1. KUHUSU MFUKO WA MAENDELEO YA SEKTA YA KOROSHO
Wananchi watambue kuwa, Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho “Cashewnut Industry Development Trust Fund (CIDTF)" ni chombo binafsi ambacho kilinzishwa mwezi Juni, 2010 na kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Miunganisho ya Wadhamini, sura ya 318. Ni Mfuko wa Wakfu tu kama ulivyo mifuko mingi binafsi na sio chombo cha Umma au Serikali. Wadau wa Korosho wa wakati huo waliamua kuanzisha Mfuko huo ili kushirikiana kwa pamoja katika ugharimiaji wa maendeleo ya zao la korosho ikiwa ni pamoja na utafiti, elimu kwa mkulima huduma za ugani, masoko na kuhamasisha ubora wa korosho.
Kabla ya kuanzishwa Mfuko huu, miaka ya 1990, kulikuwa na Mfuko kama huo ambao uliitwa “Cashewnuts Industry Development Trust Fund”. Mfuko huo nao haukuanzishwa na Serikali bali ulikubaliana na Serikali kupata fedha za ushuru wa Korosho zilizokuwa zikisafirishwa nje ya Nchi kiasi cha 2% ya bei ya FoB (thamani ya mzigo uliouzwa kabla ya kusafirishwa). Lakini kutokana ubadhirifu mkubwa wa fedha zilizoingizwa katika Mfuko huo kutoka Bodi ya Korosho Serikali ikasitisha kuupa fedha Mfuko huo na mwanzoni mwa miaka ya elfumbili, Mfuko huo ulikufa ukiwa umepoteza fedha nyingi za umma kutokana na ushuru wan korosho.
Serikali ilipozuia wakulima wasitozwe ushuru kuanzia mwaka 2005, Wakulima, Wabaunguaji, Bodi ya Korosho, Halmashauri za Wilaya na Wawakilishi wa Serikali Kuu walikutana mwezi Mei, 2010, na Randama ya Maelewano ya kuanzisha Mfuko wa Korosho mpya ambao jukumu lake lilikuwa ni kushughulikia maendeleo ya korosho nchini. Wadau hao walikubaliana pia, kuiomba Serikali Kuu kuwa fedha ambazo zilikuwa zinakusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2006 kwa lengo la kusaidia viwanda vya ubanguaji korosho, ziinghizwe kwenye Mfuko huo. Fedha hizo zilikuwa zinakusanywa kwa kwa kuzingatia marekebisho ya Sheria ya Korosho ya mwaka 1984 ambayo iliweka kiasi cha 10% ya ushuru kwa korosho ghafi kwenda nje ya nchi. TRA ilitakiwa itoe 6.5% kwenda Halmashauri za Wilaya zinazolima Korosho na 3.5% kwenda Mfuko Mkuu wa Hazina.
2. VYANZO VYA MAPATO VYA MFUKO HUU
Vyanzo vikuu vya mapato vya Mfuko wa Korohso vimeainishwa katika RANDAMA ya Makubaliano ya uanzishwaji wa Mfuko iliyosainiwa tarehe 10 mwezi Mei mwaka 2010 ni hivi hapa vinne tuvifuatavyo:
(i) Michango ya wakulima wa korosho inayotokana na mauzo ya korosho zao shilingi kumi (10) kwa kila kilo moja ya korosho;
(ii) Michango ya wabanguaji wa korosho shilingi kumi kwa kila kilo moja ya korosho ghafi;
(iii) Michango kutoka serikali kupitia mfumo wa bajeti na matumizi ya serikali kwa muda wa kati (MTEF) wa wizara kupitia huduma na kazi zinazofanywa na Bodi ya korosho kama itakavyotolewa na serikali mwaka hadi mwaka;
(iv) Michango ya mamlaka ya serikali za mitaa itakayotokana na fedha za program ya kuendeleza kilimo cha zao la korosho isiyopungua asilimia tano (5%) kwa kila halmashauri na chanzo kingine kitakachobuniwa na kuamuliwa na halimashauri husika.
