Monday, June 18, 2018

'BAKWATA HAITAKUBALI KUONEWA NA WATU WACHACHE,TUMEDHAMIRIA KUREJESHA MALI ZA WAISLAMU'

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limesema halitakubali kuonewa na watu wachache na limedhamiria kurejesha mali za Waislamu zilizohodhiwa kwa maslahi ya wachache.

Pia limesema waumini wa dini Kiislamu wameridhia kuwa chini ya kiongozi mmoja Sheikh Mkuu wa Tanzania na kuwataka wengine wote kufuata Katiba ya BAKWATA ili kuepusha vurugu.

Kauli hiyo ilitolewa ja juzi jijini Mwanza kwenye Baraza la Idd El Fitri na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA Taifa Sheikh Hassan Kabeke ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuendeleza Quraan na Suna Tanzania (JUQUSUTA).

Alisema BAKWATA hitakubali kuporwa mali za Waislamu na kuwanufaisha wachache ambao wamelifanya baraza hilo kuwa ombaomba wakati lina mtandao mkubwa kuliko taasisi nyingi za dini nchini kwa kuwa lina mtandao wa uongozi hadi vijijini.

Sheikh Kabeke alisema kuwa wamejipanga kurejesha mali za waislamu na kuwataka waumini na viongozi wa dini hiyo kuwa imara na wahakikishe mali zote za Waislamu zinarudishwa lakini wakilegea zote zitakwisha.“Tunataka BAKWATA yenye nguvu itakayopambana na watu wanaopuuza maelekezo ya baraza hilo na hatuna sababu ya kuwa ombaomba wakati tumeweka mizizi hadi vijijini, isipokuwa tunazidiwa na CCM tu.

"Lakini pia tumsaidie Mufti wa Tanzania pamoja na kudumisha amani na utulivu nchini,” alisema Sheikh Kabeke ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza.Awali katika risala yake kwa mgeni rasmi John Mongela, Kaimu Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza Sina Mwagalazi alisema kutokana na uhusiano uliopo baina ya baraza hilo na serikali aliiomba iwape ushirikiano waweze kurejesha mali za Waislamu kwa sababu orodha ya mali hizo zilizohodhiwa na kuwanufaifa watu wachache badala ya Waislamu ipo.

“BAKWATA ndiyo msimamizi wa mali za Waislamu kwa mujibu wa katiba ya baraza hilo.Tunawaomba watu waliojimilikisha mali hizo wajitokeze kwa mazungumzo ili kuwwka mambo sawa,”alisema Mwagalazi.Wakati huohuo Kaimu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Sheikh Hassan bin Almasi aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kuwa siku 30 za mfungo wa mwezi wa Ramadhani liwe darasa la kujitathmini kutokana na semina aliyowapa Mwenyezi Mungu.

Alisema Waislamu waliokuwa kwenye semina (wamefunga) wafanye tathmini je, wataendelea kufanya kama walivyofanya wakati wa mwezi wa Ramadhani, wafikiri vizuri safari yao ya kuondoka duniani je, wataimaliza salama na watakwenda kama ilivyokuwa mwezi Mtukufu?

“Kukutana kwenye baraza la Idd tafsiri yake ni kupata heri ya Ramadhani na tunakusanyika kukumbushana semina aliyotuletea Mwenyezi Mungu na kwamba ameingia kwenye vifua vyetu.Hebu tujiulize semina hiyo itaendelea ama imefika mwisho? ”alisema Sheikh Almasi.

Alisisitiza semina hiyo waliyopewa iwe endelevu kwa kuwa na madarasa ya dini badala ya kuishia kwenye siku ya Idd el Fitri na kuonya misikiti kukosa madarasa kunaifanya safari yao ya kwenda peponi isiwe nzuri sababu watu hawasomi aya za quraan na kusababisha wawatete wengine bila sababu.

“ Mambo hayo ndiyo balaa ya kuigia kaburini na huwezi kufunga wakati unamsengenya mtu ndiyo maana tunataka Waislamu waliokuwa wamefunga kufanya tathmini.Je, wataendelea kuwa kama walivyokuwa kwenye mwezi wa Ramadhani? Alieleza kaimu Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza.

Aidha alidai zipo changamoto za kufarakana kwa waumini wa dini hiyo wanaume na wanawake na kuonya kila mmoja abebe mzigo wake mwenyewe badala ya kuwabebesha wengine.
Sheikh Hassan Kabeke akizungumza kwenye Baraza la Idd jijini Mwanza ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Makutano wa New Mwanza Hotel juzi.Picha na Baltazar Mashaka

No comments: