Morogoro, June 4, 2018:SERIKALI kwa kushirikikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF wamejipanga kutekeleza mradi mkubwa wa Bwawa la Kidunda, hatua inayotajwa kuwa itatatua kabisa tatizo la uhaba wa maji katika jiji la Dar es Salaam katika kipindi chote cha mwaka.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo katika kijiji cha Kidunda, kata ya Mkulazi Wilaya ya Morogoro Vijijini, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe alisema mradi huo unalenga kufanikisha adhma ya Rais John Pombe Magufuli ya kujenga uchumi wa Viwanda.
"Tunapozungumzia ustawi wa uchumi wa viwanda hususani kwa jiji la Dar es Salaam ni lazima kuwepo pia na upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika katika kipindi chote cha mwaka. Changamoto iliyopo sasa ni kupungua kwa kiasi cha maji katika Mto Ruvu hususani katika miezi ya Septemba na Oktoba, hivyo mradi huu unakwenda kuhakikisha mto Ruvu unakuwa na uhakika wa maji katika kipindi chote cha mwaka'' alisema.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kamwene, mradi huo utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu ni wazo la zamani likiwepo tangu serikali ya awamu ya kwanza chini Mwalimu Julius Nyerere na kwamba utekelezaji wake katika kipindi hiki ni mwendelezo wa adhma ya Rais Magufuli ya kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa.
"Kukamilika kwa mradi huu tafsiri yake ni kwamba huduma ya maji katika la Dar es Salaam inakuwa ni ya uhakika katika kipindi cha mwaka mzima'' alisisitiza.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara ambae pia alikuwa ameongozana na wajumbe wa bodi ya mfuko huo alisema mradi huo pia utahusisha ujenzi wa barabara itakayoanzia eneo la mradi kupitia Ngerengere na kisha kuunganishwa na barabara ya Morogoro -Dar es Salaam katika eneo la Ubena Zomozi ikiwa na urefu wa zaidi ya Km 90.
"Zaidi pia mradi huu utahusisha ujenzi wa daraja la Kidunda litakalounganisha Wilaya ya Kisarawe na Wilaya ya Morogoro vijijini sambamba na kuzalisha umeme zaidi ya Megawatt 20 tutakazozitumia katika mradi wetu wa sukari unaotekelezwa katika eneo hili,'' alifafanua.
Alisema baada ya kujiridhisha na mradi huo waliamua kuingia ubia na serikali ambapo asilimia 60 ya uwezeshaji wa mradi huo itatolewa na NSSF huku serikali ikiwekeza asilimia 40 na kwamba tayari mfuko huo umeshatenga kiasi hicho cha fedha.
"Pamoja na faida tunayotarajia kuipata kupitia uwekezaji katika sekta ya maji, NSSF dhamira yetu pia ni kuwa sehemu ya historia ya kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa maji katika jiji la Dar es Salaam,'' alisema.
Akizungumzia mradi huo Meneja Mipango na Uwekezaji wa Mfuko huo, Xavier Lukuvi alisema unatarajia kuanza katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai mwaka huu na kwamba utekelezwaji wake mbali na faida nyingine pia utaongeza ajira zaidi kwa watanzania ambao pia watakuwa wanachama wa mfuko huo.
"Lakini pia uzoefu na mafanikio tuliyoyapata katika ujenzi wa Daraja la Nyerere lililopo wilaya ya Kigamboni ndio umetusukuma pia kuwekeza katika mradi huu. Katika kipindi hiki cha Uchumi wa Viwanda na Biashara tunaamini kwamba sekta ya maji ni moja uwekezaji mzuri kabisa'' alifafanua.
Naye Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba alisema licha ya mradi huo kuonekana kunufaisha zaidi jiji la Dar es Salaam lakini una faida kubwa kwa wananchi wake kwa kuwa unaambatana na faida nyingi ikiwemo ajira, ujenzi wa barabara, uzalishaji wa nishati ya umeme pamoja na kuongeza pato la taifa kwa ujumla kupitia kodi.
"Tukizungumzia ujenzi wa daraja la Kidunda tu hapo tayari tunamaanisha kwamba wananchi wangu wanaoishi huku Mkulazi hawatalazimika tena kusafiri zaidi ya km 90 kufika Ubena Zomozi kisha zaidi ya km 131 nyingine kwenda Dar es Salaam na badala yake sasa watavuka tu hili daraja na kutokea Kisarawe kisha kuingia Dar es Salaam'' alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephene Kebwe alisema tayari wananchi wameelimishwa kuhusu mradi huo na tayari wameshaanza kuhama kupisha mradi na kwasasa serikali inaangalia namna ya kuhamisha makaburi ya ndugu wa wakazi hao.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwene (alievaa kofia ngumu) akifuatilia maelezo ya Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Prof Felix Mtalo (wa pili kushoto)kuhusu mradi mkubwa wa Bwawa la Kidunda kutoka utakaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF alipotembelea eneo la mradi huo katika kijiji cha Kidunda, kata ya Mkulazi Wilaya ya Morogoro Vijijini mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara (katikati).
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwene (kulia) akibadilishana mawazo na wadau muhimu wa mradi huo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephene Kebwe (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara (wa pili kushoto) Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Attilio Mwang'ingo (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara hiyo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwene (katikati) akiongozana akiongoza msafara wa wadau kuelekea eneo la mradi wakati wa ziara hiyo. Wengine ni pamoja na Mkoa wa Morogoro, Dk Stephene Kebwe (kushoto) pamoja na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba (kulia).
Baadhi ya maofisa waandamizi kutoka NSSF pamoja na DAWASA wakibadilishana mawazo wakati wa ziara hiyo.
Mchoro wa Mradi wa Bwawa la Kidunda.
No comments:
Post a Comment