MUHIMU: KWENYE MAKUBALIANO YA WADAU, EXPORT LEVY SIO MOJA YA CHANZO CHA MAPATO YA MFUKO WA MAENDELEO YA SEKTA YA KOROSHO WALA BODI YA KOROSHO KWA UJUMLA
3. KUHUSU EXPORT LEVY
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Kabla ya sheria ya Korosho ya mwaka 2009 na Marekebisho yake ya mwaka 2010, Serikali ilikuwa inakusanya ushuru wa korosho inayoenda nje ya nchi kama kawaida, na makusanyo hayo yalikuwa yakifanywa na Taasisi iliyoruhusiwa kisheria kukusanya fedha za umma ikiwemo Bodi Korosho na baadae TRA.
Kwa kuwa Serikali iliagiza mwaka 2005 na 2006 kuondoa Mifuko yote ya mazao ili kutokata ushuru kwenye fedha za wakulima, Hakukuwa na Mifuko yoyote ambayo iianzishwa na Serikali baada ya hapo. Hata sasa, mtu akisoma Sheria ya Korosho ya mwaka 2009, na Sheria za Mazao mengine, hakuna kifungu chochote kinachoanzisha au kutaja Mfuko kama chombo ndani ya Serikali.
Kwa hisani, Serikali iliridhia mwaka 2010, kufanya maboresho ya Sheria ya Korosho ya mwaka 2009 kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2010. Maboresho hayo yaliongeza Kifungu cha 17A ambacho kiliongeza ushuru wa korosho ghafi kutoka 10% na kuwa 15% na kuipa TRA jukumu la kukusanya ambapo 65% iliingizwa kwenye Mfuko wa Korosho (The Cashewnuts Industry Development Trust Fund) na 35% iliingizwa Mfuko Mkuu wa Hazina. Katika Majadiliano ya Bunge wakati wa kutunga Sheria ya Fedha ya 2010 ambayo yapo kwenye Hansard, Mkutano wa Ishirini, Kikao cha Saba tarehe 15 Juni, 2010 (inapatikana katika tovuti ya Bunge: http://parliament.go.tz/polis/
4. KWANINI EXPORT LEVY ILIRUDISHWA KWA WADAU WA KOROSHO?
Sababu muhimu ya wadau wa korosho kurudishiwa Export Levy kusimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya sekta ya Korosho ni kuongeza ajira hapa nchini Tanzania kwa kuanzisha viwanda vya ubanguaji korosho, kufanya tafiti za namna bora ya uendeshaji wa zao hilo na kuhakikisha Tanzania inafanikiwa kutengeneza mapato mengi zaidi kutokana na kufanya hatua kadhaa muhimu za uzalishaji na ubanguaji wa korosho hapa hapa nchini ikiwemo na kuanzisha viwanda vya kuzalisha mbolea na viuatilifu muhimu katika zao la korosho. Korosho ambayo inasafirishwa ikiwa ghafi kwenye nchi nyingine hususan nchi za Asia, zinawasaidia wananchi wananchi wan chi hizo kiuchumi kwa kuwapa ajira na ziada ya mazao yao baki kutokana na usindikaji. Kama nia hii ingetekelezwa kwa ufasaha, sasa nchi ingepiga hatua kubwa, mikoa takribani yote inayolima Korosho ingepunguza tatizo la ajira kwa wananchi wake kwa kuwa wangepata ajira katika viwanda vidogo na vya katii.
Haikuwa lengo la msingi la makusanyo ya ushuru wa korosho ghafi (export levy) kununulia pembejeo (salfa) na kugawa kwa wakulima ili wapulizie mashamba yao. Kwa kifupi, unaweza ukasemaexport levy ililengwa kuwa kama NYAVU ambapo badala ya kumpatia Mkulima kitoweo (mbolea, viuatilifu na kadhalika) ambacho pengine hakimridhishi Mkulima au hakipati kwa wakati, ingeweza kumsaidia Mkulima kutumia NYAVU hiyo kutafuta kitoweo akitakacho yeye ( yaani kuongeza viwanda). Kupitia viwanda ambavyo vingeanzishwa katika Halmashauri pengine zote, mbali na ajira, nchi ingeweza kuongeza thamani ya korosho na pia ingeweza kujipatia fedha zaidi za kigeni.
Lakini kutokana na kubadilisha matumizi ya ushuru huo, sasa,badala ya nchi kuwa na viwanda vya salfa hapa nchini, inaagiza tena kwa bei ya juu (dola za kimarekani) Salfa kutoka nje ya nchi na kuja kuwalangua wakulima. Biashara hiyo ya Salfa inafanya na Makampuni mengi ya kitanzania ambayo mengine yamenufaika vya kutosha na mfumo huu na hivyo hayako tayari kuachia biashara hiyo ya kuwauzia salfa wakulima kwa bei ya juu na pengine ikiwa imepoteza ubora au inayochelewa kuwafikia wakulima.
JE TANGU MWAKA 2010 MPAKA SASA VIWANDA VYA KUBANGUA KOROSHO VIMEANZISHWA VINGAPI?
Bahati mbaya sana Fedha hii inayokusanywa kwa mujibu wa sheria haikutungiwa Kanuni ya namna ya kutumika, hivyo wahusika wa Mfuko wa Korosho wakawa wanaitumia kwa kadri wanavyoona wao inafaa na si kwa mujibu wa lengo la kuanzishwa kwake.
Ndio maana kuanzia mwaka 2011 fedha hii imeanza kusimamiwa na Mfuko huo mpaka mwaka 2016 inakadiriwa zaidi ya Bilioni 140 zimekusanywa lakini hakuna viwanda mahsusi vilivyojengwa kufanya kazi iliyokusudiwa na orosho ghafi zinaendelea kusafirishwa kwenda nje ya nchi hususan India na Vietnam. Hapa Watanzania tujiulize, kwa nini wenzetu wanakuja kununua korosho yetu ghafi na hata ikiongezwa ushuru bado wanaweza kulipia?. Kwa akili ya kawaidfa tu tunaweza kujua kuwa wanaonufaika na korosho ya Tanzania sio wakulima bali ni wale wanaonunua na kuiuza nje na pia Makampuni yanayopata zabuni za kuwauzia wakulima pembejeo. Wakati wakulima wa Mikoa ya Kusini wanaendelea kudidimia, pengine wapo watanzania wachache wanaonufaika na mfumo huu na hivyo kupinga vikali juhudi za Serikali za kudhibiti mapato ya umma.
Ndio maana tangu mwaka 2011 mpaka leo fedha hii inakusanywa lakini bado hakuna viwanda vya uzalishaji wa mbolea na mahitaji mengine ya utunzaji wa zao la korosho vilivyoanzishwa, Zaidi watu wanatafuna hela na kupiga siasa
5. KUHUSU WAKULIMA WA KOROSHO KUDHULUMIWA PESA ZAO
Zipo pia Propaganda zinazoenezwa na wanasiasa wasioitakia mema nchi yetu kwa maslahi yao tu ya kisiasa kuwa wakulima wamedhulumiwa fedha zao za export Levy
Huu nao ni uongo mkubwa sana. Hakuna mkulima yeyote aliyedhulumiwa fedha za export levy.
Kwa sababu ieleweke wazi kwamba EXPORT LEVY sio fedha za mkulima mmojammoja wa korosho. Ushuru wowote unaokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kamwe hauiwi mali ya yule aliyelipa ushuru ule. EXPORT LEVY ni fedha ya umma wote Watanzania wote bila kujali yupo mkoa gani na anafanya shuhuli gani. Export Levy ya korosho ni sawa tu na “Pay as you Earn” anayolipa Mwalimu wa shule ya msingi au sekondari kule kijijini Ukerewe. Export Levy ya korosho ni sawa tu na mapato yanayotokana na usafirishaji wa mazao mengine kama pamba na kahawa nje ya nchi yote yanakuwa mali ya watanzania. Ni sawa tu na kodi wanazokatwa wabunge, askari, watumishi wa umma nakadharika
Kulazimisha kusema wakulima wamedhulumiwa fedha zao Export Levy ni kujilemaza na kuwalemaza wakulima wetu wa korosho kifikra ni sawa na kesho Kampuni kama ya Bakhresa atake fedha yote inayotokana na kodi anazolipa irudishwe kwake imfanyie kazi zake za kuboresha viwanda vyake WAKULIMA WA KOROSHO WAMEPATA STAHIKI YAO HALALI, naam stahiki halali ya wakulima wa korosho imepatikana baada ya wao kuuza korosho zao kwa kadri walivyovuna, hizi nyongeza nyingine ni motisha tu ambazo kimsingi ni jambo la aibu kusimama barabarani mtu mwenye utashi kudai upendeleo kwa kurejeshewa fedha za umma.
6. KUHUSU SERIKALI ‘KUUA’ KILIMO CHA ZAO LA KOROSHO
Ni mwanasiasa mwenye mawazo mafupi tu anayeweza kuamini na kutaka kuwaaminisha watu kuwa Serikali inaweza kukiua kilimo hiki muhimu cha zao la korosho. Serikali iliyoziagiza Halmashauri zinazozalisha korosho kwa wingi kutenga maeneo Zaidi na kuwapa watanzania tena kwa gharama nafuu ili wajikite kulima zao hilo muhimu kibiashara na kuwapatia mbegu bure kwa kampeni maalum ya miaka mitatu mfululizo inawezaje kuliua zao hilo?
Serikali iliyobaini kuwa fedha zilizopangwa kutumika kuboresha zao la korosho kwa kujenga viwanda vya kubangulia korosha hazitumiki kwa mujibu wa malengo na mahitaji kisha kuamua kuzisimamia katika njia ambayo watanzania watanufaika Zaidi na zao hilo kwa kusaidia kuzalisha ajira nyingi Zaidi, kamwe haiwezi kusemwa kuwa inampango wa kuliua zao la korosho
Ninaamini wanaoeneza propaganda hizi wakitumia “UKUSINI” wanafanya hivi makusudi ili kujitafutia mtaji wa kisiasa, wapo ambao wanajiona thamani yao ya kisiasa kwa wapiga kura wao imeshuka na wanatafuta namna ya kuiongeza ama kuirudisha na wapo wanaoamini kuwa hii ni fursa ya wao kujipenyeza katika anga ya siasa hasa za kusini kwa kusambaza uwongo huu bila haya wala soni yoyote.
7. TUHUMA ZA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA ZA KOROSHO
Maelezo yangu hapo juu ya kiasi gani kimekusanywa tangu kuanzishwa kwa mfuko huu mpaka sasa, malengo yake na kilichotokea yanasadifu ni kwa namna wanasiasa na wadau wakubwa wa zao la korosho waliamua wazi kabisa kujinufaisha na zao hili kwa kufanya ubadhilifu mkubwa wa kifedha
Zipo tuhuma za wazi wazi za ubadhilifu unaotokana na manunuzi ya mbolea na dawa za kupulizia kuua wadudu wanaoharibu maua ya korosho kustawi Wapo watu ndani ya bodi ya korosho ambao leo hii ni matajiri kutokana na kuuza mbegu feki, Sulpha mbovu iliyoisha muda wa matumizi, viuatilifu visivyokidhi mahitaji ya wakulima na kutokuwafikishia wakulima mahitaji yao kwa wakati sahihi ili kufanya kilimo.
