Na Estom Sanga- TASAF.
Wataalam wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kutoka nchini Sudan
Kusini na Nigeria wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa uamuzi wake wa kukuza
sekta hiyo inayolenga kuzikwamua kaya za wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa
wakikabiliwa na umaskini mkubwa wa kipato.
Wataalamu hao ambao wako nchini kuona namna sekta hiyo
inavyotekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF-ambayo inatekeleza
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini –PSSN-wamesema Mpango huo unawagusa moja kwa
moja wananchi hususani wanaoishi katika mazingira ya umaskini uliokithiri.
Wamesema hamasa waliyoiona baada ya kuwatembelea baadhi ya
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Wilaya za Temeke,Ilala
jijini Dar es salaam na Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani katika kujiletea
maendeleo kwa kutumia fursa zilizoko kwenye Mpango huo zimeonyesha kuwa katika
kipindi kifupi cha utekelezaji wa Mpango huo maisha yao yameanza kuboreshwa.
Miongoni mwa mambo yaliyowavutia Wataalam hao ni namna TASAF
inavyoshirikisha Sekta nyingine za serikali kuwafikia Walengwa na uwezo wa Watumishi wa Taasisi hiyo katika
kuwatembelea Walengwa na kuwahamasisha kufanya kazi za uzalishaji mali ili kufikia
malengo na kuboresha maisha ya Walengwa hao.
Aidha suala la ujenzi wa makazi ya Walengwa kwa kutumia
ruzuku wanayopata kutoka TASAF limewashangaza Wataalamu hao kwani katika maeneo
waliyotembelea wamebaini kuwa Sehemu kubwa ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini wamekuwa wakidunduliza fedha na kisha kununua vifaa vya ujenzi wa
nyumba hususani mabati,na saruji ili kuboresha makazi yao.
“Hili ni jambo jema ambalo nchi nyingine barani Afrika
zinapaswa kuliiga kwani suala la makazi bora kwa wananchi wetu ni changamoto
kubwa katika nchi nyingi za kiafrika” amesema mmoja wa Wataalam hao kutoka
Sudan Kusini.Kuhusu suala la Elimu, Afya na Lishe, wataalam hao wamesema
Serikali ya Tanzania Kupitia TASAF imefanya uamuzi sahihi wa kufanya mambo hayo
kuwa miongoni mwa masharti ya kutekelezwa na Walengwa wa Mpango huo wa Kunusuru
Kaya ,mambo ambayo wamesema ni ya msingi katika kujenga rasilimali Watu.
Akizungumza na Wataalamu hao Mkuu wa wilaya ya Kibaha Bi.
Assumpta Mshama amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF
umekuwa chachu muhimu katika kuwahamasisha wananchi kufanya kazi na kujiletea
maendeleo na kusema wilaya yake imejipanga kikamilifu kufuatilia utekelezaji wa
Mpango huo wa aina yake kupata kutekelezwa nchini.
Wataalam hao wa Sekta ya Hifadhi ya Jamiii kutoka Sudan
Kusini na Nigeria wamekuwapo nchini kwa takriban wiki moja kwa lengo la
kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini kupitia TASAF ili kwenda kutekeleza katika nchi hizo.
Baadhi
ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Disunyala wilaya ya Kibaha
wakiwa katika kitalu cha miche ya mboga (nyanya,pilipili hoho)
wanazozalisha kwa lengo la kujiongezea kipato.
Baadhi
ya Wataalam wa sekta ya hifadhi ya Jamii kutoka Sudan Kusini
wakiangalia matuta yaliyolimwa na Walengwa wa TASAF yanayotarajiwa
kupangwa miche ya mboga mboga ikiwa ni mojawapo ya shughuli za
uzalishaji mali ili kujiongezea kipato.
Mmoja
wa Walengwa wa TASAF akiwa amebeba sehemu ya kuku wa kienyeji
anaowafuga kwa kutumia sehemu ya ruzuku anayoipata kupitia Mpango wa
Kunusuru Kaya maskini.
Baadhi
wageni kutoka Sudan Kusini wakiangalia tanki lililojengwa na TASAF
katika kijiji cha Disunyala wilaya ya Kibaha kwa lengo la kuvuna maji ya
mvua yanayotumika kumwagilia bustani ya mboga mboga ikiwa ni mojawapo
ya miradi ya kuwaongezea kipato Walengwa wake.
Pichani
ni baadhi ya Wataalamu wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kutoka nchini Sudan
Kusini wakiwa katika eneo la Shamba darasa la Muhogo lililoanzishwa na
TASAF kwa lengo la kuhamasisha walengwa na wananchi wa eneo hilo
kuzalisha muhogo kwa wingi kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha,Bi. Assumpta Mshama(Watatu kushoto)
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wataalam wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii kutoka Sudan Kusini walimtembelea ofisini kwake kabla ya kwenda
kukutana na Walengwa wa Mpango huo.
No comments:
Post a Comment