Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema atalazimika kuwatumia
polisi kusimamia zoezi la usafi na ujenzi wa vyoo salama katika Kijiji
cha Namasinzi, kata ya Kapenta, bonde la ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga
baada ya wananchi hao kushindwa kujenga vyoo hivyo mbali na elimu ya
umuhimu wa vyoo waliyopewa kwa muda mrefu.
Amesema
kuwa ikifikia hatua hiyo Kijiji hicho kitafungiwa na hakuna atakayetoka
wala kuingia na hatimae kusitisha shughuli za kiuchumi za Kijiji hicho
ambacho ni maarufu kwa kilimo cha mpunga hali itakayopelekea maisha
magumu kwa wananchi hao jambo ambalo asingependa litokee.
Katika
kuhakikisha hali hiyo haitokei Mh. Wangabo alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya
Sumbawanga Dk. Khalfan Haule na timu yake ya usafi ya halmashauri
kuhakikisha wanapita kaya kwa kaya ili kuzibaini kaya zisizopenda usafi
na zisizokuwa na vyoo na kuzichukulia hatua za kisheria kwani kwa
kushindwa kufanya hivyo kipindupindu hakitamalizika katika bonde hilo.
“Sasa
tutatumia nguvu ya dola, ili kuhakikisha kwamba kila mtu anaishi katika
maisha ya usafi wala sio uchafu, na kila mtu ahakikishe kwamba anakuwa
na kiboko Fulani ambacho ni kigumu amuone mtu anachemsha maji, anayaweka
maji yake yanapoa akienda shambani anakwenda na maji mbayo yamekwisha
poa, lakini mkilea lea hivi, waswahili wanasema ukicheka na nyani
unavuna mabua, mabua ambayo tunayavuna ni vifo.” Alisisitiza.
Aliyasema
hayo katika Mkutano wa hadhara alioufanya katika kijiji cha Namasinzi,
Kata ya Kapenta, Wilayani Sumbawanga, kijiji ambacho wananchi watatu
wamefariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na wengine wakiendelea kupatiwa
huduma.
Kwa
upande wake Mganga Mkuu wa hlamshauri ya Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Fani
Musa aliendelea kuishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka misaada
katika bonde hilo ili kuhakikisha wanakabiliana na ugonjwa huo na
kusisitiza kuwa wataendelea kutoa elimu bila ya kuchoka akiamini kuwa
wananchi hao wataelewa wakiendelea kusimamiwa.
“Serikali
imekuwa ikifanya kazi tatu kwa wakati mmoja, tumekuwa tukitoa elimu ya
ugonjwa huu kwa lengo la kuzuia haya yasitokee, lakini yakitokea
tunatumia nguvu kubwa ya kukabiliana na tatizo hili lakini pia serikali
inatoa dawa za kutosha ili kuweza kuponya pia, ugonjwa wa kipindupindu
ni kitendo cha kula kinyesi ambacho ni kibichi, hivyo watu ni muhimu
kujenga vyoo salama,” Alimalizia.
Tangu
kulipuka kwa ugonjwa huo tarehe 6 Mei, 2018 watu 14 wameshafariki na
wengine 221 wakiendelea na kupatiwa matibabu katika kambi za wagonjwa
hao katika bonde la ziwa Rukwa, Wilayani Sumbawanga.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto) akiwa Mkuu
wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (wa kwanza kushoto pamoja na
timu ya afya ya wilaya na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wakikagua
vyoo katika Kijiji cha Namasinzi, Kata ya kapenta, Wilayani Sumbawanga.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akikabidhi tenki la lita
5000 kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Liweliyamvula, Kijiji cha Lumbesa,
Kata ya Kapenta, Wilayani Sumbawanga Paulo Maufi, ikiwa ni miongoni mwa
juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na
kuhifadhiwa sehemu salama, kuepukana na kipindupindu.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akikabidhi dawa za “Water
guard” kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Liweliyamvula, Kijiji cha
Lumbesa, Kata ya Kapenta, Wilayani Sumbawanga Paulo Maufi, ikiwa ni
miongoni mwa juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji safi
na salama, kuepukana na kipindupindu.
No comments:
Post a Comment