Zipo pia tuhuma za Mfuko huo kutoa zabuni kiholela kiasi cha kupelekana Mahakamani na kuitia hasara nchi ya mabilioni ya shilingi. Mfano, ipo Kampuni moja tena ya Kitanzania na ni ya Wamiliki kutoka huko huko Kusini ambayo ilichota mamilioni ya fedha za Mfuko wa Korosho na baadae ikabadili jina na kwenda kuomba tena zabuni kwenye Mfuko wa Korosho na ukaipa tena zabuni nyingine ya mabilino ya fedha za Umma. Kutokana na kesi ya ujanja ujanja ya kampuni hiyo, inasadikika kuwa Mfuko wa Korosho ulipoteza zaidi ya Tshs. 300Milioni kwa ajili ya gharama ya kesi hiyo. Kwa mtanzania Mzalendo, alipaswa kuwahudumia wakulima lakini wenye Kampuni hiyo ambao inadaiwa wengine ni miongoni ya wanaohamasisha taharuki, hawaoni huruma kwa matendo yao kwa Watanzania wenzao.
Waliofanya haya ni watanzania wenzetu na tena wanawafanyia watu wa kwao (Kusini) . Kwa mwanasiasa anayeitakia mema nchi hii angejiuliza kwa nini kila mwaka fedha nyingi zinaenda kwenye manunuzi ya salfa? Huko ndiko kuliko na ulaji wa wajanja wachache. Ukitizama Makampuni mengi yanayouza Salfa kwa wakulima sasa, mengine wamiliki wake wanatokea Kanda zinazolima Korosho lakini cha kusikitisha bado wanawaletea wakulima salfa zisizokidhi mahitaji yao, au nje ya msimu kama sio kutoleta kabisa.
8. MGAWANYO WA KITAIFA
Mikwara na kauli za “KUSINI TUMENYONYWA, KUSINI TUMEDHARAULIWA, SAFARI HII LAZIMA TUANDAMANE” na kauli nyingine za namna hiyo huku msingi wa kauli zao ukiwa ni kulilia upendeleo wa kupewa gawio linalotokana na mapato ya watanzania wote ni hatari mno kwa mshikamano wa kitaifa
Leo hii wabunge wa kila eneo wakihamasisha wananchi wao kudai mapato yanayokusanywa na TRA yawanufaishe wao tu na si wengineo kwa visingizo vya namna hii ya wabunge wetu wa kusini kamwe hatutakuwa na taifa liitwalo Tanzania tena. Kwamba kila mkoa wahamaki hatutaki hiki kitoke mpaka tupewe hiki, hatutaki hili liwe mpaka hili likamilike ama hatutaki hili lifanyike mpaka tupate gawio letu, na tukawachekea waendelee kutugawa kwa mtindo huo hatuwezi kufika.
Ndio maana tunaandika kukemea na kukosoa namna ambayo wenzetu wanasiasa wanataka kuitumia kufikia malengo yao ya kisiasa.Malengo ya kisasa kufikiwa kwa hoja za kibaguzi ni hatari sana katika dunia ambayo wananchi wake wanaziunganisha jamii zao bila kujali asili
9. NINI KIMEBADILIKA ?
Kilichobadilika ama kinachotaka kubadilika ni mtunzaji tu wa fedha zilizopangwa kutumika kwa mujibu wa sheria, kwa sasa sheria ilielekeza Fedha zinazokusanywa na TRA kama ushuru wa kusafirisha korosho nje ambazo ni asilimia 15 ya thamani ya korosho au dola mia moja na sita kwa kila tani kulinganisha na ipi itakuwa na thamni kubwa, asilimia 65 ya fedha hizo zitunzwe na Mfuko Mkuu wa Hazina ili ikibidi ziwe na manufaa kwa wananchi wote wa Tanzania.
Tunajua kuwa Mfuko wa Korosho sasa haupo kwa kuwa baada ya tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma, zinazotokana na Export Levy Serikali ilisimamisha shughuli zake. Tunajua kuwa Mdhibiti na na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alishafanya Ukaguzi maalumu kwenye Mfuko huo na amekuta madudu ya kutisha sana kuhusu matumizi fedha za umma. Wenzetu waheshimwa Wabunge wa Kusini wanaodai Serikali imekose, wangeomba wapewe Taarifa hiyo wasome ili waona kama kuna uhalali tena wa fedha za export levy kuingizwa kwenye Mfuko au Bodi ya Korosho. Watanzania wenzetu tumeambiwa walikuwa wanalipana posho za kutisha kupitia fedha za export levy, kulikuwa na mikopo mikubwa ya mamilioni ambayo haijarejeshwa, zabunio zisizofuata taratibu nk. Inasadikikia zaidi ya Bilion 11 zimepotea katika Mfuko huo.
