemwa na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania alipokutana na Bw. Jon Lamoy, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Norway lijulikanalo kwa kifupi kama NORAD mwanzoni mwa ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mjini Oslo, makao makuu ya Norway.

Katika mazungumzo yao, Mkurugenzi Lamoy alimueleza Waziri Mahiga kuwa shirika hilo limekuwa na uhusiano wa karibu na wa kindugu kwa zaidi ya miongo mitano na nchi ya Tanzania. Yeye binafsi na washirika wengi wa Tanzania nchini humo wanasifu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hususan kwenye mapambano dhidi ya rushwa. 

Rushwa inarudisha nyuma maendeleo kwa kuikosesha nchi mapato, hivyo jitihada za Tanzania za kupambana na rushwa, hususan kwenye ukusanyaji kodi, zitawawezesha wananchi wa Tanzania kunufaika na huduma za kijamii na hatimaye kupata maendeleo kwa haraka.

Hata hivyo mkurugenzi huyo alitoa angalizo kuwa nia nzuri ya Serikali ya Tanzania ya kuweka mifumo thabiti ya uwekezaji wenye faida  ukiwemo ule wa sekta ya madini, ni muhimu ikakamilika mapema ili kutoa fursa kwa wawekezaji wapya kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa wakati.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Mahiga alielezea kuwa suala hilo tayari linafanyiwa kazi ambapo pamoja na Serikali kuweka mazingira rafiki  kwa wawekezaji, uwekezaji huo ni lazima uwe na faida kwa Watanzania na kwa maendeleo ya nchi.

“Serikali ya Rais Magufuli imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda. Katika kutekeleza hilo, Serikali imepitia na kurekebisha baadhi ya sheria na mikataba ambayo ilikua inanufaisha upande mmoja. Marekebisho yanayofanyika sasa yanalenga kwenye kuleta faida kwa pande zote mbili yaani win win situation”alisisitiza Dkt. Mahiga.

Kwenye mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi wa Tanzania nchini Norway, Dkt. Wilbroad Slaa mwenye makazi yake nchini Sweden kwa pamoja walielezea kuwa marekebisho hayo, yatakapokamilika, yatarutubisha mazingira ya uwekezaji Tanzania ikiwemo mikataba itakayoridhiwa na Bunge ambayo italeta manufaa kwa pande zote mbili kama zifanyavyo nchi nyingi duniani, ikiwemo Norway.

Awali kabla ya mkutano huo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya STATOIL yenye makao yake makuu Mjini Oslo, ambayo kwa sasa nchini humo inajulikana kama Equinor. Kampuni ya STATOIL Tanzania ni mshirika mkubwa nchini Tanzania kwenye shughuli za utafutaji na upatikanaji wa gesi.

Makamu wa Rais Mtendaji wa kampuni ya Statoil Bw. Lars Christian Bacher alielezea shughuli za kampuni hiyo Tanzania ikiwemo kujenga uwezo wa ndani ya nchi kwa Watanzania kuijua na kuendesha sekta hiyo muhimu kwa ukuaji wa uchumi. Kwa sasa kampuni hiyo inatoa ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili kwa Watanzania kumi kila mwaka kwenye eneo la mafuta na gesi.

Bw. Bacher pia alieleza kuwa uwekezaji wa kampuni hiyo kwenye masuala ya gesi ni wa muda mrefu, na matunda yake yanachukua muda kuonekana. Lakini yakishatoka yataongeza mara mbili upatikanaji wa nishati ya umeme nchini Tanzania, ambapo itaongeza uzalishaji wa viwanda pamoja na faida nyingine nyingi za kiuchumi.

Ujumbe wa Waziri Mahiga ulisifu jitihada za kujenga uwezo kwa Watanzania na kuelezea kuwa hatua hiyo itasadia sana kwenye kutoa elimu kwa Watanzania ili wawe na matarajio sahihi ya matokeo ya shuguli za uwekezaji wa kampuni hiyo nchini Tanzania. Waziri Mahiga aliwasihi kuendelea kujenga uwezo wa kada ya kati ya wataalam wa gesi kwa kushirikiana pia na vyuo vya ndani ya nchi ili utaalamu huo uendelezwe nchi nzima.

Waziri Mahiga yupo nchini Norway kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 18 hadi 20 Juni 2018, kufuatia mualiko wa mwenyeji wake Mhe. Ine Eriksen Soreide, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway. Ziara hiyo imekuja baada ya Tanzania na Norway kusaini makubaliano ya ushirikiano mwaka 2017. 

Mbali na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Mheshimiwa Mahiga na ujumbe wake wanatarajiwa kukutana na makampuni ya Norway yanayowekeza Tanzania pamoja na kuzungumza kwenye Jukwaa la Oslo kuhusu uthabiti wa amani kwenye Eneo la Maziwa Makuu na mchango wa nchi jirani.

Jukwaa la Oslo linakutanisha watu mashuhuri duniani wanaoshughulika na utatuzi wa migogoro duniani akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Mkutano huu hufanyika mara moja kila mwaka kujadili masuala ya utatuzi wa migogoro duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,



Dar es Salaam, 19 Juni, 2018

No comments: