Na Estom Sanga- TASAF
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema mchango unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF katika shughuli za maendeleo hususani katika jitihada za kupunguza umaskini wa wananchi ni za kupongezwa kwani unatekelezwa kwa kuzingatia sera za serikali za kupambana na umaskini.
Balozi Seif akizungumza na Ujumbe wa Maafisa Waandamizi wa Benki ya Dunia waliokuwako kisiwani Zanzibar pamoja na mambo mengine kuona namna Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na serikali kupitia TASAFwanavyonufaika , amesisitiza kuwa maisha ya Walengwa wanaonufaika na huduma za Mpango huo yameboreshwa na kuwawekea msingi imara wa kujitegemea.
Amesema TASAF ni kielelezo stahiki cha namna serikali inavyowajali wananchi hususani wanaoishi katika umaskini uliokithiri kwa kuwawekea mazingira ya kufanya kazi za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato huku pia mkazo ukiwekwa katika sekta za Elimu, Afya na Lishe kwa kaya za Walengwa.
Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pia amesema mchango wa kaya za Walengwa katika ukuaji wa uchumi umeanza kuonekana kutokana na shughuli wanazozifanya hasa katika nyanja za kilimo cha Mpunga, bustani ,ususi na ufugaji wa kuku wa kienyeji na mbuzi kwa kutumia ruzuku kutoka TASAF masuala ambayo amesema yanawaongezea kipato .
Akitoa mfano,Balozi Seif amesema miradi mingi iliyoanzishwa na Wananchi katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} na kupata msukumo wa Benki ya Dunia imeleta ukombozi kwa Wananchi walio wengi kisiwani humo.Mapema Mkurugenzi Mtendaji TASAF} Ladislaus Mwamanga amesema kazi kubwa inayofanywa na Wananchi wa Zanzibar kwenye miradi ya Maendeleo kupitia programu zinazosimamiwa na Mfuko huo imeleta mafanikio makubwa.
Mwamanga amesema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko huo itaendelea kuongeza nguvu mara dufu katika kuona kundi kubwa la Wananchi walio na kipato duni hasa Vijijini wanaongezewa nguvu za uwezeshaji ili kuondokana na mazingira magumu yanayowakabili.
Akitoa salamu kwa niaba ya Ujumbe wa Viongozi hao wa Benki ya Dunia Mkurugenzi na Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia Bwana Michal Rutkowski alisema Taasisi hiyo ya Kimataifa ya Fedha haina sababu ya kusua sua katika kuongeza nguvu kwenye miradi ya TASAF inayoendelea vizuri katika utekelezaji wake.
Bwana Michal alisema Uongozi wa juu wa Benki ya Dunia {World Bank} umefurahishwa na jitihada kubwa zinazochukuliwa na Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii inayosimamiwa na TASAF .
Akimkaribisha mgeni rasmi katika tafrija hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia umesaidia kupunguza umaskini kwa baadhi ya Kaya Nchini Tanzania.
Waziri Aboud alisema ushirikiano huo unaendelea kuwa kigezo tosha kinachotoa majibu ya uwepo wa utulivu wa kimaisha kwa Baadhi ya Familia za Kaya hizo jambo ambalo limeleta faraja zaidi kwa watoto wao katika kushiriki vyema masomo yao.
Hii ni mara ya pili kwa Mkurugenzi ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia Bwana Michal Rutkowski na Maafisa wake kutembelea miradi ya maendeleo ya Kijamii inayosimamiwa na Mfuko wa TASAF Nchini Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd akizungumza na Maafisa wa Benki ya Dunia,TASAF na serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya mchango muhimu wa TASAF katika kukabiliana na umaskini nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akishukuru ushirikiano uliopo kati ya SMT,SMZ na Benki ya Dunia uliosaidia kuzikomboa Kaya Maskini Nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga akipongeza usimamizi mzuri wa serikali katika kufanikisha shughuli za taasisi hiyo kwenye hafla iliyohudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Maafisa wa Benki ya Dunia.
Mkurugenzi na Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia Bwana Michal Rutkowski akizungumza kwenye hafla iliyohudhuriwa na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Balozi Seif Ali Idd (walioketi katikati )akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa TASAF na Benki ya Dunia baada ya kutoa hotuba kufuatia ziara ya maafisa hao ksiwani Zanzibar kuona shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
No comments:
Post a Comment