Tunajua katika Ukaguzi kumebainika tangu mwaka 2011 mpaka 2016 Serikali imeuingizia Mfuko huu zaidi ya shilingi Bilioni 146.7 na imebainika pia wadau wa korosho ambao kimsingi ni wakulima na wabanguaji hawajaingiza michango yao ya shilingi 10 kwa kilo ya korosho walizouza ambayo ni zaidi ya Bilioni 4.8 haizkuingizwa kwenye Mfuko. Halafu leo, Wabunge tunasema bado fedha hizo ni za wakulima ambao hata michango yao hawakutoa.
NANI ATATUNZA FEDHA HIZO?
Serikali kama ambavyo ni Msimamizi mkuu wa fedha zote ambazo ni mali ya umma, anawajibu wa kuzisimamia fedha hizo. Ndio maana serikali kupitia wizara ya kilimo imeleta mapendekezo ya kuzikusanya fedha zote zinazotokana na ushuru na mauzo ya mazao ya kilimo na kuzitunza katika akaunti moja na kila wadau wa kilimo husika kupatiwa fedha kwa kadri ya mahitaji, malengo na matakwa ya kimkakati ya zao husika.
MUHIMU PIA KUZINGATIA KUWA MFUKO WA MAENDELEO YA SEKTA YA KOROSHO sio taasisi ya Serikali ni asasi ya kijamii iliyoundwa na wadau wa sekta hiyo LAKINI EXPORT LEVY waliokuwa wanaipokea ni fedha ya Serikali kwa sababu inatokana na makusanyo halali ya kisheria yaliyofanywa na mamlaka ya mapato Tanzania TRA na hivyo ni vigumu serikali kuisimamia fedha ya umma ambayo haipo katika himaya na mamlaka yake
Sasa hivi Serikali inataka kurudisha mamlakani usimamizi wa fedha hii Wanasiasa wale wale ambao kila siku wanalia kuhusu usimamizi mbovu wa fedha za umma leo wanaipinga dhamira njema hii .
Aidha wanasiasa wetu hawa wanasambaza taarifa za uwongo na chuki kuwa Serikali imezuia zaidi ya Bilioni 200 zao za Export Levy huku taarifa za Mamlaka ya Mapato TRA zikionyesha kuwa Export levy kwa mwaka wa fedha 2016/17 ni Tshs 127,743.53 millioni tu na Julai –Mei, 2017/18 ni Tsh 168,464.93 millioni. Tujiulize kuwa, Je wenzetu wametoa wapi hizi tuhuma za Bilioni 200? Au ndio wamezoea kuropoka ropoka tuhuma za fedha kubwa kubwa ili kutengeneza chuki na taharuki?.
