Saturday, June 16, 2018

SERIKALI MKOANI SIMIYU YAITAKA JAMII KUSHIRIKI KIKAMILIFU KUPINGA MIMBA ZA UTOTONI

Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali Mkoani Simiyu imeitaka jamii kushiriki kikamilifu katika suala la kupinga mimba za utotoni ili kukabiliana na ongezeko la mimba lililofikia 195  kwa wanafunzi wa Shule za msingi na Sekondari katika kipindi cha miaka mitatu  mkoani humo.

 Wito  huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.  Benson Kilangi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa  wa Simiyu, mhe. Anthony Mtaka katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Afrika, yaliyofanyika Kimkoa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nanga B wilayani humo na kuhudhuriwa na wananchi na wadau wa maendeleo lengo likiwa ni kuikumbusha jamii haki za Mtoto.


Kilangi amesema Serikali haitawafumbia macho wale wote watakaowapa mimba wanafunzi hivyo akawataka wananchi kuungana na Serikali katika kulaani na kufichua wale wote wanaojihusisha na suala hilo ambalo linasababisha watoto wa kike kukatisha masomo yao.

“ Mpaka kufikia  mwaka 2016/2017 watoto 195 kati yao 25  wa shule za msingi na sekondari 170 wamepata mimba ndani ya mkoa wetu, hili ni tatizo na sisi hatutamfumbia macho wala kumlea mtu yeyote atakayempa mimba mtoto wa shule, niwaombe wananchi wote muungane na Serikali kulaani kwa nguvu zote mimba kwa watoto wetu wa kike” alisisitiza Kilangi

Katika hatua nyingine Kilangi amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Simiyu kuunda mabaraza ya watoto ambayo yatalenga kusaidia katika kuwapatia watoto fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo stadi za maisha zitakazowafanya wawezekutambua haki zao, kujieleza na kupata mbinu za kukabiliana na  changamoto wanazokutana nazo katika jamii

Baadhi ya wanafunzi wameiomba Serikali kuwachukulia hatua kali wale wote wanaowarubuni wanafunzi wa kike na kuwapa mimba hali inayochangia wanafuzi hao kukosa haki ya msingi ya kupata elimu na kufikia kwenye ndoto zao.

“Watu wanaowapa mimba wanafunzi wapewe hukumu kali maana wanachangia wanafunzi kuacha shule halafu wanashindwa kufikia malengo yao, kwa mfano waliokuwa  na mpango wa kuendelea na elimu ya juu wanaishia njiani sababu ya mimba, mimi naona serikali iwafunge tu” Kabula Masanja mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nanga B.

“Wapo wanafunzi wa kike wamepata mimba kutokana na vishawishi vya baadhi ya watu wasio waaminifu na Serikali imeanza kuchukua hatua kwa wote waliobainika kuhusika na kosa hilo, tunaomba Serikali iendelee kuwachukulia hatua ili tabia hii ikomeshwe kabisa na wanafunzi wa kike wabaki salama “ alisema Luhangija Maduhu mwnafunzi Shule ya msingi Nanga akisoma risala ya watoto wa Mkoa wa Simiyu

Naye Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la World Vision, Ngasa Michael  amesema shirika hilo linaungana na Serikali katika vita dhidi ya mimba za utotoni ambapo wamekuwa wakishirikiana na  viongozi wa dini na Serikali katika jamii hususani  katika maeneo yote ambayo shirika hilo linafanya kazi mkoani Simiyu , huku akibainisha kuwa sasa jamii imeanza kuelewa athari za mimba za utotoni kwa watoto wa kike katika kiafya, kielimu na kijamii


Katika maadhimisho hayo ya Mtoto wa Afrika ya Mwaka 2018 ambayo Kauli Mbinu yake ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Tusiwaache Watoto Nyuma” Shirika la World Vision limekabidhi madaftari,kalamu na vifaa vya Michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa wanafunzi shule 15 Wilayani Itilima.
 Baadhi ya wanafunzi  wa shule za Msingi za kata ya Chinamili wilayani Itilima Mkoani Simiyu wakipita na mabango yenye jumbe mbalimbali mbele ya mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika Kimkoa yaliyofanyika katika Viwanja vya shule ya msingi Nanga B wilayani humo.
 Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.  Benson Kilangi (wa tatu kulia) na viongozi wengine wakipokea maandamano ya watoto(Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu) katika maadhimisho ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa wilayani Itilima katika viwanja vya Shule ya Msingi Nanga B.
 Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi (akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka) akizungumza na wazazi na watoto katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Kimkoa katika viwanja vya shule ya Msingi Nanga B wilayani 
 Kwaya ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Senani wilaya ya Itilima mkoani Simiyu wakitoa burudani ya wimbo katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Nanga B wilayani humo.
 Mtoto Luhangija Maduhu kutoka Shule ya Msingi Nanga B wilayani Itilima akisoma risala mbele ya Mkuu wa Wilaya  hiyo, Mhe. Benson Kilangi (ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka )kwa niaba ya watoto wa Mkoa wa Simiyu, katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa wilayani Itilima katika viwanja vya Shule ya Nanga B. 
 Baadhi ya wazazi na wanafunzi na wazazi wilayani Itilima mkoani Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Benson Kilangi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa  katika viwanja vya Shule ya Msingi Nanga B, wilayani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Bw. Mariano Mwanyigu akitoa taarifa fupi kuhusu Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika, ambayo yamefanyika kimkoa wilayani humo katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nanga B.

No comments: