Mwenyekiti wa halmashauri ya Mkuranga ,Juma Abeid akizungumza jambo katika kikao cha baraza la madiwani ,wa kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Mshamu Munde.
Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Mkuranga, Filberto Sanga, ametoa tathmini ya awali ya maafa yaliyotokea katika mvua zilizonyesha hivi karibuni ambapo wanafunzi watano wamepoteza maisha kwenye mvua hizo. Aidha ametoa tahadhari kwa watu na watoto kuacha kukatiza katika mito na maeneo hatarishi ili kuepukana na maafa yanayoweza kujitokeza.
Akitoa tathmini hiyo kwa baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, Sanga alitaja kata walizopoteza watoto hao kuwa ni Tambani wanafunzi wawili ambao walizama, kata ya Mianzi, Mwarusembe,Mwandege mwanafunzi mmoja mmoja. Alieleza kuwa, pia ipo miundombinu ya barabara ambayo imeharibika vibaya na haipitiki. Sanga alisema ,wakati mvua ikiwa ni neema lakini mazingira yalishindwa kuhimili ,hivyo wamejipanga kuanza kukarabati baadhi ya miundombinu baada ya mvua kukoma. Alifafanua ,tathmini bado inaendelea na watatoa ukubwa wa maafa yaliyotokea baadae.
Diwani viti maalum Mkuranga, Daima Utanga akizungumza jambo wakati wa kikao cha baraza la madiwani wilayani humo .
WAKATI HUO HUO , Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mkuranga wamemtaka afisa elimu msingi wa halmashauri hiyo, kuweka wazi idadi ya shule zilizotumika kiasi cha fedha mil.29. Fedha hizo ni kati ya mil.151 iliyopangwa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa shule mbalimbali wilayani humo ambapo inadaiwa kutumika mil.29 .
Diwani wa kata ya Mwandege ,Kowero Edward na diwani wa viti maalum Daima Utanga waliibua hoja hiyo, katika kikao cha madiwani kilichofanyika wilayani hapo. Walitaka kujua zilizotumika kwenye ukarabati na ujenzi wa madarasa na shule ngapi kwani taarifa inaonyesha gharama bila idadi ya shule husika, zilizotumika fedha hiyo.
"Tunahitaji majibu ya fedha hizi ,na mchanganuo ili tuweze kujiridhisha" alieleza Daima.
Nae Mwenyekiti wa kamati ya elimu, afya na maji ,Shaban Manda alibainisha ,fedha hizo zimetumika kweli lakini kutokana na suala la idadi ya shule zilipoelekezwa fedha hizo ,watarejea kwenye kamati na kikao kijacho kutaletwa majibu ya uhakika ya hoja hiyo.
Alisema ,afisa elimu msingi wa halmashauri ya Mkuranga ni mgeni ,hivyo kutokana na hilo ,hawezi kuwa na majibu ya moja kwa moja. Manda ,alieleza jumla ya Tsh. mil.151 zimetengwa kwa ajili ya kukarabati na ujenzi ambapo hadi sasa mil.29 pekee.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ,Juma Abeid alisema masuala ya fedha na matumizi yazingatiwe ili kuondoa maswali kwa madiwani. Alisema ,uongozi wowote ni vijiti hivyo hakuna ugeni kwenye ofisi. Abeid aliwataka madiwani wawe na subira ,kuiachia kamati kwenda kukaa ,na kikao kinachofuata watapatiwa majibu ya uhakika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Mkuranga, Mshamu Munde alisema wanajivunia kupata hati safi .
"Hati safi hii tuliyoipata sio sifa ya mtu mmoja ,tunajipongeza wote watendaji,mbunge wetu Abdallah Ulega, madiwani na wilaya ";
",Tusiishie hapa tuendelee na jitihada na kufanya kazi kwa kujituma ili kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya tano" alifafanua Munde.
Aliwaomba watendaji kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi ya wanaMkuranga. Munde alisema ,ushirikiano ndio nguzo pekee katika utendaji kazi hivyo aliwaomba watendaji hao na madiwani kuwa kitu kimoja ili kuleta maendeleo chanja na kuinua uchumi.
No comments:
Post a Comment