Na Mahmoud Ahmad,Hanang.
Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la KujengaTaifa(SUMAJKT) linakusudia kujenga hoteli kubwa ya kisasa yenye hadhi ya nyota tano na miradi mingine mikubwa ya kiuchumi wilayani Hanan’g mkoani Manyara kwa lengo la kuinua kiuchumi wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT Brigedia Jenerali Charo Yateri aliyasema hayo jana katika hafla fupi ya kutia saini makubaliano ya kufanya uwekezaji wilayani Hanang kati ya SUMA JKT na Halmashauri ya wilaya ya Hanang yaliyofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri hiyo.
Alisema kuwa wameamua kuwekeza wilayani Hanang kwa kuwa kuna fursa kubwa za uwekezaji ikiwemo upatikanaji wa ardhi isiyo na migogoro,mandhari nzuri ya kuvutia na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo na ufugaji ambapo kupitia miradi yake inayotekelezwa eneo hilo litawafaa .
Kwa mujibu wa Brigedia Yateri Makubaliano hayo ya uwekezaji yatahusika katika ujenzi wa miradi mingine ya kiuchumi ya Karakana ya zana za kilimo, Duka la vipuri vya matrekta, uuzaji wa matrekta,Kituo cha mafuta,Kilimo, Kiwanda cha usindikaji wa nafaka.
Alisema kupitia uwekezaji huo viongozi kutoka makao makuu ya nchi Dodoma watapata nafasi ya kulala katika hoteli hiyo ya kisasa wakiwa na familia zao pasipo kuwa na mwingiliano wa watu wengi jambo ambalo litaongeza mzunguko wa fedha kwa wakazi wa Hanang.
Alisema watu wengi wamekuwa hawajui shirika hilo kuwa ni la umma na la serikali, lina Nyanja nyingi za kufanya kazi pamoja na jamii kuanzia kwenye kilimo ambapo awali liliendesha mashamba yaliyokuwa ya JKT kwa sasa yametengenishwa kwa ajili ya kuzalisha chakula na kuelimisha wananchi kuzalisha chakula kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kulisha vijana wanaojiunga na JKT.
SUMAJKT kama shirika la uzalishaji mali alisema limeanzisha mashamba ambayo yanaendeshwa kibiashara yaani kilimo cha biashara ambacho kinalenga kuongeza thamani ya mazao katika eneo la Chita,Mlundika,Eneo la Songwe,Katavi,Musoma na sasa Hanang ambapo jumla ya ekari 1,000 za kulima mazao ya Ngano,Alizeti na mazao mengine zimetengwa.
“Ni Fursa kubwa kwa upande wa Hanang kushirikiana kwasababu kama SUMAJKT ina kampuni yake ya kuzalisha mbegu bora zitakazotolewa kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji kwa ekari, mbegu nyingi watu wengi wa nje huwa wanachakachua unaweza kutumia mbegu unakuta zinapandwa hapa zinaota na hapa hazioti kwa sababu ya uchakachuaji” Alisema
Alifafanua kuwa shirika la SUMAJKT halitegemei kutengeneza biashara na faida kubwa bali ni kuwasaidia wakulima kwa kutoa mafunzo zaidi na mbegu ili kumkomboa mkulima kwa kuzalisha mazao yenye viwango vinavyokubalika kimataifa na kupata masoko ya uhakika na bei nzuri.
Alitaja shughuli zingine zinazofanywa na shirika hilo kuwa ni uvuvi wa samaki kwenye vizimba, maziwa ambapo elimu ya ufugaji wa samaki imekuwa ikitolewa kujua uhakika wa idadi ya samaki waliozalishwa,watakuwa lini na muda wa kuuzwa.
“Hakuna haja ya kutafuta samaki ambao hujui utawavua wangapi lakini kwenye kizimba utajua idadi yake ya kuvua na hata soko lake utajua utawauza wangapi na kwa muda gani ikiwa pia na kwenye maeneo madogo ya nyumbani ya matanki na mabwawa”
Kuhusu Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyama alisema utalenga kuongeza thamani katika kuanzisha viwanda vya kuchakata na kusindika nafaka za maziwa na mifugo ambapo kwa sasa unatekelezwa katika mikoa ya Iringa eneo la Mafinga na Oljoro- Arusha.
Alisema ujio wa SUMAJKT utapunguza tatizo la ajira kwa vijana na kupitia kampuni ya zana za kilimo na matrekta watu wengi watakopeshwa matrekta kwa bei nafuu ya kulipa kidogo kidogo na matrekta mengine kukodishwa msimu wa kilimo kuweza kulima na kulipa kila msimu.
Kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyojegwa malighafi zake zitatokana na kilimo ili kuongeza thamani ya mazao badala ya kuuza mazao kama yalivyo na kuongeza ajira ili fedha zibaki katika eneo husika badala ya kuzitoa nje na kukuza uwekezaji.
Kwa upande mkuu wa wilaya ya Hanang, Sara Msafiri alisema SUMAJKT itakuwa chachu ya maendeleo ya wilaya hiyo kwa uwekezaji katika kilimo kwani wakazi wa wilaya hiyo wamehamasika kununua matrekta kwa wingi lakini yanapoharibika hupelekwa mkoa jirani wa Arusha kwa matengenezo.
Alisema uwepo wa Karakana ya zana za kilimo na Matrekta utatoa ufumbuzi wa tatizo hilo na kuwafanya wakulima kulima kwa tija.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang Bryceson Kibasa alipongeza hatua hiyo ya uwekezaji na kusema kuwa itaongeza mapato ya Halmashauri.
“Uwekezaji kwa wilaya hii ni kipaumbele chetu tuna maeneo mengi kama shamba la Gawe ambalo ni eneo la viwanda ekari 646 lina hati na mpango wetu ni kutenga maeneo ili mtu anayetaka kuwekeza tunamkaribisha” Alisema.
“SUMAJKT imefungua mlango wapo wawekezaji wengine wanaendelea na mazungumzo, Hanang kuna nafasi za uwekezaji hakuna urasimu na wanaowahi mwanzo wawekezaji kumi tutawapatia maeneo ya kutosha”
No comments:
Post a Comment