10. JE MAZAO MENGINE YA KIMKAKATI NAYO YANA MIFUKO KAMA HUU WA KOROSHO?
Jibu ni hapana,
Tanzania mpaka sasa kuna mazao kadhaa ya kihistoria nay a kimkakati yanayosafirisha na kuuza mazao yake nje ya nchi lakini hayana MFUKO WA UPENDELEO KAMA HUU WA KOROSHO
i. Kanda ya ziwa ni mashughuli kwa ukulima wa PAMBA, na hakika iko mpaka Bodi inayosimamia zao hili la pamba, lakini zao la pamba wala halina Mfuko uliowahi kupokea export levy ya pamba wa namna hii ya Korosho na wabunge wanaotokea kanda ya ziwa hawafanyi siasa za kibaguzi za namna ya wabunge wanaotokea inapolimwa korosho
ii. Ipo pia Bodi inayosimamia zao la PARETO linalolimwa mikoa kadhaa hapa nchini, wala zao hili halina mfuko wa namna ya upendeleo n ahata wabunge wanaotoka maeneo haya hawapigi kelele za kibaguzi kama wanavyotaka kujaribu kufanya hawa wenzetu wa kusini
iii. Lipo zao la KATANI (MKONGE) nalo lina mpaka bodi ya usimamizi lakini wala halina mfuko wa kiupendeleo kama huu wa kusini n ahata wabunge wanaotoka kwenye mikoa inayolima zao hili wala hawatutishi watanzania kwa maneno ya kibaguzi ya namna ambavyo wabunge wa kusini wanafanya
iv. Lipo zao la TUMBAKU na hakika linalimwa kwa ustadi mkubwa katika mikoa kadhaa hapa nchini, zao la tumbaku pia linayo mpaka bodi ya usimamizi na tumbaku inauzwa ndani nan je ya nchi lakini halina mfuko wa upendeleo kama wa korosho na wala sijawahi kuwasikia wabunge wanaotoka mikoa inayolima tumbaku wakienda bungeni kuitishia serikali nyau na hata kutishia ustawi wa mshikamano wa taifa letu uliojengwa na kuasisiwa na wazee wetu kwa upendo na mshikamano mkubwa
v. Lipo maarufu la KAHAWA nalo linalimwa maeneo mbalimbali ya nchi kwa ustadi mkubwa sana, nako mpaka kuna bodi ya kahawa inayosimamia shughuli zake lakini wala zao la kahawa halina mfuko wa aina hii ya kibaguzi na upendeleo kama mfuko wa korosho, na wala wanasiasa na wabunge wanaotoka mikoa hii hawajawahi kufungua midomo yao kuhamasisha ubaguzi na utengano wa kitaifa
vi. Lipo zao maarufu na muhimu la CHAI, nalo lina mpaka bodi yake ya usimamizi lakini halina mfuko wa kiupendeleo wa namna hii na hatujasikia wabunge wake wanaotoka mikoa inayolima zao hili kutupiga mikwara ya kibaguzi kama wanavyotupiga wabunge wetu hawa wa Mtwara na lindi
vii. Ipo mpaka bodi ya NAFAKA NA MAZAO MCHANGANYIKO na wao wanalima mazao muhimu kama mpunga, mahindi, mtama alizeti nakadharika, mazao haya wala pia hayana mfuko wa upendeleo kama iliyokuwa nayo zao la korosho, na wala hatujawahi kusikia wabunge wa mikoa hii wakilalamika barabarani kusema kuwa wanataka wapewe pesa zao
viii. Mazao ni mengi sana na yote yanafaida na umuhimu kwa taifa na uchumi wa taifa kwa ujumla, lakini haiingii akilini kwanini watu wa kusini wanatumiwa na wanasiasa wao kama mfano mbaya katika ujenzi wa taifa kwa kuhubiri siasa za chuki na ubaguzi baina ya taifa ambalo kila mtanzania amekubali kuchanga kila akiwezacho kupitia mishahara, kodi, ushuru natozo mbalimbali kuhakikisha nchi inasonga mbele
Upekee huu unaotaka kulazimishwa na wabunge wetu hawa wa kusini kana kwamba Taifa limewabagua sana wananchi wa mikoa hiyo lengo lake ni nini hasa?
Ni siasa tu au kuna mambo mengine yaliyojificha ndani yake, kama yapo yepi?. Je ni chuki ya kimadaraka na kutokutimia kwa matarajio ya kiasiasa kwa baadhi ya wanasiasa?.
Nawakumbusha kuwa tumetengenezewa taifa likiwa moja lenye mshikamano na mashirikiano baina ya watanzania bila kujali maeneo yao ya asili. Wanasiasa wa kusini, wabunge wa kusini tafadhali msitupasulie taifa letu.
-------------------------
Ndimi,
Habib Mchange
Mwananchi wa kawaida
0762178678
No comments:
Post a Comment