Thursday, June 28, 2018

NAIBU SPIKA DKT. TULIA MGENI RASMI SIMIYU FESTIVAL 2018

Na Stella Kalinga, Simiyu,

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Tulia Ackson anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio kubwa linalojulikana kwa jina la Simiyu Jambo Festival, ambalo linatarajiwa kufanyika Julai 8 mwaka huu katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, ambapo kwa mwaka huu 2018 linafanyika kwa mara ya pili

Tukio hilo ambalo linafanyika kwa mara ya pili , limebeba vipengele vikuu vinne vya mashindano ambavyo ni mashindano ya mbio za baiskeli, ngoma za asili( wagika na wagalu), mbio fupi kilomita 10 kwa wanaume na wnawake, mbio za uwanjani kwa watoto na uandishi wa insha ambapo kauli mbio yake ni Familia Yangu, Afya Yangu, Furaha Yangu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati ya uzinduzi wa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema kuwa tukio hilo, linalengo la kukuza vipaji kwa vijana wa Mkoa wa Simiyu na kutangaza tamaduni za kabila la Kisukuma na kwamba litahusisha wananchi wote kutoka mikoa mbalimbali.

“Tutakuwa na mashindano ya mbio za baiskeli kilomita 150 wanaume, kilomita 100 wanawake, kilomita 11 watu wenye ulemavu, mbio fupi za kilomita 10 wanaume na wanawake, mbio za watoto za uwanjani, uandishi wa insha kwa wanafunzi na zaidi ya shilingi milioni 22 zitashindaniwa nitoe wito kwa Watanzania wote hususani vijana kuchangamkia fursa hii” alisema Mtaka

“Hii ni fursa pia kwa Wanasimiyu ambao ni wenyeji, sisi tunasema mbio za barabarani na uwanjani ni biashara , mashindano ya baiskeli ni biashara lakini kikubwa zaidi hili ni tukio ambalo litautangaza utamaduni wa Wasukuma wenye mvuto sana ambapo makundi mawili ya Wagika na Wagalu watacheza ngoma za asili na fisi na chatu, nitoe wito kwa watu wote kuja kuona haya” alisisitiza

Mtaka amesema ushiriki katika mashindano ya mbio za baiskeli, ngoma za asili na uandishi wa insha ni bure isipokuwa mbio za kilomita 10 kwa wanawake na wanaume ambazo washiriki watatakiwa kulipa gharama ya shilingi 5,000/= kwa ajili ya usajili.

Naye Joseph Paulo Mwenyekiti chama cha Baskeli Mkoa wa Simiyu amesema kuwa uongozi mzima wa chama chao tayari wamejipanga ipasavyo kupokea na kusajili washiriki ambao watakuwa tayari kushiriki mashindano hayo ya Baiskeli kwa wanawake na wanaume.

Dkt. Amir Ibrahimu mwakilishi wa shirika la UNFPA, Mkoa wa Simiyu amesema shirika hilo limeamua kuwa ni moja ya wadhamini wa Simiyu Jambo Festival waweze kufikisha elimu wananchi wa Simiyu na jamii yote kwa ujumla itakayowasaidia kuona umuhimu wa uzazi wa mpango, kupinga mimba za utotoni na kuhamasika wakina mama wajawazito kujifungua kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua.

Aidha Akizungumzia zawadi kwa washindi watakao shiriki mashindano mbalimbali katika tukio hili la Simiyu Jambo Festival , Afisa Masoko wa Jambo Food Products Company ambao ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Anthony Paul amesema kwa mwaka huu zawadi zimeongezeka hadi kufikia milioni 22.

Naye Mratibu wa mashindano hayo Zena Mchujuko alisema maandalizi yanaenda vizuri hivyo wananchi wote ndani ya Mkoa wa Simiyu na nje ya Mkoa wajitokeze kwa wingi kushiriki mashindano hayo.

Simiyu Jambo Festival mwaka 2018 inadhaminiwa na Jambo Food Products Company, UNFPA, Maswa Standard Chalks, Meatu Milk, NGS Petroleum Limited, Alliance Ginneries Ltd, NGM Gold Mine Limited, SIBUKA na Busega Mazao Limited.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo kuhusu, Simiyu Jambo Festival inayotarajiwa kufanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.
Baadhi ya waandishi wahabari mkoani Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati akizungumza nao kuhusu uzinduzi wa Simiyu Jambo Festival ambayo itafanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.
Afisa Masoko wa Kampuni ya Vinywaji Bariadi ya Jambo (Jambo Food Products Company), Anthony Paul akisoma zawadi zitakazotolewa kwa washindi watakoashiriki katika matukio tofauti ya Simiyu Jambo Festival,ambalo litafanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Bw. Joseph Paulo akitoa maelezo juu ya masuala mbalimbali yahusuyo mchezo wa mbio za baiskeli ambao utachezwa wakati wa Simiyu Jambo Festival , ambalo litafanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia idadi ya watu (UNFPA) Mkoa wa Simiyu Dkt Amir Ibrahimu akitoa taarifa ya ushiriki wa Shirika hilo katika Simiyu Jambo Festival, ambalo litafanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.
Mratibu wa Simiyu Jambo Festival, Bi. Zena Mchujuko akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya tukio hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.
Kutoka kushoto Mwakilishi wa UNFPA Mkoa wa Simiyu Dkt Amir Ibrahimu, Afisa Masoko wa Kampuni ya Jambo, Anthony Paul, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na viongozi wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu wakionesha vinywaji baridi vya Kampuni ya Jambo, mara baada ya mkutano na waandishi wa habari kuhusu Simiyu Jambo Festival tukio linatarajiwa kufanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.
Kutoka kushoto Mwakilishi wa UNFPA Mkoa wa Simiyu Dkt Amir Ibrahimu, Afisa Masoko wa Kampuni ya Jambo, Anthony Paul, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na viongozi wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu wakinywa vinywaji baridi vya Kampuni ya Jambo, mara baada ya mkutano na waandishi wa habari kuhusu Simiyu Jambo Festival tukio linatarajiwa kufanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.

No comments: